Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT.JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA TAIFA WA CHAMA DODOMA, TAREHE 12 MACHI, 2017

Sunday 12th March 2017

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Zanzibar;

Mzee Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM- Tanzania Bara;

Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;

Ndugu Viongozi Wastaafu wa CCM;

Wajumbe wa Kamati Kuu;

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM;

Wageni Waalikwa, Viongozi wa Vyama Rafiki;

Ndugu Wana-CCM Wenzangu;

Mabibi na Mabwana:

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutukutanisha hapa tukiwa wazima. Aidha, nawashukuru ninyi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kuja kwa wingi kuhudhuria Mkutano huu. Hii inathibitisha kuwa mtambua wajibu wenu na kuthamini umuhimu wa Mkutano huu. Nafahamu kuwa baadhi yenu mmesafiri umbali mrefu kuja hapa Dodoma kuhudhuria Mkutano huu; hivyo nawapa pole ya safari.

Napenda pia kutumia fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kuwashukuru Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya iliyowezesha tukutane hapa leo. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, nawashukuru watendaji wa Chama chetu wakiongozwa na jembe letu, Komredi Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chama, kwa maandalizi ya Mkutano huu. Maandalizi ni mazuri sana. Hongereni na ahsanteni sana.

 

Ndugu Wana-CCM Wenzangu;

Kama mnavyofahamu, tarehe 5 mwezi Februari mwaka huu, Chama chetu kilitimiza miaka 40 tangu kilipozaliwa. Miaka 40 sio muda mfupi. Ni kipindi kirefu. Na katika kipindi chote hicho, Chama chetu kimeshika hatamu ya uongozi wa Taifa letu. Kimeweza kusimamia vizuri amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu. Na pia kimewaongoza Watanzania katika harakati za kujiletea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Hayo, bila shaka, ni mafanikio makubwa. Hivyo basi, sisi wana-CCM tunapaswa kujipongeza. Tuzidi kumwomba Mungu na kufanya kazi kwa bidii ili Chama chetu kiendelee kudumu na kubaki madarakani milele daima. Amina.

Napenda pia kutumia fursa hii kuwapongeza wana-CCM wote kwa ushindi mkubwa tuliopata kwenye chaguzi ndogo za Ubunge na Udiwani zilizofanyika hivi karibuni. Ushindi huu tulioupata unadhihirisha sio tu uimara na ubora wa Chama chetu, bali pia imani kubwa waliyonayo Watanzania kwetu. Ninawashukuru Watanzania wote wa vyama mbalimbali kwa kuendelea kuonesha imani kwa CCM, Chama kikongwe na chenye kuheshimika duniani kote.

Niwaombeviongozi waliochaguliwawakafanye kazi kwa bidii na kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu. Na katika hili, napenda niwapongeze na kuwashukuru kwa dhati kabisa, Wabunge na Madiwani wote wa CCM kwa namna ambavyo wanaiunga mkono Serikali katika masuala mbalimbali Bungeni na pia kwenyeHalmashauri zetu. Endeleeni na moyo huo ambao unadhihirisha mapenzi makubwa mliyonayo kwa Chama.

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu Wajumbe na Wanachama wenzangu;

Leo ni sikumuhimu na ya kihistoria kwa Chama chetu. Tumekutana hapa kwa kazi maalum. Kazi ya kufanya marekebisho madogo kwenye Katiba ya Chama chetu, lakini makubwa kwa ajili ya uhai na ustawi wa Chama. Hata hivyo, kabla sijazungumzia suala hilo kubwa ambalo limetuleta hapa leo, napenda nitumie muda mfupi kueleza utekelezaji wa majukumu ya Serikali, hususan Ilani yetu ya Uchaguzi.

Kama mnavyofahamu, sasa yapata mwaka mmoja na ushee tangu Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama chetu kuingia madarakani. Hivyo, ni dhahiri kuwa wana-CCM na Watanzania kwa ujumla wanayo haki ya kufahamu mambo ambayo yametekelezwa na Serikali yao. Kwa ujumla, katika kipindi cha mwaka mmoja tuliokaa madarakani, tumetekeleza mambo mengi. Lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nitaeleza machache.

Suala la kwanza, tumeendelea kudumisha na kuimarisha amani nchini.Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeendelea kulinda usalama na kudhibiti mipaka ya nchi yetu. Vitendo vyenye kutishia usalama, ikiwemo ujambazi wa kutumia silaha tumevidhibiti kwa kiasi kikubwa. Tumezidisha mapambano dhidi ya biashara haramu ya madawa ya kulevya, ambayo nayo ilikuwa inahatarisha usalama wa nchi yetu. Kwa ujumla, nchi ni tulivu na mipaka yetu yote ipo salama. Navipongeza sana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa zinavyofanya za kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa na amani.

Halikadhalika, tumeendelea na jitihada za kudumisha na kuimarisha umoja na mshikamano wetu. Watanzania wamebaki wamoja licha ya tofauti zetu za dini, kabila, itikadi na rangi. Muungano wetu nao unazidi kuimarika. Diplomasia yetu nje ya nchinayo imezidi kukua. Viongozi mbalimbali wa nchi za nje wametembelea nchi yetu. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Makamu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar tumetembelea nchi mbalimbali. Halikadhalika, ndani ya mwaka mmoja uliopita tumeweza kufungua Balozi mpya sita kwenye nchi za Uturuki, Israeli, Sudan, Algeria, Qatar na Korea Kusini.Kupatikana kwa mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga ni ishara nyingine ya kuimarika na kukua kwa Diplomasia yetu.

Kuhusu hali ya uchumi tunaendelea vizuri. Mwaka jana uchumi wetu ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotangualia. Hii imefanya nchi yetu kushika nafasi ya pili kwa ukuaji uchumi Barani Afrika baada ya Cote d’Ivoire. Tumeongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi.  Lakini bado hatujaridhika. Tunataka angalau tuwe tunakusanya shilingi trilioni 1.8. In Sha Allah, naamini tutafika huko, hasa kwa vile tumeazimia kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi.

Tumeimarisha nidhamu ya watumishi wa umma kwa kuwatumbua baadhi yao. Aidha, tumedhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwaondoa watumishi hewa wapatao 19,708 na pia wanafunzi hewawapatao 65,000. Tumepunguza safari za nje zisizo na tija na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa rasilimali za umma. Tayari tumeanzisha Kitengo Maalum cha Mahakama kwa ajili ya kushughulikia makosa makubwa ya rushwa na uhujumu uchumi kama tulivyoahidi wakati wa Kampeni. Kitengo hicho cha Mahakama kilianza kazi mwezi Novemba mwaka jana. Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Wabunge wa CCM kwa kutunga sheria ya kuanzisha Kitengo hiki cha Mahakama. Kama mnavyofahamu, wakati wa mjadala wa kuanzisha Mahakama hii pale Bungeni, wale wenzetu walitoka nje na kususia mjadala. Lakini kwa uimara wa Wabunge wa CCM, mswada ulipitishwa. Nawapongeza sana Wabunge wa CCM. Mmedhihirisha kuwa mnachukia rushwa na ufisadi.

 

Ndugu Wajumbe na Wanachama wenzangu;

Kutokana na ongezeko la ukusanyaji mapato na kufanikiwa kudhibiti matumizi, Serikali imeweza kuwa na fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan ujenzi wa miundombinu ya usafiri na umeme. Mathalani, kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, ambapo takriban asilimia 40 tumeielekeza kwenye miradi ya maendeleo, tumetenga takriban shilingitrilioni 5.47 sawa na asilimia 25.4 ya bajeti yote kwa ajili ya miundombinu ya usafiri. Fedha hizo, ndizo zimetuwezesha kutangaza zabuni ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), ambapo Mkandarasi amepatikana kwa gharama ya shilingi trilioni moja. Ujenzi wa reli hiyo utaanza wakati wowote kuanzia sasa. Tumenunua ndege sita mpya, ambapo mbili zimewasili na tayari zimeanza kutoa huduma. Ndege nyingine moja itakuja mwezi Mei mwaka huu, nyingine tatu zitakuja mwakani, ikiwemo moja kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 250. Ununuzi wa ndege hizi utasaidia sana kukuza sekta yetu ya utalii, ambapo kwa sasa bado tunapokea watalii wachache; chini ya milioni moja na nusu. Tunataka wafikie milioni mbili au tatu.

Tunaendelea naukarabati viwanja vyetu vya ndege, upanuzi wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.Wiki iliyopita nimeshiriki uwekaji wa Jiwe la Msingi la upanuzi wa Bandari ya Mtwara kwa gharama ya shilingi bilioni 137. Aidha, tunaendelea na ukarabati wa meli zetu na mipango ya kununua meli mpya  kwa ajili ya kutumika kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika unaendelea vizuri. Kwa upande wa ujenzi wa barabara na madaraja nao unaendelea vizuri. Barabara kadhaa zimekamilika na nyingine zinaendelea kujengwa. Tatizo la usimamishaji kazi limekwisha kwa sababu Makandarasi wanalipwa fedha zao. Tunataka kuhakikisha nchi yetu yote inafunguka kwa barabara.

Tuliahidi wakati wa Kampeni kushughulikia tatizo la msongamano wa magari kwenye jiji la Dar es salaam. Tayari tumeanza ujenzi wa barabara ya juu pale TAZARA kwa gharama ya shilingi bilioni 100na mwezi huu natarajia kuweka Jiwe la Msingi kwa ajili ya interchange ya Ubungo kwa gharama ya shilingi bilioni 188.715. Napenda pia kuwafahamisha kuwa tumefanikiwa kupata fedha za ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa mwendokasi kwa awamu ya pili hadi ya nne. Barabara zitakazohusika ni za Kilwa na Chang’ombe; Nyerere na Uhuru; pamoja na Babarara ya Bagamoyo hadi Tegeta na Sam Nujoma. Ujenzi wa Barabara hizo unatarajiwa kuanza mwaka ujao wa fedha kwa gharama za shilingi bilioni 820. Katika Jiji la Mwanza, tunaendelea na Ujenzi wa Daraja la Furahisha pamoja na upanuzi wa barabara ya kwenda Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Tunayo pia mipango kabambe ya ujenzi wa barabara hapa Dodoma. Tunataka kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kisasa ili uendane na hadhi ya kuwa Makao Makuu ya Chama na Serikali.

Kwenye sekta ya nishati, tumetenga shilingi trilioni 1.3kwenye bajeti ili kuongeza uzalishaji wa umeme. Bila shaka mtakubaliana nami kuwa Watanzania kwa sasa wameanza kusahau msamiati wa “mgawo wa umeme”. Hivi sasa tunatekeleza miradi mikubwa miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.  Mradi wa kwanza ni Kinyerezi I, ambao tunapanua uwezo wake ili uweze kuzalisha Megawati 335 kutoka Megawati 150 za sasa.  Mradi mwingine ni waKinyerezi II wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 240.  Sambamba na miradi hiyo, Serikali ipo kwenye maandalizi ya ujenzi wa mradi wa Kinyerezi III utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 600, na Kinyerezi IV wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 330

Tunaendelea pia na utekelezaji wa miradi mingine ya kufua umeme kwa kutumia maji, jua, makaa ya mawe, upepo n.k. Tunataka ikifika mwaka 2020nchi yetu izalishe angalauMegawati 5000kutoka kama Megawati1500 za sasa. Aidha, tumeanza utekelezaji wa awamu ya tatu ya programu ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ambapo mwaka huu zimetengwa shilingi bilioni 534.4 kuanza utekelezaji wa mradi huo. Tunataka Watanzania wengi zaidi wapate huduma hii muhimu ya umeme.

Ndugu Wajumbe na Wanachama wenzangu;

Sambamba na hatua hizo za kuboresha miundombinu, tunaendelea na jitihada za kupanua na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii, hususan elimu, afya na maji. Kwenye elimu, kama mtakavyokumbuka, mara tu baada ya kuingia madarakani, Serikali ilipitisha uamuzi wa kuanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 18.77. Tangu kuanza kutekeleza uamuzi huu wanafunzi waliodahiliwa darasa la kwanza  na kidato cha kwanza wameongezeka maradufu. Kama mtakavyokumbuka, ongezeko la wanafunzi lilikuza tatizo sugu na la muda mrefu lililokuwa likiikabili nchi yetu; tatizola upungufu wa madawati katika shule zetu za msingi na sekondari. Lakini kufuatia jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, tulifanikiwa kulimaliza tatizo hilo ndani ya muda mfupi. Hivi sasa kwenye baadhi ya shule zetu kuna madawati mengi kuliko vyumba vya madarasa. Jitihada za kujenga vyumba vya madarasa, na miundombinu mingine kama vile ofisi za walimu, maabara, vyoo na nyumba za walimu zinaendelea. Tunataka watoto wetu wasome katika mazingira mazuri na kupata elimu bora.

 Kwa upande wa vyuo vikuu, tuliongeza bajeti kwa ajili ya ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka shilingi bilioni 340 iliyokuwa imepitishwa na Bunge kwenye bajeti ya Mwaka wa Fedha 2015/2016hadi kufikia shilingi bilioni 473. Hatua hii iliongeza idadi ya wanachuo waliopata ufadhili wa Serikali kutoka 98,300 hadi kufikia 124,358. Katika mwaka huu wa fedha, tumeongeza bajeti ya ufadhili wa wanachuo kutoka shilingi bilioni 473 hadi kufikia shilingi bilioni 483.

Kuhusu afya, tumeendelea na jitihada za kuongeza upatikanaji wa huduma za tiba, ikiwemo madawa na vifaa. Tunaendelea pia na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya pamoja na hospitali za rufaa za mikoa, hususan kwenye maeneo ambayo huduma hizo hazipo. Kwenye bajeti ya mwaka huu, ambapo sekta ya afya imetengewa shilingi trilioni 1.99, tumeongeza bajeti ya ununuzi wa madawa kutoka billion 31 mwaka jana hadi billioni 250. Katika kuhakikisha dawa hizo zinawafikia walengwa, tumeagiza Hospitali zote za Serikali kuanzisha Maduka ya Madawa kwenye maeneo yao.

Kwenye sekta ya Maji, tunaendelea na utekelezaji wa miradi ya kusambazaji maji kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, Musoma, Sumbawanga, Kigoma, Lindi, Sengerema na Chalinze. Miradi mingine mikubwa tunayoitekeleza ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda Dar es Salaam ambalo litagharimu shilingi bilioni 430 na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Mkoa wa Simiyu ambao utagharimu shilingi bilioni690. Halikadhalika, katika Mkoa wa Tabora, tunatarajia kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa miwili; mradi wa kwanza ni wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria utakaogharimu shilingi bilioni 592 na mwingine wa kutoa maji Mto Malagalasi wenye thamani ya shilingi bilioni 720. Kama tulivyoahidi wakati wa kampeni, tunataka ifikapo mwaka 2020, asilimia 85 ya watu wa vijijini na asilimia 90 - 95 ya wananchi wanaoishi mijini wawe wanapata maji safi.  Hii ndiyo sababu katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Wizara ya Maji imetengewa fedha nyingi, takribani shilingi trilioni 1.02.

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu Wajumbe na Wanachama wenzangu;

Licha ya hatua tulizozichukua na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ni dhahiri kuwa yapo masuala ambayo bado yanayohitaji muda kuendelea kuyashughulikia na kuyatatua. Baadhi ya masuala hayo ni matatizo ya umaskini na ukosefu wa ajira, uboreshaji wa huduma za jamii; vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma; uwajibikaji usioridhisha miongoni mwa watendaji wa serikali; migogoro kati ya wakulima na wafugaji, maslahi madogo kwa watumishi n.k.Lakini niseme tu kati ya masuala hayo yote, tatizo la umaskini na ukosefu wa ajira ni kubwa zaidi na linahitaji mbinu endelevu katika kukabiliana nalo.

Suala hili la umaskini na ukosefu wa ajira halipo tu hapa nchini kwetu bali katika nchi zote zinazoendelea. Hata hivyo, napenda niwahakikishie kuwa Serikali imejipanga vizuri kulishughulikia. Tunafahamu njia rahisi ya kukabiliana na tatizo hili ni kujenga viwanda. Tayari tumeanza kuchukua hatua za kujenga uchumi wa viwanda, ambapo mwezi Julai mwaka jana Serikali ilipitisha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021)wenye dhima kuu ya kujenga uchumi wa viwanda. Tunataka ifikapo mwaka 2020 sekta ya viwanda iwe inachangia asilimia 40 ya ajira zote.

Nafarijika kuona kuwa dalili za Tanzania ya viwanda zimeanza kuonekana. Kwa mujibu wa takwimu tulizonazo, kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jumla yaviwanda 2169 vimesajiliwa, vikiwemo vya mbolea, saruji, chuma na usindikaji wa mazao. Wiki iliyopita wakati nikiwa safarini kuelekea Mikoa ya Lindi na Mtwara, niliweka jiwe la Msingi la Kiwanda kikubwa cha vigae pale Mkuranga, lakini nikiwa njiani niliweza kuona zaidi ya viwanda kumi, vikiwa vinajengwa na vingine vimeanza uzalishaji.  Kwa Mkoa wa Pwani pekee kuna viwanda vikubwa 83 na vingine vidogo vidogo vidogo zaidi ya 200. Miongoni mwa viwanda vinavyotarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni ni cha kutengeneza matrekta. Nina imani kuwa kwa kasi hii, baada ya muda si mrefu tutakuwa na viwanda vingi.  Tukiwa na viwanda vingi tutapunguza tatizo la ajira nchini. Na ajira zikipatikana tutaweza pia kukabiliana na tatizo la umaskini.

Halikadhalika, kukua kwa sekta ya viwanda, kutasaidia kuimarisha sekta nyingine za uchumi, hususan kilimo, uvuvi na mifugo, madini, misitu na biashara ambazo nazo zinaajiri wananchi walio wengi. Sekta hizi zikikua zitasaidia sio tu katika kupambana na umaskini na tatizo la ajira bali pia kukuza uchumi wetu. Hivyo basi, Serikali inaendelea na jitihada za kuzikuza sekta hizi, hasa kwa kuhakikisha upatikanaji wa zana bora na za kisasa, pembejeo na ruzuku. Tutaendeleakutenga maeneo ya malisho na ya wachimbaji wadogo wa madini; kutafutamasoko ya mazao pamoja na kuondoa baadhi za kero zinazokwamisha ukuaji na ustawi wa sekta hizo. Mwaka uliopita, tulifanikiwa kupata soko la zao la dengu nchini India na mihogo nchini China. Aidha, tulianza kushughulikia tatizo la utitiri wa kodi kwa baadhi ya mazao, hususan kwa zao la korosho. Matokeo yakesote  tumesikia, sihitaji kueleza.  Tutaendelea kuchukua hatua kama hizo kwenye mazao mengine. Niwaombe tu wakulima kote nchini kuendelea kulima kwa bidii mazao mbalimbali.

Nina uhakika kabisa kuwa, kutokana na mipango na mikakati mizuri iliyopo Serikalini, tutaweza kushughulikia masuala na kero nyingine ambazo bado zinawasumbua wananchi. Wito wangu kwa wana-CCM wenzangu, kwanza tujitahidi kutangaza mafanikio yaliyopatikana. Tuzidi pia kuisimamia Serikali kutekeleza yale yote tuliyowaahidi wananchi. Aidha, tushirikiane katika kuhamasisha sekta yetu binafsi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo nchini, hususan ujenzi wa viwanda. Binafsi nafurahi sana kuonakuwa sekta binafsi imeitikia vizuri wito wa Serikali wa kujenga viwanda. Lakini tuzidi kuwahamasisha. Tunawahitaji wafanyabiashara kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na shughuli nyingine za maendeleo.

Sambamba na hilo, napenda kuwahimiza Watanzania wote kufanya kazi kwa bidii. Kazi ni utu. Kazi ni msingi wa maendeleo. Lakini pia kazi ni uhai. Bila kufanya kazi tutakufa ama kwa njaa au kukosa huduma muhimu. Nawaomba pia kuwahimiza Watanzania wenzangu tuendelee kulipa kodi. Nafurahi tangu tumeingia madarakani, mwamko wa wananchi kulipa kodi umeongezeka. Naomba tuendelee na moyo huo. Kodi mnazozilipa ndizo zinaiwezesha Serikali, kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii. Nawahakikishia kuwa hakuna senti hata moja itakayotumika vibaya. Fedha zote zitatumika kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote. Hakuna mtu atakayejinufaisha nazo binafsi.

 

 

 

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu Wajumbe na Wanachama wenzangu;

Naomba sasa nizungumzie suala muhimu ambalo limetuleta hapa. Kama mnavyofahamu, Chama chetu kimekuwa na utamaduni wa kujitathmini kila wakati na kufanya mageuzi. Mageuzi hayo ndio yamekuwa chachu yenye kukifanya Chama chetu kiendelee kudumu, kizidi kuimarika na kwenda na wakati.Kutokana na utamaduni huo huo ambao umejengeka ndani ya Chama chetu, Halmashauri Kuu yetu ya Taifa ilikutana mwezi Desemba mwaka jana na kupokea Taarifa ya Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Baada ya kupitia taarifa hiyo ambayo ilibainisha changamoto na mapendekezo ya kushughulikia, Halmashauri Kuu ilipitisha maazimio yenye lengo la kukiwezesha Chama chetu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuendana na mazingira ya sasa ya ushindani.

Baadhi ya maazimio yalianza kutekelezwa mara moja lakini mengine yalihitaji kufanyika kwanza kwa marekebisho ya Katiba yetu ndipo yaweze kutekelezwa. Hii ndiyo sababu kubwa ya kuitisha Mkutano Mkuu huu Maalum. Tumeuitisha ili kuwapa fursa ninyi wajumbe kupitia marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa, muyatafakari na ikiwezekana muyapitishe.Natambua kuwa Katibu Mkuu wetu, Mzee Kinana, baadaye leo atawasilisha waraka utakaofafanua kwa kirefu kiini, shabaha na maeneo tunayotaka kuyafanyia marekebisho. Kwa sababu hiyo, mimi nitajikita zaidi kueleza malengo na madhumuni ya mabadiliko tunayotaka kuyafanya. Yapo mengi, lakini nitataja machache makubwa.

Kwanza kabisa,marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa na Halmashauri Kuu yanalenga kuboreshamfumo na muundo wa Chama chetu na Jumuiya zake. Kama mnavyofahamu, mfumo na muundo wa Chama tulionao, licha ya kuwa umetupatia mafanikio kwa miaka 40 iliyopita, una mapungufu. Mathalani, kuna mwingiliano mkubwa wa kimajukumu baina ya taasisi za Chama na Jumuiya zake. Mwingiliano huo ndiyo umechangia Chama chetu kuwa na watendaji wengi wanaotekeleza majukumu yanayofana na hivyo kuleta migongano. Sambamba na hilo, hivi sasa ndani ya Chama chetu kumeibuka vyeo ambavyo vinanguvu katika maamuzi lakini havipo kikatiba, kama vile Makamanda wa Vijana au Washauri wa Jumuiya. Na wapo baadhi ya watu wametumia vyeo hivyo kwa maslahi yao binafsi. Hivyo basi, marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa yanalenga kuondoa mapungufu niliyoyataja kwa kuboresha mfumo na muundo wa Chama. Tunataka Chama chetu kiwe na muundo mdogo kitaasisi, wenye kuonesha mgawanyo wa majukumu na uwajibikaji (yaani pawe distribution of duties and clear chain of command), kuanzia ngazi ya juu ya Chama hadi chini. Na pia uoneshe uhusiano kati ya Chama na Jumuiya zake.Vyeo vyote ambavyo havipo kikatiba, tunataka kuviondoa.

Pili, Halmashauri Kuu inaleta kwenu mapendekezo ya marekebisho ya Katiba yenye lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi wa Chama. Naamini mtakubaliana nami kuwa utendaji kazi wa Chama chetu umekuwa ukishuka sana, hasa uchaguzi ukimalizika. Hali hii inatokana na Chama kujiweka pembeni katika kusimamia Serikali na kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo. Baadhi ya viongozi na watendaji wa Chama wanabaki kuwa watazamaji na walalamikaji badala ya kuwa mfano wa utendaji bora kwa wananchi. Mathalan, hivi sasa mvua zinanyesha karibu nchi nzima lakini nina uhakika ni viongozi wachache wa Chama wanawahamasisha wananchi kulima. Hivyo basi, tunataka tuboreshe utendaji kazi wa Chama, ikiwemo kwa kukifanya Chama kuwa na watumishi wachache lakini wenye moyo na weledi wa kukitumikia vizuri. Aidha, tunataka kupunguza idadi ya vikao vya Chama na wajumbe wa vikao hivyo kwa lengo lakuongeza ufanisi na kutoa fursa kwa watendaji kutumia muda mwingi kutekeleza shughuli za Chama.

Tatu, mabadiliko tunayotaka kuyafanya yanalenga kukipeleka Chama kwa wananchi. Waasisi wetu, walianzisha Chama hiki  kwa ajili ya kuwatetea wananchi wanyonge, hususan wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi n.k. Hivyo, tunataka tukirudishe Chama kwa wananchi badala ya kubaki kwa viongozi na matajiri wachache. Tunalenga kuimarisha utendaji kazi wa Chama kwenye ngazi ya matawi na mashina. Kama mnavyofahamu, kwenye matawi na mashina ndiko kwenye wanachama na wananchi wengi. Hivyo, tukiimarisha ngazi hizo itakuwa rahisi kwetu kufahamu matatizo yanayowakabili wanachama na wananchi na hivyo kuweza kutafuta majawabu yaharaka. Hii ndiyo sababu nyingine pia tunalenga kupunguza idadi ya vikao vya Chama na wajumbe wake. Tunataka viongozi na watendaji wetu watumie muda mwingi kushughulikia matatizo ya wananchi badala ya kufanya vikao ambavyo vinatumia fedha nyingi huku tija yake ikiwa ni ndogo. Vikao hivyo ndivyo wakati mwingine vimekuwa vikitumika kutengeneza  majungu ndani ya Chama na hata kupanga mikakati ya kuwazuia baadhi ya watu wenye sifa kugombea nafasi za uongozi kwenye Chama.

Nne, mabadiliko tunayotaka kuyafanya yana nia ya kukifanya Chama kijitegemee kiuchumi. Nyote mnafahamu kuwa Chama chetu kina rasilimali nyingi. Lakini mnajua pia jinsi gani rasilimali hizo hazikinufaishi sana Chama chetu. Licha ya utajiri wa rasilimali tulionao, tumeendelea kuwa ombaomba. Hivyo basi, mabadiliko tunayotarajia kuyafanya ni pamoja na kujenga uwezo wetu wa kitaasisi wa kuweza kutambua, kutunza na kutumia vizuri rasilimali za Chama. Yeyote atakayetaka kujinufaisha na rasilimali za Chama, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Haya niliyoyaeleza ni baadhi tu ya malengo na madhumuni ya mabadiliko tunayokusudia kuyafanya. Yapo mengine mengi. Napenda kusisitiza kuwa, mabadiliko ndani ya Chama chetu si kitu kigeni. CCM imekuwa ikifanya mabadiliko mara kwa mara kulingana na mazingira na mahitaji. Mabadiliko haya tunayoyapendekeza ni ya 16 tangu Chama chetu kizaliwe mwaka 1977. Mabadiliko haya, kama mengine yaliyopita, yanalenga kukiimarisha Chama chetu kimfumo, kimuundo, kiungozi, kiutendaji na kirasilimali. Tunataka kukipa Chama chetu uwezo wa kustahimili mazingira ya sasa na yajayo kwa lengo la kukifanya kiendelee kubaki madarakani kwa miaka mingi ijayo. Mabadiliko haya ni kwa maslahi ya wananchama wetu wa sasa na wajao. Hivyo, niwaombe wajumbe wa Mkutano Mkuu myaunge mkono na kuyapitisha. Nafahamu wapo wanachama wenzetu watakaoguswa na mabadiliko haya kwa namna moja au nyingine, lakini kutokana na mapenzi ya dhati kwa Chama na kuweka maslahi ya Chama mbele, naamini wataunga mkono. Na sisi hatutawaacha.

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu Wajumbe na Wanachama wenzangu;

Kabla sijahitimisha hotuba yangu ninayo masuala mawili ya mwisho ambayo ningependa kuyaeleza. Jambo la kwanza, mtakumbuka katika Mkutano Mkuu uliopita nilieleza dhamira yangu ya kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma kabla ya mwaka 2020. Napenda kuwahakikishia kuwa tumedhamiria kwa dhati kabisa kuhamia Dodoma. Nasema hivi, tutahamia Dodoma. Na utekelezaji wa dhamira hiyo tayari umeanza. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, Waziri Mkuu pamoja naViongozi Wakuu wa Wizara zote, yaani Mawaziri, Naibu Mawaziri; Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na baadhi ya Wakurugenzi na watumishi wameshahamia Dodoma. Aidha, vikao vya Makatibu Wakuu na Baraza la Mawaziri kuanzia mwezi Machi, vyote vitafanyika hapa Dodoma. Kwa maneno mengine, maamuzi makuu ya Serikali yameanza kufanyika Dodoma. Mimi nami najipangapanga kuhamia Dodoma. Mabalozi na Wawakilishi wa nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa nao wameonesha nia ya kuanza kuhamia Dodoma. Hivyo, nina uhakika kuwa lengo letu la kuhakikisha Serikali yote imehamia Dodoma ifikapo mwaka 2020 litatimia.

Jambo la pili ni suala la uchaguzi ndani ya Chama chetu. Kama mnavyofahamu, mwezi ujao tutaanza uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali wa Chama chetu. Uchaguzi huo ni muhimu sana kwa uhai na ustawi wa Chama. Hii ni kwa sababu viongozi tutakaowachagua ndio watakaotuongoza kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Tukichagua viongozi wazuri tutakirahisishia Chama chetu kupata ushindi kwenye chaguzi hizo, lakini tukichagua wasiofaa tutapata shida. Hivyo basi, natoa wito kwa wanachama wenzangu kuchagua viongozi waadilifu, wachapakazi, wenye mapenzi ya dhati kwa Chama chetu  na wanaokubalika na wananchi.

Tusichague watu kwa fedha zao au umaarufu wao. Natambua chaguzi ndani ya Chama chetu zimekuwa zikigubikwa na matatizo ya rushwa na udanganyifu. Nilishasema na napenda kurudia tena leo, chini ya uongozi wangu, rushwa haitakuwa na nafasi katika kuchagua viongozi wa chama. Nasisitiza kuwa msisumbuke kuhonga. Najua na ninaelewa namna ya kushughulika na wote watakaojihusisha na vitendo hivyo. Kama Serikalini hatuvumilii na tunawatumbua, hatutashindwa kuchukua hatua kama hizo ndani ya Chama. Nawasihi Sekretarieti kujipanga vizuri kusimamia uchaguzi huu.  Hatutaki uchaguzi huu uvurugike kwa kuingiza mapandikizi, mamluki au kwa namna yoyote ile. Atakayebainika kuvuruga uchaguzi wetu, hatua kali za kinadhamu na maadili zitachukuliwa dhidi yake.

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu wajumbe na Wanachama wenzangu;

Napenda kuhitimisha kwa kuwashukuru tena wajumbe kwa kuhudhuria mkutano huu. Nawasihi tufanye uamuzi wa busara wa kupitisha mapendekezo yatakayoletwa kwenu. Narudia tena, mapendekezo hayo ni muhimu kwa ajili ya uhai, ustawi na mustakabali mzima wa Chama chetu.

Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Wenyeviti na viongozi wetu mbalimbali wastaafu waliokuja kujumuika nasi hapa. Nafurahi kumwona Mzee Mwinyi, Mzee Kikwete, Makamu wa Rais Mstaafu Mzee Bilal; Rais Mstaafu wa Zanzibar Mzee Karume; Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mzee Warioba, Mzee Macelela, Mzee Dkt. Salim na Mzee Pinda; pamoja na Spika Wastaafu, Mama Makinda na Mzee Kificho. Tunawashukuru sana. Uwepo wenu mahali hapa leo unadhihirisha upendo na mapenzi ya dhati mliyonayo kwa Chama hiki. Napenda kuwahakikishia kuwa sisi vijana ambao mmetuachia dhamana tunawapenda, tunawahitaji na tutaendeleakutumia busara na uzoefu wenu. Maana kama msemo wa kiswahili usemavyo, “uzee ni dawa”.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM umefunguliwa rasmi.

 

Mungu Ibariki Tanzania!

         Kidumu Chama cha Mapinduzi!

       “Asanteni sana kwa Kunisikiliza”