Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA JENGO LA JULIUSU NYERERE LA UMOJA WA AFRIKA ADDIS ABABA, ETHIOPIA, 29 JANUARI, 2017

Sunday 29th January 2017

Mheshimiwa Idris Deby Itno, Rais wa Chad na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika;

Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali mliopo;

Mheshimiwa Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika;

Waheshimiwa Mawaziri na Mabalozi Mliopo;

Waheshimiwa Wageni Waalikwa wote;

Mabibi na Mabwana:

         Najisikia furaha na heshima kubwa kupata fursa ya kuzungumza katika tukio hili kubwa na muhimu la kumuenzi Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Viongozi wote wa Umoja wa Afrika kwa uamuzi wenu wa kulipa Jengo hili Jipya la Baraza la Amani na Usalama jina la Julius Nyerere ili kumuenzi.  Lakini kwa kipekee kabisa, napenda nimshukuru Mheshimiwa Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe, ambaye wakati uamuzi huu unafanyika alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Kwa pamoja, nawashukuruni wote.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana;

Kama ambavyo walivyosema wazungumzaji walionitangulia, Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mahiri na shupavu. Alikuwa Mwafrika Halisi. Na kwa hakika, naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye wamewahi kutokea katika Bara letu. Katika maisha yake yote, Mwalimu Nyerere alipambana kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Waafrika. Alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa Umoja huu. Sisi Watanzania kwa hakika, tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa letu.

Lakini sio kwamba Mwalimu Nyerere alipigania umoja na mshikamano pekee. Alisimama pia kidete katika kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina. Kama ambavyo wengi wenu hapa mnatambua, Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere ilitoa mchango mkubwa katika harakati za kuondoa ukoloni na ubaguzi wa rangi Barani Afrika. Nchi yetu ilikuwa mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU kwa kipindi chote, tangu ilipoanzishwa mwaka 1964 hadi ilipovunjwa mwaka 1994, baada ya ubaguzi wa rangi kukomeshwa nchini Afrika Kusini. Kwa kipindi chote tulichokuwa wenyeji wa Kamati hii ya Ukombozi, ardhi ya Tanzania ilitumika kwa ajili ya kutoa hifadhi, kuandaa mipango na mikakati na kutoa mafunzo kwa wapigania uhuru. Na ningependa nitumie fursa hii kuwaeleza kuwa Watanzania wamekuwa wakijisikia furaha sana kwa nchi yao kuweza kutoa mchango huu kwenye Bara letu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana;

Baada ya Baba wa Taifa kung’atuka katika hatamu ya uongozi wa Taifa aliendelea kutoa mchango wake kwenye Bara letu katika nyadhifa mbalimbali. Na kama mnavyofahamu, wakati mauti yanamkuta mwezi Oktoba mwaka 1999, alikuwa Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi. Na kwa sababu hiyo, binafsi naona kuwa heshima hii ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kulipa Jengo hili la Baraza la Amani na Usalama jina lake, ni muafaka kabisa. Hii ni namna nzuri kabisa ya kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa sio mpigania haki pekee bali pia amani. Napenda kutumia fursa hii kuarifu kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania italeta kinyago cha Mwalimu Nyerere ili kupamba Jengo hili.

 

Wito wangu kwenu Waheshimiwa Viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa Jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa Bara hili, wakiwemo Hayati Kwameh Nkhrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kumsahau shujaa wetu mwingine Nelson Mandela. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumejitendea haki sisi wenyewe lakini pia mchango mkubwa uliotolewa na viongozi hawa waasisi wa Bara letu utadumu na kurithishwa vizazi kwa vizazi. Na kwa sababu hiyo, mimi nikiwa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naahidi kuwa nitajitahidi kufuata nyayo sio tu za Mwalimu Nyerere bali viongozi wote waasisi wa Bara letu ambao walijitolea maisha yao kwa manufaa ya Bara hili. Natambua kufuata nyayo za viongozi hawa sio rahisi lakini naahidi kujitahidi.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

Waheshimiwa Viongozi;

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamisheni,

Mabibi na Mabwana;

Siwezi kuhitimisha hotuba yangu hii fupi bila kutoa shukrani zangu nyingi kwa Serikali na Wananchi wa Shirikisho la Ujerumani. Hawa ndiyo waliotoa fedha zilizowezesha ujenzi wa jengo hili imara na la kisasa kabisa. Tunawashukuru sana ndugu zetu wa Ujerumani. Nina matumaini makubwa kuwa Jengo litatoa mchango mkubwa katika kutafuta amani lakini kuwa na  Afrika isiyo na migogoro.

Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda niishukuru Serikali ya Ethiopia kwa kuridhia ujenzi wa Jengo hili kujengwa kwenye ardhi yake.

 

“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”