Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA DAR ES SALAAM, TAREHE 13 DESEMBA, 2016

Tuesday 13th December 2016

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Zanzibar;

Mzee Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM - Tanzania Bara;

Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;

Wajumbe wa Kamati Kuu;

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;

Ndugu Wana-CCM Wenzangu:

 

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutukutanisha hapa tukiwa wazima. Aidha, nawashukuru ninyi wajumbe kwa kuja kwa wingi kuhudhuria Mkutano huu. Nawakaribisha Dar es Salaam. Nawakaribisheni sana hapa Ikulu. Jisikieni mko nyumbani. Hapa ni nyumbani kwenu.

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu Wajumbe wenzangu wa NEC;

Leo ni mara yangu ya kwanza kuongoza Mkutano huu wa Halmashauri Kuu ya Taifa tangu nimechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu mwezi Julai mwaka huu. Nakumbuka wakati napokea wadhifa wa Uenyekiti niliwashukuru Wajumbe wote kwa kunichagua. Lakini napenda, kwa mara nyingine tena, niwashukuru kwa dhati kabisa, wajumbe wote wa NEC kwa kunichagua kwa kishindo. Mlinipa kura zote.

Ahsanteni sana kwa imani kubwa mliyonionesha. Kama nilivyoahidi wakati ule, sitawaangusha.

 

Napenda kutumia fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Mwenyekiti Mstaafu wa Chama chetu, Mzee Kikwete, kwa uamuzi wake wa kung’atuka kabla ya muda wake ili kuniachia kijiti cha kuongoza Chama hiki. Uamuzi wake huo, ni kielezo kingine cha ubora na kukomaa kwa demokrasia kwenye Chama chetu. Nafurahi Mama Salma Kikwete yupo hapa. Natumaini atafikisha shukrani zangu kwake. 

 

Ndugu Wajumbe wa NEC;

 

Katika hotuba yangu ya kupokea Uenyekiti nilieleza kwa kirefu masuala ambayo tutayapa kipaumbele katika Awamu hii ya uongozi. Nilieleza masuala mengi. Nisingependa nirudie. Lakini nitawakumbusha japo kwa haraka haraka.

 

  • Kwanza, uimarishaji wa Chama katika ngazi zote pamoja na Jumuiya zake. Tunataka kuwa na Chama imara chenye uwezo wa kuisimamia Serikali na kutetea wanyonge. Hatutaki kuwa na Chama legelege cha watu walalamikaji. Sisi ndio tumepewa ridhaa na wananchi kuongoza hivyo hatuna budi kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake ipasavyo. Kwa maana nyingine, ninyi viongozi wa Chama mnapaswa kutoa maelekezo kwa Serikali kuhusu masuala mbalimbali.

 

  •  Pili, kuongeza idadi ya wanachama. Chama ni wanachama. Bila wanachama hakuna Chama. Hivyo, ni lazima tuhakikishe Chama chetu kina idadi kubwa ya wanachama, hususan vijana.

 

  • Tatu, kuondoa rushwa katika Chama. Chama chetu ni miongoni mwa taasisi zinazotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa nchini. Uwepo wa rushwa kwenye Chama chetu umekuwa ukijidhihirisha zaidi nyakati za uchaguzi. Ni lazima tutafute ufumbuzi wa gonjwa hili sugu. Hatutakuwa na msamaha na watoa na wapokea rushwa. Tutahakikisha Chama chetu kina viongozi na wanachama waadilifu.

 

  • Nne, Chama kujitegemea kiuchumi. Tunataka Chama chetu kijitegemee kiuchumi. Haifai na ni aibu kwa Chama kikongwe kama chetu kutegemea fedha za ruzuku na watu binafsi kujiendesha. Tunazo rasilimali nyingi: mashamba, viwanja na vitega uchumi vya kila aina. Kinachohitajika ni kuhakikisha rasilimali hizo zinakinufaisha Chama chetu. Hivi sasa rasilimali zetu nyingi hatunufaiki nazo kutokana na usimamizi mbovu, ubadhirifu na kuingia mikataba isiyo na tija.

 

  • Tano, kukomesha usaliti na kuvunja makundi. Wapo wanachama wachache ambao hukisaliti Chama chetu hasa nyakati za uchaguzi. Wapo pia wenye kuendekeza makundi hata baada ya uchaguzi kumalizika. Tutanataka kuikomesha tabia hii, ambayo inakidhoofisha sana Chama chetu. Napenda kutumia fursa hii kupongeza Kamati za Siasa za Wilaya na Mikoa ambazo zimechukua hatua dhidi ya watu waliotusaliti kwenye Uchaguzi mwaka jana.

 

  • Sita, tunataka tuwe na Chama kilicho imara, hususan kwenye ngazi ya chini, ambako kuna wanachama wengi. Na sio Chama ambacho kipo kwa ajili ya viogozi wa juu pekee. Hivyo basi, katika awamu hii tunalenga kuwa na viongozi na vikao vichache vya ngazi ya juu.

 

  • Saba, tunataka Chama chenye kuzingatia kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Toleo la Mwaka 2012 ambazo zinaelekeza mwanachama kutokuwa na kofia mbili za uongozi katika Chama. Aidha, tunataka Chama chenye kuzingatia Katiba yake. Mathalan, vyeo katika Chama viwe ni vile tu vinavyotambulika kikatiba. Vile visivyotambuliwa Kikatiba, visiruhusiwe kama Mwenyekiti wa Wenyeviti, Makamanda au Walezi.

 

  • Nane, Tunataka kanuni za Jumuiya za Chama ziendane na kanuni na matakwa ya Chama. Hivyo Jumuiya ni lazima zitekeleze majukumu yake kwa kuzingatia Katiba na Malengo ya Chama.

 

  • Tisa, Tunataka kuwa na Chama kinachoongozwa na wanachama badala ya kuwa na mwanachama anayekiongoza Chama, na hivyo kufanya Chama kumfuta mwanachama badala ya mwanachama kukifuata Chama. Kwa hiyo, Chama ni lazima kiendelee kuwa mali ya wanachama badala ya Chama kuwa mali ya mwanachama.  

 

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo tutayapa kipaumbele. Yapo mengine mengi. Lakini niseme tu kwamba itakuwa ni vigumu sana, mimi peke yangu, kutekeleza haya yote. Ni lazima tushirikiane. Na kwa kweli, mimi nawategemea ninyi katika kutekeleza mambo niliyoyataja. Hivyo, ni lazima tuwe kitu kimoja katika kukijenga Chama chetu.

 

Ndugu Wajumbe wa NEC;

 

Mwakani Chama chetu kitakuwa na jukumu moja kubwa: Kuchagua viongozi ambao wataongoza Chama chetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Zoezi la uchaguzi litaanza mwezi Februari na kukamilika mwezi Novemba 2017. Hili ni zoezi muhimu sana kwa vile uongozi tutakaouchagua ndio utakuwa na jukumu la kukipa Chama chetu ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Tukichagua safu bora ya uongozi tutakuwa na uhakika wa ushindi wa kishindo kwenye chaguzi hizo. Tukichagua viongozi wabovu, tutapata shida kushinda.

 

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuhimiza Sekretarieti na Kamati za Siasa katika ngazi zote kuanza maandalizi ya uchaguzi huo, kwa kuwahamasisha wana-CCM kote nchini kujiandaa kushiriki uchaguzi huo. Aidha, napenda kutoa wito kwa wana-CCM wenzangu kuhakikisha tunachagua safu bora ya uongozi. Tuwachague viongozi wenye weledi, wachapakazi, waadilifu na wenye kukubalika kwenye jamii. Kamwe tusiwachague wala rushwa. Napenda kurudia onyo langu kuwa katika awamu hii hatutamsamehe mtu yeyote mwenye kutafuta uongozi kwa njia ya rushwa. Rushwa sasa basi kwenye Chama chetu. Aidha, naviagiza vyombo husika kuhakikisha kuwa wajumbe halali tu ndiyo wanashiriki uchaguzi. Pasiwe na mapandikizi. Tukipata taarifa za kuwepo kwa mapandikizi hatutasita kufuta uchaguzi.

 

Ndugu Wajumbe wa NEC;

 

Kwa mara nyingine tena, mwaka jana Watanzania walituamini na kutupa dhamana ya kuendelea kuliongoza taifa letu. Lakini kama mnavyofahamu, mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi unaofuata. Uchaguzi Mkuu mwingine utafanyika mwaka 2020. Hivyo basi, hatuna budi kujiandaa. Nafarijika kuona kuwa kwa upande wetu  tumeanza kujiandaa kwa uchaguzi ujao, hususan kwa kuanza kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka jana.

 

Kama mtakavyokumbuka, Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka jana ilisheheni masuala mengi. Ilikuwa na ahadi nyingi. Tuliahidi kudumisha amani, muungano, umoja na mshikamano wetu. Tuliahidi kujenga uchumi wa viwanda ili kupambana na umaskini na tatizo la ajira. Tuliahidi kuboresha huduma za jamii, hususan elimu na afya. Tuliahidi kuzidisha mapambano ya kuondoa urasimu, uzembe, ubadhirifu na rushwa pamoja na kero nyingine zinazokabili wananchi. Tuliahidi kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi yake. Tuliahidi kuimarisha uhusiano wetu na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa.

 

Ndugu Wajumbe wa NEC;

 

Kama nilivyosema, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 unakwenda vizuri. Nchi yetu ina amani. Mipaka yetu iko salama.  Nchi ni tulivu.  Vyombo vyetu vya ulinzi viko imara katika kukabiliana na tishio lolote la usalama. Muungano wetu nao upo imara. Umoja na mshikamano wa Watanzania unaendelea.

 

Hali ya uchumi wetu ni nzuri. Tumepanga uchumi mwaka huu ukue kwa asilimia 7.2 kutoka asilimia 7.0 mwaka jana. Dalili za kufikia azma hiyo zinaonekana. Uchumi katika robo ya pili ya mwaka huu ulikua kwa asilimia 7.9. Tumeweza kushusha mfumko wa bei kutoka asilimia 6.5 mwezi Januari mwaka huu hadi kufikia asilimia 4.5 mwezi uliopita. Tunaedelea na utekelezaji wa ahadi yetu ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuwezesha nchi yetu kuwa ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, kama ambavyo Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo inavyoelekeza. Ili kujenga uchumi wa viwanda, inahitajika miundombinu imara ya usafiri na nishati ya umeme. Tunaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

 

Katika bajeti ya mwaka huu, ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tumeelekeza asilimia 40 kwenye shughuli za maendeleo, tumetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri na umeme. Tunataka kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), ambapo tumetenga shilingi trilioni 1. Reli hii itaunganisha nchi yetu na majirani zetu wa Rwanda na Burundi na hivyo kukuza shughuli za kiuchumi. Tunataka kununua meli mbili, moja Ziwa Victoria na nyingine Ziwa Tanganyika. Tunataka kununua ndege mpya ili kufufua Shirika letu la Ndege na kuboresha viwanja vya ndege. Tayari tumenunua ndege mpya sita na mbili zimeanza kufanya kazi. Taratibu za kununua ndege kubwa mbili zinaendelea. Hii itasaidia sana kukuza utalii nchini kwetu. Ni vigumu sana kukuza uchumi wa kitalii kama hatuna ndege. Sambamba na hatua hizo, tunaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.

 

Miradi mikubwa miwili ya umeme inatekelezwa, ikiwemo upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi I ili uwe na uwezo wa kuzalisha Megawati 335 kutoka Megawati 150 za sasa. Mradi mwingine ni Kinyerezi II ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 240. Sambamba na miradi hiyo, tunatekeleza miradi mikubwa miwili ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 wa kutoka Iringa-Dodoma-Singida-Tabora-Shinyanga wenye urefu wa kilometa 670 na kutoka Dar es Salaam – Tanga – Arusha wenye urefu wa kilometa 702. Katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 534.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini utakaotekelezwa na Wakala wa Nishati vijijini (REA). Aidha, wafadhili mbalimbali wameonesha nia ya kutuunga mkono kwa kuahidi kutoa zaidi ya shilingi bilioni 200.

 

Ndugu Wajumbe wa NEC;

Kuhusu huduma za jamii, tunaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na maji. Tumetenga takriban shilingi trilioni 1.99 kwa ajili ya sekta ya afya. Nyingi ya fedha hizo tutazitumia katika kununulia madawa na vifaa tiba. Tumeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka jana hadi kufikia shilingi bilioni 250 mwaka huu.

Kwenye elimu nako tumeanza kutoa elimumsingi bila malipo, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 18.77 kwa ajili ya kugharamia. Tumeongeza fedha za mikopo ya Elimu ya Juu kutoka shilingi bilioni 340 hadi kufikia shilingi bilioni 483. Matokeo ya hatua hizi ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza na wale elimu ya juu imeongezeka. Wanafunzi wa darasa la kwanza wameongezeka kwa zaidi ya asilimia 84, wanafunzi wa sekondari kwa asilimia 26  na wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wameongezeka kutoka wanafunzi 98,300 hadi kufikia takriban wanafunzi 125,000.

 

Tunaendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo urasimu katika utoaji huduma za umma na rushwa. Tunachukua hatua kali za “kuwatumbua” watumishi wa umma wazembe na wabadhirifu.  Tumeanzisha Mahakama ya Mafisadi. Tumepunguza kero za kodi na tozo kwa wakulima. Wakulima wa korosho kwenye Mikoa ya Kusini ni mashahidi. Hivi majuzi nimewaagiza Wakuu wa Mikoa kuacha mara moja kuwabughuzi wafanyabiashara wadogo wadogo.

 

Tumeongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi. Hii imewezekana baada ya kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi. Tumedhibiti matumizi ya fedha za Serikali kwa kuzuia safari za nje, kuwaondoa takriban watumishi hewa 19,000 pamoja na kubaini kaya maskini hewa 55,000 waliokuwa wakipata misaada kutoka Mpango wa TASAF na wanafunzi hewa 65,000 wa shule za msingi. Tumepungua makato ya kodi kwa wafanyakazi kutoka asilimia 11 hadi 9.

 

Kuhusu masuala ya diplomasia, tumeendelea kukuza mahusiano yetu na mataifa ya nje pamoja na taasisi za kimataifa. Viongozi Wakuu wa Nchi mbalimbali wametutembelea kutoka Vietnam, India, Rwanda, Cuba, DRC, Morocco na Zambia. Mimi nimetembelea Rwanda, Uganda na Kenya. Katika ziara zote hizo, mkazo tumeweka katika ushirikiano wa kiuchumi.

 

Ndugu Wajumbe wa NEC;

 

 Nina imani kabisa, kwa kasi hii tuliyoanza nayo tutaweza kutekeleza yale yote tuliyoyaahidi wakati wa kampeni. Niwaombe wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa mjivunie na kutangaza kwa wananchi mafanikio tuliyoyapata. Tuwahimize wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. Tuwahimize wananchi pia kulipa kodi. Tutafute na kuwahamasisha wafanyabiashara kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Nafurahi wafanyabiashara wengi wameanza kuwekeza hapa nchini. Nawakaribisha wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini na Serikali itaendelea kutoa vivutio mbalimbali.

 

Waheshimiwa Makamu Wenyeviti wa CCM Taifa;

Ndugu Katibu Mkuu;

Ndugu Wajumbe wenzangu wa NEC;

 

Siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kutoa shukrani zangu nyingi za dhati kwa Makamu wa Wenyeviti, Mheshimiwa Dkt. Shein na Mzee Mangula kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Binafsi naendelea kujifunza mambo mengi kutoka kwao. Aidha, napenda nimshukuru Katibu Mkuu, Mzee wangu Kinana. Huyu ni nguzo na hazina muhimu sana kwenye Chama chetu. Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya Chama kwa kazi kubwa mnayoifanya. Nawashukuru Wabunge na watumishi wa Serikali. Nawashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali. Nipo pamoja nanyi nyote. Tuendelee kushirikiana.

 

Napenda kuhitimisha kwa kusema kuwa tupo hapa kwa ajili ya kazi maalum. Katika mkutano wa leo tutaleta mapendekezo mbalimbali ya kuboresha muundo wa Chama chetu. Mapendekezo hayo hayamkusudii mtu bali kuboresha ubora wa Chama chetu.  Hivyo basi, nawaombeni sana muyaunge mkono. Mkifanya hivyo, nina matumaini makubwa kuwa Chama chetu kitazidi kuimarika na kitaweza kuwatumikia vizuri Watanzania ambao wanakiamini sana.

 

 

Mungu Ibariki Tanzania!

         Kidumu Chama cha Mapinduzi!

       “Asanteni sana kwa Kunisikiliza”