Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE YA UFUNGUZI WA AWAMU YA KWANZA YA MIUNDOMBINU NA UTOAJI WA HUDUMA KATIKA MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA (BRT) KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM, KITUO KIKUU CHA MABASI KARIAKOO - GEREZANI TAREHE 25 JANUARI, 2017

Wednesday 25th January 2017

Mhe. Profesa Makame M. Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI;

 

Mhe. Dkt. Makhtar Diop, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

 

Katibu Mkuu Kiongozi;

 

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;

 

Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;

 

Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wote mliopo;

 

Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia;

 

Watendaji Wakuu wa TANROADS na DART;

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara DART;

Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:

 

Napenda nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa TAMISEMI pamoja na Ujenzi kwa kunialika.  Binafsi najisikia faraja sana kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuzindua mradi huu. Mimi naufahamu vizuri mradi huu. Nafahamu namna ulivyoanza pamoja na madhumuni na malengo yake. Hivyo basi, kuwepo mahali hapa leo najisikia furaha sana.

 

Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wana-Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili. Nawashukuru pia wageni wetu waliotoka nje ya nchi kuja kujumuika nasi hivi leo. Na kwa kipekee kabisa, namshukuru Mheshimiwa Mukhtar Diop, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika. Your Excellency, Dr. Diop, we thank you very much for being with us today. Kwa ujumla wenu wote, nawashukuru sana.  Uwepo wenu mahali hapa muda huu ni uthibitisho tosha kuwa mradi huu ni muhimu.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi ;

Mabibi na Mabwana ;

Dar es Salaam ni Jiji kuu la biashara nchini. Na pia ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi kubwa Barani Afrika. Shughuli za kiuchumi zinaongezeka na vivyo hivyo idadi ya watu. Hivi sasa Dar es Salaam inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 5.

 

Kutokana na kukua kwa kasi kwa Jiji hili, zimetokea changamoto. Mojawapo ni msongamano wa magari. Athari za msongamano wa magari barabarani sote tunazifahamu. Nitazitaja chache. Kuongezeka kwa ajali, watu kushindwa kufika kazini kwa wakati, huduma  za uokoaji kama vile zimamoto na usafiri wa magari ya wagonjwa kuathirika na pia upotevu wa fedha. Mathalan, kabla ya kuanza kazi kwa mradi tunaozindua leo watu walilazimika kukaa kwa zaidi ya masaa mawili kutoka Kivukoni hadi Kimara. Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanyika mwaka 2013, nchi yetu ilikuwa ikipoteza kiasi cha shilingi bilioni 411.55 kwa mwaka kutokana na tatizo la msongamano barabarani.

 

Waheshimiwa Viongozi ;

Mabibi na Mabwana ;

Ili kukabiliana na changamoto hii ya msongamano wa magari, Serikali ilibuni mradi huu wa Mabasi ya Mwendokasi (Dar es Salaam Rapid Bus Transit – BRT). Mradi huu umepangwa kutekelezwa kwa awamu mbalimbali. Awamu ya kwanza ndiyo hii tutakayoizindua leo, ambayo inahusisha barabara zenye urefu wa kilometa 20.9 ambazo tayari zimeanza kutumika. Ujenzi  wa barabara za awamu ya kwanza ulianza mwezi Agosti 2010 na kukamilika mwezi Desemba 2015. Gharama zilizotumika katika awamu hii ya kwanza ni shilingi bilioni 403. Kati ya fedha hizo, shilinngi bilioni 317 zilitokana na mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.  Serikali yetu ilitoa shilingi bilioni 86.5.

 

Napenda kutumia fursa hii, kutoa shukrani zangu nyingi kwa Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mzee Kikwete, kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha mradi huu. Nawashukuru pia watendaji wote wa Serikali, Mkandarasi pamoja na Mshauri Mtaalam kwa kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Naishukuru pia Kampuni ya Simon Group kwa kukubali kwao kushirikiana na Serikali katika kuendesha mradi huu. Kwa namna ya kipekee kabisa, naomba kwa niaba yenu, niwashukuru washirika wetu kwenye mradi huu, Benki ya Dunia, kwa kukubali kutufadhili. Nimefarijika sana kuona leo katika uzinduzi huu tunaye Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia hapa, Dkt. Diop. Dr. Diop, we thank you very much for the contribution your Bank has given us.  Naomba ufikishe salamu zetu nyingi kwenye Benki yako.  Namshukuru Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Mama Bella na wafanyakazi wote wa Benki ya Dunia kwa ushirikiano mzuri wanaoutoa kwa nchi yetu.

 

Mabibi na Mabwana 

Benki ya Dunia mpaka sasa imefadhili hapa nchini miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.2. Kwa sasa Benki ya Dunia inafadhili takriban miradi 28 hapa nchini kwenye sekta za nishati, usafiri, kilimo, afya, elimu, maji na utawala bora. Mwaka jana (2016) pekee, Benki ya Dunia ilikubali kufadhili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.6, ikiwemo mradi wa maboresho ya usafiri wa reli wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300; upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam  wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 600 (majadiliano yanaendelea); miradi ya usafiri wa mwendokasi kama nilivyowishaeleza awali yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 428; kufaya mageuzi (reforms) kwenye mahakama zetu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 65; mradi wa kupeleka umeme vijijini wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 200 ; mradi wa kuboresha huduma mjini Zanzibar wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 55 (majadiliano yanaendelea); na uboreshaji wa Vyuo Vikuu vya Sokoine na Nelson Mandela wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 24. Aidha, Benki ya Dunia itaendelea kufadhili mradi wa TASAF wenye thamani ya takriban Dola za Marekani milioni 200, ingawa katika majadiliano yetu katika awamu inayofuata tunataka kufanya marekebisho kidogo kuhusu utaratibu unaotumika kuzisaidia kaya maskini. Tunataka kaya maskini zifanye kazi lakini pia kuwadhibiti watu wasio waaminifu wenye nia ya kujinufaisha na fedha hizo kama ilivyotokea siku ya nyuma, ambapo zilitengenezwa kaya maskini hewa takriban 55,000. 

 

Pamoja na kufadhili miradi hiyo mingi, ombi langu kubwa leo kwa Benki ya Dunia ni kwamba, mradi huu wa mwendokasi tunaouzindua leo unakabiliwa na changamoto. Changamoto kubwa ni tatizo la msongamano wa magari katika eneo la makutano ya barabara pale Ubungo. Hali hii inasababisha magari ya mwendokasi kukaa muda mrefu barabarani na hivyo kuondoa dhana nzima ya usafiri wa haraka. Nafahamu majadiliano yetu na Benki ya Dunia ili kupata mkopo wa kujenga barabara za juu pale Ubungo yanaendelea vizuri. Lakini napenda kutumia fursa hii kuhimiza pande husika kukamilisha mazungumzo hayo mapema ili mkandarasi apatikane na ujenzi uanze mara moja.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana;

Baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya usafiri huu wa mwendokasi, Serikali inajipanga kuanza utekelezaji wa awamu nyingine za mradi huu. Awamu zinazofuata ni kama ifuatavyo:

(i)           Ujenzi wa Awamu ya Pili utakaohusisha Barabara ya Kilwa kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu na barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi eneo la Jitegemee zikiwa na jumla ya urefu wa kilometa 19.3. Awamu hii itahusisha pia ujenzi wa Barabara za Juu (Flyovers) katika makutano ya Barabara ya Nyerere na Kawawa (Chang’ombe – VETA) na makutano ya Barabara ya Kilwa na Mandela (Uhasibu) na pia ujenzi wa vituo vya mabasi ya BRT. Awamu ya Pili itajengwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka  Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

 

(ii)         Awamu ya Tatu itahusisha barabara za Nyerere hadi Gongo la Mboto, Uhuru, Bibi Titi, Mitaa ya Azikiwe na Maktaba zenye jumla ya urefu wa kilometa 23.6.  Awamu ya Nne itahusisha barabara za Bagamoyo hadi Tegeta, kuanzia Barabara ya Bibi Titi, Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma zenye jumla ya urefu wa kilometa 25.9. Awamu hizi zitafadhiliwa na Benki ya Dunia.

 

(iii)       Benki ya Dunia pia inatarajia kugharamia usanifu wa awamu ya V na VI. Usanifu utahusisha barabara zenye urefu kilometa 22.8 ikiwemo barabara ya Mandela.  Vilevile, Benki ya Dunia imekubali kufanya usanifu wa barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 27.6 ikiwemo barabara ya Mwai Kibaki.

 

Mabibi na Mabwana ;

Mbali na miundombinu hii ya mabasi ya mwendo kasi, Serikali imepanga kutekeleza miradi mingine ya miundombinu kama tulivyoahidi kipindi cha Kampeni, ikiwemo ujenzi wa Daraja la kupita juu ya bahari kutoka Aga Khan hadi Coco Beach ambalo litajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea. Aidha, tutajenga barabara za juu (flyovers) katika makutano ya barabara kwenye maeneo ya Mwenge, Morocco, Magomeni, Ubungo, Tabata, KAMATA na TAZARA. Kama mtakavyokumbuka, ujenzi wa barabara ya juu pale TAZARA tayari umeanza ambapo tarehe 16 Aprili, 2016 niliweka jiwe la msingi. Ujenzi wa barabara hii unafadhiliwa na Serikali ya Japan.

 

Sambamba na miradi hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2016/17 imetenga fedha za ndani Shilingi billioni 38 kwa ajili ya kuboresha barabara za Jiji la Dar es Salaam. Aidha, hivi karibuni tutaanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa ambayo itatumia umeme au mafuta. Tutaanza na kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na tutaendelea na ujenzi kwa awamu. Vilevile, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ameeleza hivi punde kuwa maandalizi ya ujenzi wa barabara za haraka za njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze yanaendelea vizuri. Nilikuwa nikinong’ona na Mheshimiwa Dkt. Diop muda mfupi uliopita kuhusu ujenzi wa reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Ruvu ambako tutajenga Kituo Kikubwa cha kupokea Mizigo na ameonesha kuukubali mradi huo. Azma yetu sio tu kuondoa tatizo la msongamano bali pia kulifanya jiji letu la Dar es Salaam kuwa la kisasa. Liwe jiji linalovutia. Hapa ndio kioo cha nchi yetu. Hata uamuzi wetu wa kuhamia Dodoma utasaidia kupunguza msongamano hapa Dar es Salaam.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana;

Licha ya hatua tunazozichukua, ni dhahiri kuwa tatizo la msongamano haliwezi kumalizika kwa siku moja. Lakini napenda niwahakikishie kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inalimaliza tatizo hilo. Hivyo basi, wito wangu kwenu ni kwamba tuendelee kushikamana na kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo nchini mwetu. Nimefurahi hapa tupo watu kutoka vyama vyote, ikiwemo Mheshimiwa Lipumba wa CUF na Mstahiki Meya Mwita wa CHADEMA, na pia wapo watu wasio na vyama hivi ndivyo inapaswa kuwa. Maendeleo hayana chama.   

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwaomba wahusika wote kusimamia vizuri mradi huu. Kwa bahati mbaya, katika taarifa zilizosomwa na Waheshimiwa Mawaziri pamoja Kiongozi wa DART hazikuonesha namna mradi huu unavyoendelea. Kama tunapata faida au la. Hivyo basi, natoa changamoto kwa wahusika wote kuandaa taarifa hiyo na nitafurahi kama nitaipata leo. Ndiyo, niipate leo. Mradi huu umegharimu fedha za walipa kodi wa Tanzania, hivyo wanayo haki ya kufahamu utendaji kazi wake.   Lakini niseme tu kuwa binafsi sitegemei kuwa mradi huu utaendeshwa kwa hasara. Ni lazima uendeshwe kwa faida. Na kama hivyo ndivyo, kama ningepata taarifa hiyo, huenda leo ningeagiza kiasi cha fedha kilichopatikana kitumike katika kujenga Kituo Kikubwa cha Kupaki Magari na pia Kituo cha Usafiri wa Daladala pale Kimara ili kuwaondolea usumbufu watumiaji wa usafiri huu wa mwendokasi.

 

Sambamba na hilo, ni lazima vyombo husika vihakikishe kuwa  mradi huu unatunzwa na unatimiwa vizuri ili uweze kudumu. Sheria za barabarani ni lazima zifuatwe. Watu watakaobainika kuharibu au kuingilia miundombinu hii ni lazima wachukuliwe hatua kali. Huu ni mradi wa kipekee Barani ya Afrika hivyo ni lazima tuulinde. Aidha, tukumbuke ya kuwa miundombinu ya barabara iliyojengwa na mingine itakayojengwa imetumia fedha nyingi. Hivyo basi kila mmoja wetu hana budi kuutunza mradi huu. Tukumbuke ule usemi wetu usemao “kitunze, kidumu”au “kitunze kikutunze”.

Waheshimiwa Viongozi;

Mheshimiwa Dkt. Diop ;

Mabibi na Mabwana;

Kazi kubwa iliyonileta hapa leo ni kuzindua Mradi huu wa Mabasi ya Mwendo Kasi Awamu ya Kwanza. Hivyo, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Naomba niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kuwashukuru washirika wetu Benki ya Dunia na watendaji wote waliofanikisha ujenzi wa mradi huu. Napenda niwahakikishie Benki ya Dunia na wafadhili wote kwa ujumla fedha mnazotupatia zitatumika kwa makusudi yaliyopangwa. Nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wa Kamati zote husika, Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Madiwani, wana-Dar es Salaam na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kuiunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ninayoiongoza. Kwa Wabunge na Madiwani wa Dar es Salaam ningependa kuwahimiza kumaliza majadiliano kuhusu fedha zilizotolewa na Simon Group katika kipindi cha wiki moja ili zitumike katika shughuli za maendeleo ya wana-Dar es Salaam.

 

Napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa Ujenzi na TAMISEMI na vyombo vyote husika kwa kusimamia mradi huu. Wito wangu kwenu, simamieni vizuri mradi huu. Ni lazima mradi huu uendeshwe kwa faida. Kamwe asitokee mtu wa kutaka kujinufaisha kupitia mradi huu. Aidha, niwashukuru viongozi wa vyama vya siasa na dini kwa kujitokeza kwenye shughuli hii. Halikadhalika, nawashukuru wanahabari kwa kuendelea kuwaelimisha na kuwapasha habari Watanzania kuhusu shughuli mbalimbali za maendeleo.

 

Baada ya kusema hayo sasa niko tayari kufungua rasmi Miundombinu na Utoaji wa Huduma katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika Jiji la Dar es Salaam.

 

Mungu Wabariki Wana-Dar es Salaam!

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu bariki mahusiano mazuri kati yetu na Benki ya Dunia!

 

“Asanteni Sana kwa Kunisikiliza”.