Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MGENI RASMI, MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA DAR ES SALAAM, TAREHE 2 FEBRUARI, 2017

Thursday 2nd February 2017

Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania;

Mhe. Job Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

Mheshimiwa Harrison Mwakyembe (Mb), Waziri wa Sheria na Katiba;

Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;

Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali;

Waheshimiwa Majaji Wakuu Wastaafu;

Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa,

Mheshimiwa Jaji Kiongozi;

Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu;

Mheshimiwa Msajili Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama;

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania Bara;

Waheshimiwa Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Waheshimiwa Wasajili, Mahakimu na Mawakili;

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa;

Viongozi wa Dini;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Napenda nianze kwa kuungana na walionitangulia kuzungumza katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa salama. Aidha, naushukuru uongozi wa Mahakama chini ya Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kunialika kujumuika nanyi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. Nimefurahi kuona kuwa miongoni mwetu leo, tunaye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Ndugai. Huu ni uthibitisho tosha kuwa mihimili yetu mitatu ya Dola inafanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano mkubwa. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Spika.

Kabla sijaendelea zaidi, napenda nitumie fursa kumpongeza, Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Othman Chande, kwanza kabisa kwa kufikisha umri wa kustaafu. Lakini pili, kwa mchango wake mkubwa katika Mahakama yetu. Kama ambavyo Kaimu Jaji Mkuu Prof. Juma ameeleza, Jaji Mkuu Mstaafu Mzee Chande amefanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi kwenye Mahakama. Mageuzi aliyoyafanya  yamesaidia kuboresha utendaji kazi wa Mahakama. Sambamba na kumpongeza Jaji Mkuu Mstaafu,  nawapongeza pia wengine wote ambao nao walitoa mchango katika kufanya mageuzi kwenye Mahakama, wakiwemo Majaji, Mahakimu, watumishi wengine wa Mahakama na bila kusahau Benki Kuu ya Dunia. Wote kwa pamoja nawashukuru na kuwapongeza sana.  

Mheshimiwa Kaimu Jaji Mkuu;

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana:

Hii ni mara yangu ya pili kushiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tangu nimekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana. Nakumbuka siku ile nilitoa ahadi kubwa mbili. Kwanza niliahidi kushirikiana na Mahakama katika kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili, hususan kuhakikisha Mahakama inapata fedha zake zote za Bajeti ya Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 12, ambazo Bunge ilipitisha kwenye bajeti ya mwaka 2015/16. Nimeambiwa kuwa fedha hizo zilitolewa katika kipindi cha siku tatu tu baada ya kutoa ahadi yangu. Ingawa sijapewa taarifa namna zilivyotumika, ni imani yangu kuwa zilitumiwa vizuri.

 

Ahadi yangu ya pili, ambayo iliendana na ahadi niliyoitoa kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ilihusu uanzishaji wa Mahakama ya kushughulikia Mafisadi. Nafurahi kuwa ahadi hiyo nayo imeweza kutimizwa kama nilivyokuwa nimeahidi. Napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyote vilivyofanikisha kuanzishwa kwa Mahakama hii, ikiwemo Mahakama yenyewe, Wizara ya Sheria na Katiba, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Rai yangu kwa majaji walioteuliwa/watakaoteuliwa kufanya kazi kwenye Mahakama hii wajitahidi kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili malengo na makusudi ya Serikali ya kuanzisha Mahakama hii yaweze kutimia.

Mheshimiwa Kaimu Jaji Mkuu;

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana:

Maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi”. Kaulimbiu hii bila shaka ina maana kuwa haki ikitendeka au kutolewa kwa wakati inachangia ukuaji uchumi katika taifa. Binafsi naiona kaulimbiu hii kuwa nzuri na inakwenda sambamba na kaulimbiu yetu ya “Hapa Kazi tu”. Kwa sababu hiyo, nawapongeza Mahakama kwa kuchagua kaulimbiu hii ambayo kwa hakika imekuja kwa wakati muafaka.

 

Nina matumaini makubwa kuwa kama kila mdau atatimiza kaulimbiu hii, nchi yetu itapata mafanikio makubwa ya kiuchumi. Tutaokoa muda na rasilimali ambazo zimekuwa zikipotea kutokana na ucheleweshaji wa utoaji haki. Na pia tutarahisisha na kuharakisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Nafurahi hivi punde Kaimu Jaji Mkuu ametueleza kuwa mwaka 2016 Mahakama iliweza kusikiliza na kumaliza mashauri 295,662, sawa na asilimia 101 ya mashauri yote yaliyosajiliwa mwaka huo, ambayo jumla yake ilikuwa 292,424. Hii ni dalili njema na nzuri. Hivyo basi, nawapongeza majaji, mahakimu, mawakili, jeshi la polisi na magereza, pamoja na vyombo vyote vilivyohusika katika kupatikana kwa mafanikio hayo.

Mheshimiwa Kaimu Jaji Mkuu;

Mabibi na Mabwana:

Licha ya mafanikio na pongezi nilizozitoa kwenu, Mahakama haipaswi kubweteka. Bado mfumo wetu wa utoaji haki hapa nchini unakabiliwa na changamoto kadhaa. Nitazitaja chache na ikiwezekana nitatoa mifano.

Kwa taarifa nilizonazo, mwaka jana jumla ya mahakimu 28 walishitakiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai, hususan kwa tuhuma za rushwa. Hata hivyo, katika mashauri yote hayo, hakuna hakimu aliyetiwa hatiani. Kwa mwananchi wa kawaida akiona hali hii ni lazima atajiuliza maswali mengi. Je, makosa haya yalikuwa ya kusingizia? Je, upelelezi haukufanyika vizuri au kuna upendeleo wa aina fulani umefanyika dhidi ya mahakimu hao? Maswali haya yanaleta kwenu Mahakama changamoto kubwa, hasa kwa kuzingatia kuwa sisi raia tumekuwa tukisikia tuhuma nyingi dhidi yenu. Nafahamu kuwa baadhi ya tuhuma hizo ni za uongo lakini zipo pia zenye ukweli. Kwa sababu hiyo, ningeshauri leo tunapoadhimisha Siku ya Sheria, Mahakama ijitathmini na kuangalia namna ya kushughulikia changamoto hii, ambayo inashusha hadhi yenu mbele ya jamii. Msiruhusu watu wachache wachafue sifa nzuri ya Mahakama.

Changamoto nyingine kwenye Mahakama inahusu ucheleweshaji wa utoaji maamuzi kwenye baadhi ya kesi, hususan kwa kesi za madai ya kodi. Kwa takwimu nilizonazo hapa, kuanzia mwaka 2001 hadi sasa kuna kesi 467 zinazohusu pingamizi za kodi ambazo thamani yake inafikia shilingi trilioni moja. Sambamba na hilo, zipo takwimu zinazoonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi 2016, Serikali ilishinda kesi kwenye Baraza la Rufani za Kodi (Tax Revenue Appeal Tribunal) zenye thamani ya shilingi trilioni 2.5 na Dola za Marekani bilioni 2.47, zikiwa ni sawa na jumla ya shilingi trilioni 7.5. Hivyo basi, naiomba Mahakama na vyombo vingine husika kuharakisha usikilizaji wa mashauri yanayohusu masuala ya kodi, hasa yale yenye ushahidi wa kutosha. Sambamba na hilo, navihimiza vyombo husika kuhakikisha fedha zote ambazo Serikali inadai baada ya kushinda kesi zinakusanywa ili ziweze kutumika kwenye shughuli za maendeleo.

Nimefahamishwa kuwa wakati mwingine Mahakamani kuna mtindo unaoitwa kupaki kesi. Mtindo huu unampa mdaiwa wa kodi aliyeshidwa kesi,  kukata rufaa na akishindwa baada ya kukata rufaa, anakwenda kupaki kesi mahakamani. Wakati akiwa amepaki kesi, mdaiwa huyu wa kodi hachukuliwi hatua zozote na anaendelea kufanya shughuli zake za biashara kama kawaida. Hatupaswi kuacha jambo liendelee. Ni lazima wakwepa kodi wachukuliwe hatua tena za haraka. Kwenye nchi zilizoendelea ambazo hutupatia misaada, kukwepa kodi ni kosa kubwa. Haijalishi una wadhifa gani au cheo gani. Hivyo basi, sisi nasi ni lazima tuchukue hatua kali na za haraka dhidi ya wakwepa kodi.

Changamoto nyingine inayohusu Mahakama inahusu ucheleweshaji wa kusajili au kutaja kesi. Baadhi ya kesi zinasajiliwa au kutajwa kwa haraka na nyingine zinacheleweshwa kwa makusudi. Hili nalo ni tatizo ambalo linapaswa kushughulikiwa.

Mheshimiwa Kaimu Jaji Mkuu;

Mabibi na Mabwana:

Sio Mahakama pekee ndiyo yenye changamoto. Hata taasisi nyingine za utoaji haki nazo zina changamoto. Ni jambo ambalo liko wazi kuwa Ofisi mbili za Serikali, yaani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwendesha Mashtaka zina msuguano. Kwa bahati nzuri wahusika wote leo mko hapa: Mheshimiwa Waziri wa Sheria na Katiba; Mwanasheria Mkuu; na Mkurugenzi wa Mashtaka. Ni lazima tutafute ufumbuzi wa changamoto hii. Kama tatizo ni madaraka au kasma, ningeshauri mlete marekebisho ambayo yatawezesha vyombo hivi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuleta ufanisi katika utendaji kazi. Wakati mwingine Serikali imekuwa ikishindwa kesi kutokana na kuwepo kwa migogoro kama hii.

Kwa upande wa polisi na TAKUKURU nako kuna changamoto, lakini kubwa ni ucheleweshaji wa upelelezi. Wakati mwingine ucheleweshaji huu unafanyika huku kukiwa na ushahidi na vielelezo vya kutosha. Hili nalo ni lazima tulirekebishe. Kesi zenye ushahidi wa kutosha ni lazima uamuzi wake ufanyike kwa haraka.

Mabibi na Mabwana:

Rais wa Jumuiya ya Wanasheria wa Tanganyika ameeleza mambo mengi na kutoa maoni mazuri. Aidha, amenialika kushiriki kwenye Mkutano wao na napenda kumwaahidi kuwa nitalifanyia kazi ombi lao. Lakini ninyi nanyi mna changamoto zenu zinazowakabili, ambazo ni kubwa tu. Jumuiya hii imejiingiza kwenye masuala ya kisiasa. Inatumika kisiasa. Hili sio jambo zuri hata kidogo. Jumuiya hii inapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ueledi na kwa manufaa ya taifa. Mkijielezeka kwenye Chama chochote mtapoteza mwelekeo. Jumuiya yenu ikiwa huru itaheshimiwa na kila Mtanzania. Hivyo, fanyeni kazi zenu kwa maslahi ya Watanzania wote. Kumbukeni ya kuwa maendeleo hayana Chama.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;

Hivi punde umeeleza baadhi ya changamoto zinazokabili Mahakama. Umeeleza kuhusu ufinyu wa bajeti, maslahi madogo, uhaba/ubovu wa miundombinu pamoja na uhaba wa watumishi. Nakubaliana na wewe kuhusu umuhimu wa kuzishughulikia. Naahidi Serikali  italifanyia kazi suala hili sio tu kwa Mahakama bali kwa vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya utoaji haki. Ombi langu kwenu, nanyi mjitahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kutoa haki kwa haraka ili muweze kuchangia ukuaji uchumi wa taifa letu. Mashauri yanayohusiana na masuala kama ya kodi ni vyema yakaendeshwa kwa haraka.

 

Kuhusu changamoto ya uhaba ya watumishi wa mahakama, ningependa nitoe maelezo kidogo. Kwa takwimu zilizopo, Mahakama ni moja ya taasisi zenye idadi kubwa ya watumishi. Zipo taasisi nyingine za Serikali zenye majukumu makubwa kama Mahakama lakini zina watumishi wachache. Mathalan, kwa taarifa nilizonazo, Mahakama ina waajiri wa kazi ya ulinzi wapatao 1179. Je, ni kweli Mahakama inahitaji walinzi wote hao? Kwanini msitumie Jeshi la Polisi au Makampuni ya Ulinzi au kuunganisha baadhi ya majukumu ili zifanywe na watu wachache ambao watalipwa maslahi mazuri.

 

Hivyo basi, nitafurahi kuona mageuzi mnayofanya katika Mahakama yatazingatia pia suala hili la watumishi. Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi takriban shilingi bilioni 600 kuwalipa watumishi mishahara. Hivyo, itakuwa sio jambo la busara kuendelea kuongeza idadi ya watumishi Serikalini. Tunataka fedha nyingi zitumike kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kutatua matatizo ya wananchi. Pamoja na hayo, napenda kuwahakikishia kuwa kwa zile nafasi nyeti na muhimu zinazohitajika kuzibwa, tutaendelea kuajiri.

 

Mheshimiwa Kaimu Jaji Mkuu;

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana:

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru tena Mheshimiwa Kaimu Jaji Mkuu kwa kunikaribisha kwenye shughuli hii muhimu. Naahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wote wa mfumo wa utoaji haki hapa nchini. Niwaombe, kama mtaona inafaa, kuanzisha Jukwaa ambalo mtalitumia kujadili masuala yenu na ikiwezekana kuishauri Serikali.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda niwatakie wadau wote wa utoaji haki nchini utekelezaji mzuri wa majukumu katika mwaka huu mpya mnaouanza.

 

“Ahsanteni Sana kwa Kunisikiliza”