Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA ALIYOINDAA KWA AJILI YA MABALOZI NA VIONGOZI WA TAASISI ZA KIMATAIFA KUKARIBISHA MWAKA MPYA 2017 IKULU, DAR ES SALAAM, 10 FEBRUARI, 2017

Friday 10th February 2017

 

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje

na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;

Mheshimiwa Meja Jenerali Mstaafu Edzai Chimonyo,

Balozi wa Zimbabwe na Kiongozi wa Mabalozi nchini;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;

Mabibi na Mabwana:

 

Awali ya yote, napenda niwashukuru sana, Waheshimiwa Mabalozi, kwa kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria hafla hii. Nawakaribisheni nyote hapa Ikulu na naomba mjisikie kuwa mko nyumbani. Aidha, napenda nitumie fursa hii hapa mwanzoni kabisa, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania niwatakie Waheshimiwa Mabalozi pamoja na familia zenu Heri ya Mwaka Mpya 2017. Naomba pia mnifikishie salamu zangu za Heri ya Mwaka Mpya 2017 kwa Viongozi, Wananchi pamoja na watumishi wa Taasisi  mnazoziwakilisha.

Waheshimiwa Mabalozi;

Kama ilivyo ada, hafla hii hutoa fursa kwetu sote kutafakari masuala ya mwaka uliopita na kupanga mikakati ya mwaka mpya. Napenda kutumia fursa hii, kueleza kuwa kwa nchi yetu, mwaka uliopita ulikuwa wenye matukio mengi. Licha ya kuwa ulikuwa mwaka wa kwanza tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, tulipata mafanikio makubwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Tuliweza kudumisha amani, umoja na mshikamano wetu. Nchi yetu iliendelea kuwa ya amani na kimbilio la watu wengi. Watanzania tulibaki kuwa wamoja na Muungano wetu ulizidi kuimarika. Tuliongeza jitihada za kuimarisha demokrasia na utawala bora. Tumezidisha vita dhidi ya wala rushwa, ujangili na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Kama nilivyokuwa nimeahidi kipindi cha kampeni zangu, tayari Serikali imeanzisha Kitengo Maalum cha Mahakama kwa ajili ya kushughulikia rushwa kubwa na ufisadi.

Kiuchumi pia mwaka 2016 ulikuwa ni mzuri kwa nchi yetu. Tulikuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake ulikua kwa kasi Barani Afrika. Taasisi mbalimbali za kimataifa zinazoshughulikia masuala ya uchumu, ziliitaja nchi yetu kushika nafasi ya pili kwa ukuaji uchumi baada ya Cote d’Ivoire. Uchumi wetu ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotanguliwa. Mfumko wa bei nao ulishuka kutoka asilimia 6.5 mwezi Januari hadi kufikia asilimia 4.5 mwezi Septemba 2016, ingawa uliongezeka kidogo kufikia asilimia 4.8 mwezi Novemba 2016. Tuliongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi.

Waheshimiwa Mabalozi, Mabibi na Mabwana;

Mwaka jana nchi yetu ilipitisha Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21). Dhima kuu ya Mpango huu ni kujenga misingi imara ya sekta ya viwanda ili kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira yetu ya Maendeleo inavyoelekeza. Utekelezaji wa Mpango huu utatumia takriban shilingi trilioni 107. Kati ya fedha hizo, Serikali inatarajiwa kutoa shilingi trilioni 59 sawa na takriban shilingi trilioni 11.8 kwa mwaka. Utekelezaji wa Mpango huo, umeanza mwezi Julai mwaka jana ambapo Serikali ilipitisha bajeti ya shilingi trilioni 29.5.  Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tumeelekeza asilimia 40 ya bajeti yote kwenye shughuli za Maendeleo.

Kama mnavyofahamu, ili kujenga uchumi wa viwanda unahitaji miundombinu imara ya usafiri na nishati ya umeme. Hivyo, tumezielekeza fedha nyingi kwenye sekta hizo. Tumetenga shilingi trilioni 5.47 kwenye sekta ya ujenzi na shilingi trilioni 1.2 kwenye nishati. Hii imetuwezesha kuendelea au kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga, maji pamoja na miradi ya umeme. Tuliweza pia kununua ndege mpya sita lengo likiwa ni kuimarisha usafiri wa anga na hatimaye kukuza sekta ya utalii nchini.

Maeneo mengine ambayo tumeyapa kipaumbele ni uboreshaji wa huduma za jamii, hususan elimu na afya. Tumetenga shilingi trilioni 4.77 kwa ajili ya elimu na maendeleo ya sayansi na shilingi trilioni 1.99 kwenye sekta ya afya. Matokeo yake ni kwamba udahili kwa darasa la kwanza, kidato cha kwanza na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu umeongezeka maradufu. Tumeboresha pia huduma za afya, hususan upatikanaji wa vifaa tiba na madawa. Tumetoa kipaumbele pia katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, maji n.k.

 

Waheshimiwa Mabalozi;

Kwenye masuala ya diplomasia nako tulipata mafanikio makubwa mwaka jana. Nchi yetu ilitembelewa na viongozi wa mataifa kadhaa. Na kwa upande wetu, mimi pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tuliweza kutembelea baadhi ya mataifa. Ziara hizi zilikuza zaidi uhusiano wetu. Tuliweza kusaini mikataba kadhaa ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali. Aidha, mwaka jana tuliweza kufungua Balozi mpya kwenye mataifa kadhaa ambayo hatukuwa na uwakilishi.

Sambamba na kuimarisha uhusiano na mataifa ya nje, tumeendelea kutoa mchango wetu kupitia taasisi mbalimbali za kimataifa ambazo sisi ni wanachama. Mwaka 2016 tulipata heshima ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti  wa Chombo kinachosimamia Siasa, Ulinzi na Usalama cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Troika Organ on Politics, Defense and Security). Kupitia taasisi hizo, tumeweza kutoa michango mbambali, hususan kwenye usuluhishi wa migogoro nchi za Burundi, DRC, Lesotho na Sudan Kusini. Aidha, vikosi vyetu vimeendelea kulinda amani nchini Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa ujumla mwaka uliopita ulikuwa wenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Na kwa hakika, naweza kusema kuwa mafanikio mengi tuliyopata mwaka uliopita yalitokana na ushirikiano wenu mkubwa mliotupa. Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru Mabalozi wote mnaowakilisha nchi na taasisi za kimataifa hapa nchini kwa ushirikiano wenu mkubwa.

Mheshimiwa Kiongozi wa Mabalozi;

Waheshimiwa Mabalozi,

Mabibi na Mabwana;

Pamoja na mafanikio hayo niliyoyataja, mwaka jana pia ulikuwa na changamoto. Tena nyingi tu. Lakini mojawapo kubwa ni kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuzipongeza nchi zote, ambazo tayari zimeridhia Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Sisi Tanzania tayari tumeanza mchakato wa kuridhia Mkataba huo, ambao tuliusaini mwezi Aprili mwaka jana. Nina matumaini makubwa kuwa endapo nchi zote zitasaini, kuridhia na kutekeleza Mkataba huo, tutaweza kukabiliana na tatizo hili la mabadiliko ya tabianchi.

 

Waheshimiwa Mabalozi,

Katika mwaka huu tulioanza, Serikali na wananchi wa Tanzania wamejipanga kuendelea na utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo, hususan Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Tunataka ifakapo mwaka 2020 uchumi wetu ukue kwa asilimia 10, sekta ya viwanda itoe ajira kwa asilimia 40 ya Watanzania, pato la kila Mtanzania liongezeke na hatimaye ikifika mwaka 2025 tuwe nchi ya kipato cha kati. Tumepanga pia kukuza sekta yetu ya utalii, ambayo inayoongoza kwa kutupatia fedha nyingi za kigeni. Hivyo basi, tunawakaribisha wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza kwenye sekta ya viwanda hapa nchini. Nchi yetu ina fursa nyingi za ustawi wa viwanda, ikiwa ni pamoja na malighafi za kutosha, nguvu kazi na soko kubwa. Tunawakaribisha pia wawekezaji kuja kushirikiana nasi katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya uchumi. Mwaka huu tunaanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma na ambayo itafika nchi za Burundi na Rwanda. Hii ni  fursa nzuri ya uwekezaji, hivyo, tunawaomba Waheshimiwa Mabalozi mtangaze fursa zilizopo hapa Tanzania kwa wananchi wenu.

 

Sambamba na kutekeleza mipango hiyo ya maendeleo, tumejipanga katika mwaka huu, kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na mataifa pamoja na taasisi mnazowakilisha. Na pia mataifa ambayo hayana uwakilishi hapa nchini. Aidha, tutaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na mwaminifu wa taasisi zote ambazo sisi ni wanachama, ikiwemo EAC, SADC, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Nchi zisizofungamana na Upande wowote, Umoja wa Mataifa, n.k. Tutaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ambayo imepitishwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa, ikiwemo Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika pamoja na Agenda 2030 kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

 

Mheshimiwa Kiongozi wa Mabalozi;

Waheshimiwa Mabalozi,

Mabibi na Mabwana;

 Ningependa nikomee hapa. Lakini kabla sijahitimisha, ninalo jambo moja la mwisho ambalo sina budi nilieleze. Mwaka 1973, Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya nchi yetu kutoka hapa Dar es Salaam kwenda Dodoma. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali, uamuzi huo haukuweza kutekelezwa kikamilifu. Mwaka jana mwezi Julai, wakati nikipokea Uenyekiti wa Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niliahidi kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wangu, nitahakikisha Serikali itahamia Dodoma. Napenda niwaarifu Waheshimiwa Mabalozi kuwa Serikali itahamia Dodoma katika kipindi hicho. Tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na baadhi ya Wizara na taasisi zimeanza kuhamia Dodoma. Hivyo, nina uhakika ahadi hiyo itatimia. Kwa sababu hiyo, niwaombe Waheshimiwa Mabalozi nanyi muanze kufikiria kuhamia Dodoma. Serikali imejipanga kuanza kutoa viwanja kwa ajili yenu hivyo anzeni kuleta maombi yenu. Nafurahi kuwa baadhi ya Balozi tayari zimeanza kuleta maombi yao.

 

Napenda kuhitimisha kwa kuwashukuru tena kwa kukubali mwaliko wangu. Nawashukuru pia kwa jitihada mbalimbali mazozifanya za kuimarisha ushirikiano kati yetu. Nawahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwenu ili muweze kutekeleza majukumu yenu ipasavyo.

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”