Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA RELI YA KATI KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA PUGU, DAR ES SALAAM, TAREHE 12 APRILI, 2017

Wednesday 12th April 2017

Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa,

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Yesamin Eralp, Balozi wa Uturuki nchini;

 

Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi wa Benki ya Dunia

         nchini Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro;

 

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Mstahiki Meya na Waheshimiwa Madiwani mliopo;

Ndugu Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

 

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kushuhudia uwekaji Jiwe la Msingi la Mradi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge). Aidha, namshukuru Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Prof. Mbarawa pamoja na uongozi mzima wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kunialika ili nishiriki nanyi katika  shughuli hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa wana-Pugu. Hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza nanyi tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo basi, nawashukuru kwa kura zenu nyingi mlizonipigia. Nawaahidi kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya Watanzania wote.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 yapo mambo tuliahidi. Yalikuwa mengi lakini moja wapo ilikuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafiri. Ahadi ni deni. Nafurahi leo tupo hapa kushuhudia uwekaji Jiwe la Msingi la Mradi huu wa reli. Hakuna shaka, tukio hili ni la kihistoria kwa nchi yetu.

 

Kama mnavyofahamu, nchi yetu kwa sasa inazo njia mbili kuu za usafiri wa reli. Reli ya Kati, ambayo sehemu yake kubwa, ilijengwa enzi za ukoloni wa Ujerumani na Uingereza kati ya mwaka 1899 hadi 1929. Na Reli ya TAZARA iliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China mwanzoni mwa miaka ya 1970, ambayo inatuunganisha na ndugu zetu wa Zambia. Hivyo basi, reli hii mpya tunayotaka kuijenga itakuwa ya tatu. Hili ni jambo la kihistoria kwa nchi yetu na hasa kwa kuzingatia kuwa mipango na mikakati yote ya kuijenga reli hii tumeibuni sisi wenyewe. Na hata utekelezaji wake, tumejipanga kuusimamia wenyewe, ingawa tunawakaribisha washirika mbalimbali kuja kushirikiana nasi.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ujenzi wa reli hii una umuhimu wa pekee na manufaa mengi kwa nchi yetu. Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ametaja baadhi ya manufaa yatakayoletwa na reli hii. Lakini naomba mniruhusu nirudie kutaja kwa uchache baadhi ya manufaa:

(i)           Kwanza kabisa, reli hii itarahisisha usafiri wa mizigo na abiria hapa nchini na kwenda nchi jirani za Burundi, Rwanda, DRC, Uganda na Sudan Kusini. Kama mnavyofahamu, reli hii inajengwa kuanzia hapa Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Mwanza na Kigoma na baadaye inatarajiwa kuelekea nchi za Burundi na Rwanda. Na kwa kuwa Kigoma na Mwanza ni karibu na nchi za DRC, Uganda na Sudan Kusini, itarahisisha usafiri kwenda nchi hizo pia.

(ii)         Pili, reli hii itakuza biashara kati ya nchi yetu na nchi hizo nilizozitaja. Moja ya kikwazo kikubwa cha biashara miongoni mwa nchi za Afrika ni ukosefu au ubovu wa miundombinu ya usafiri. Ukosefu/ubovu wa miundombinu ya usafiri unakadiriwa kuongeza gharama za biashara kwa asilimia 40 Barani Afrika. Hii ndio sababu mchango wa Bara la Afrika kwenye biashara duniani (Africa’s share in the global trade) ni chini ya asilimia 5. Na hii ndiyo sababu pia biashara miongoni mwa nchi za Afrika (intra-African trade) ni chini ya asilimia 15, wakati kwenye Mabara mengine ni kati ya asimilia 40 na 60. Hivyo, kwa kujenga reli hii, biashara kati ya nchi yetu na mataifa mengine itaongezeka maradufu.

(iii)       Tatu, ujenzi wa reli hii utakuza sekta nyingine za uchumi nchini. Kama mnavyofahamu, ustawi wa sekta za viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi, madini na utalii hutegemea sana kuwepo kwa usafiri wa uhakika. Mathalan, reli hii itakapokamilika itawezesha malighafi kama vile pamba, samaki, ngozi, nyama, maziwa, madini, mbao, asali, n.k, kusafirishwa kutoka maeneo yanakozalishwa kwenda kwenye maeneo ya viwanda. Na bidhaa zitakazozalishwa viwandani zitafika kwenye masoko kwa wakati. Reli hii pia itakuza utalii. Kama mtakumbuka, miezi kama miwili au mitatu iliyopita, mlishuhudia watalii kutoka Afrika Kusini wakija hapa Dar es Salaam kwa kutumia reli ya TAZARA. Hivyo, reli hii ikikamilika, mtalii ataweza kutoka nchini Afrika Kusini hadi Mikoa ya Kigoma na Mwanza.

(iv)       Nne, ujenzi wa reli hii utasaidia kutunza barabara zetu. Kama mnavyofahamu, nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kujenga barabara. Zaidi ya kilometa 17,000 zimejengwa na binafsi nafurahi nilishiriki katika ujenzi wa barabara hizo. Lakini barabara zetu nyingi zinaharibika ndani ya muda mfupi kutokana na kutumika kusafirishia mizigo mizito. Tafiti nyingi zimethibitisha kuwa usafiri wa reli ndio sahihi katika kusafirisha mizigo mikubwa. Una gharama nafuu na unawezesha kusafirisha mzigo mkubwa umbali mrefu kwa kipindi kifupi. Mathalan, treni zitakazotumia reli hii zitaweza kusafirisha mzigo wa tani 10,000 kwa mara moja sawa na malori ya semi-trella 500 yenye uwezo wa kubeba tani 20 kila moja. Hivyo basi, hii itasaidia sana kutunza barabara zetu.

(v)         Tano,ujenzi wa reli hii utaongeza upatikanaji wa ajira nchini. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, inakadiriwa kuwa, wakati wa ujenzi wa reli hii, takriban watu laki sita watapata ajira, wakiwemo 30,000 ambao watapata ajira za moja kwa moja.  Aidha, reli hii itakapokamilika, inatarajiwa kutoa ajira takriban milioni moja kupitia viwanda na kukua kwa sekta nyingine za kiuchumi, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini, utalii, nk.

 

Hizi ni baadhi tu ya faida zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa reli hii. Zipo nyingine nyingi. Hivyo basi, niwasihi Watanzania wenzangu kujipanga ili kuweza kunufaika na mradi huu.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ujenzi wa reli hii yenye urefu kilometa 1,219 umegawanywa kwenye vipande vitano. Kipande cha kwanza ni hiki ambacho nitaweka Jiwe la Msingi hivi punde. Kipande hiki kinahusisha ujenzi wa njia kuu ya reli kutoka hapa Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 205 pamoja na kilometa 95 kwa ajili ya njia za kupishana na maeneo kupangia mabehewa; na hivyo kufanya jumla yake kuwa kilometa 300. Aidha, awamu hii itahusisha ujenzi wa stesheni 6 na Yadi kubwa ya kupanga mabehewa pale Ruvu mkabala na Bandari Kavu ya Mamlaka ya Bandari na hivyo itapunguza msongamano wa magari hapa 

 

Reli hii itakuwa ya kisasa kabisa na yenye uwezo mkubwa. Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO wameeleza kuwa injini za treni katika reli hii zitatumia umeme na dizeli. Mwendokasi wake utakuwa kilometa 160 kwa saa kwa treni za abiria na kilometa 120 kwa saa kwa treni za mizigo. Reli hii itakuwa na uwezo wa kuhimili uzani wa tani 35 kwa ekseli. Ujenzi wa kipande hiki cha kwanza unatarajiwa kuchukua miezi 30, sawa na miaka miwili na nusu.

 

Gharama za ujenzi za kipande hiki cha kutoka Dar es Salaam ni Dola za Marekani milioni 1.22 sawa na shilingi trilioni 2.8. Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha (2016/2017), Serikali imetenga shilingi trilioni 1 kuanza kugharamia. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha bajeti ya kuanza ujenzi wa reli hii. Na haya ndio majibu kwa baadhi ya watu wanaodai kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo katika mwaka huu wa fedha kwa kukosa fedha. Hii sio kweli. Fedha tunazo. Lakini ni vyema ikaeleweka kuwa wakati mwingine Serikali inashindwa kutoa fedha ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa vile maandalizi yanakuwa bado kukamilika. Mathalan, fedha za mradi huu zilikuwepo tangu mwezi Julai mwaka jana. Lakini Mkandarasi, kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki na Mota-Engil ya Ureno, tumewekeana naye saini mwezi Februari 2017.  Sasa Serikali ingewezaje kutoa fedha wakati Mkandarasi alikuwa bado kupatikana? Sasa Mkandarasi amepatikana na tayari tumeshamlipa kiasi cha shilingi bilioni 300.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Baada ya kumpata Mkandarasi na kuanza ujenzi wa kipande hiki cha Dar es Salaam, sasa Serikali inaelekeza nguvu katika vipande vilivyobaki vya Marogoro -  Makutopora (km. 336), Makutopora – Tabora (km. 294), Tabora – Isaka (km. 133) na Isaka – Mwanza (km. 248). Zabuni za usanifu na kujenga tayari zimetangazwa na zinatarajiwa kufunguliwa mwanzoni mwa mwezi ujao.

 

Ninayo furaha kuarifu kuwa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki hapa nchini mwezi Januari 2017, aliahidi kutusaidia kupata fedha kwa ajili ya kujenga kipande cha kutoka Morogoro hadi Dodoma. Na mpaka sasa wawakilishi wa Mabenki takriban matano kutoka Uturuki wameshakuja nchini kwa ajili ya kufanya mazugumzo ili watupatie mkopo nafuu wa kujenga kipande hicho. Lakini pia alipokuja Rais wa Benki ya Dunia hapa nchini mwezi uliopita (Machi 2017) alionesha nia ya kutusaidia kupata fedha za kutekeleza mradi huu pamoja na kutupatia mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 300 kukarabati reli ya zamani. Nimefurahi hapa leo tunaye Mwakalishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Mama Bird, ambaye naamini ataendelea kuwakumbusha viongozi wake ili kutupatia mkopo huo.

 

Kama mnavyofahamu, reli ya kati tunayoitumia sasa bado ni muhimu. Tutaendelea kuitumia kusafirisha mizigo na abiria. Aidha, vifaa vya ujenzi wa reli hii mpya vitasafirishwa kupitia reli yetu hii ya sasa. Na hata ujenzi wa reli mpya utakapokamilika, reli ya zamani itaendelea kuitumia. Hii ni kwa sababu, reli mpya ya standard gauge tunayoijenga itakuwa na stesheni 28 tu kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Reli ya kati inayotumika sasa ina stesheni 67. Hivyo, itaendelea kuhitajika kutoa huduma kwenye maeneo ambayo reli mpya haitakuwa na stesheni.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ni dhahiri kuwa hatua hizi tulizoanza kuzichukua ni nzuri na kila Mtanzania hana budi kujivunia. Hata hivyo, nafahamu kuwa wapo baadhi ya wenzetu ambao wanabeza hatua hizi. Kubeza kwao kusitukatishe tamaa. Tukumbuke tu kuwa safari ya maendeleo. Safari ya maendeleo inafanana sana na usafiri wa lori. Madereva wa malori wanafahamu kuwa ukibeba abiria ni kawaida kumwona kila mmojawapo anaangalia upande wake, lakini watakuwepo pia wenye kuongea, kuimba na kukaa kimya. Dereva mzuri huwa hajishughulishi sana kuwaangalia au kuwasikiliza abiria hao. Yeye atajitahidi sana kuangalia mbele lori linakoelekea ili awafikisha abiria wake salama. Hivyo basi, napenda niwahakikishie Watanzania wenzangu kuwa mimi ni dereva mzuri. Ninafahamu ninakoelekea na nitawawafikisha salama. Na dalili zimeanza kujionesha.

 

Jana Benki ya Dunia imetoa Ripoti yake ambayo imetaja nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi tano zinazofanya vizuri kiuchumi Barani Afrika. Hii ni ishara tosha kuwa tunaelekea sehemu nzuri. Lakini hata ninyi wana-Dar es Salaam ni mashahidi kuwa tunaendelea. Mwezi uliopita tumeweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara za Juu (interchange) pale Ubungo. Tunajenga nyingine pale TAZARA. Aidha, baada ya kukamilisha ujenzi wa Awamu ya Kwanza wa Barabara za Mwendokasi, tumefanikiwa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa Awamu ya Pili hadi ya Nne, ambapo Awamu ya Tatu itahusisha barabara ya kutoka maeneo ya huku, hapo Gongo la Mboto, kupita Barabara za Nyerere, Uhuru, Bibi Titi, Mitaa ya Azikiwe na Maktaba zenye jumla ya urefu wa kilometa 23.6. Mipango ya kuanza ujenzi wa Daraja la kupita juu ya bahari kutoka Aga Khan hadi Coco Beach, ujenzi wa barabara za njia sita za kutoka Ubungo hadi Chalinze inaendelea vizuri. Aidha, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga shilingi bilioni 38 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami za mzunguko (Dar es Salaam Outer Ring Road) zenye urefu wa kilometa 34.

 

Lakini sio hivyo tu. Kwenye usafiri wa anga, tumenunua ndege mpya sita, mbili zimeshawasili na kuanza kufanya kazi. Ndege nyingine zinatarajiwa kuwa zimewasili mapema mwakani, ikiwemo ndege kubwa moja aina Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba watu 262. Tunaendelea pia na ukarabati wa viwanja vya ndege sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Dodoma, Iringa, Mwanza, Mtwara, Kigoma, Songea, n.k. Haya ndiyo mambo Chama Cha Mapinduzi kiliwaahidi Watanzania wakati wa kampeni. Tutaendelea kuyasimamia na kamwe hatutamruhusu mtu yeyote kutuyumbisha na kututoa katika agenda zetu za maendeleo.

 

Mheshimiwa Wazi wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kabla sijahitimisha hotuba yangu, ninayo masuala mawili ya mwisho ambayo ningependa kueleza. Jambo la kwanza ni kuhusu usimamizi wa mradi. Nawasihi sana Wasimamizi wa Mradi huu kuusimamia ipasavyo mradi huu ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyohitaji. Aidha, natoa wito kwa Mkandarasi kuonesha umahiri wake, ikiwezekana mradi huu umalizike kabla ya muda uliopangwa. Fedha zipo, hivyo, hakuna sababu ya mradi huu kuchelewa kukamilika kwa mradi huu. Watanzania wanausubiri kwa hamu kubwa. Sambamba na kuwahimiza Wasimamizi na Mkandarasi, nawasihi sana Watanzania wenzangu watakaopata fursa za kufanya kazi kwenye mradi huu kuwa wazalendo na waaminifu. Tusiibe vifaa wala kuanzisha migomo isiyo na msingi.

 

Jambo la pili, napenda kutoa shukrani zangu nyingi kwa Kamati za Bunge zinazosimamia masuala ya Bajeti na Miundombinu kwa kazi nzuri zinazofanya. Tunawashukuru kwa kupitisha bajeti ya kuanza ujenzi wa reli hii. Natumaini katika mwaka huu pia mtapitisha bajeti kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa mradi huu.  Watanzania wanahitaji maendeleo. Maendeleo hayana chama. 

Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Reli Mpya ya Kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

 

Mungu Wabariki Wana-Dar es Salaam!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Asanteni Sana kwa Kunisikiliza”.