Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA WAKUU WA NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAKATI WA KUFUNGA MKUTANO MAALUM WA 17 WA WAKUU WA NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI DAR ES SALAAM, TANZANIA, TAREHE 8 SEPTEMBA, 2016

Thursday 8th September 2016

Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda;

 

Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda;

 

Mheshimiwa William Ruto, Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya;

 

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar

na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

 

Mheshimiwa Alain Aime Nyamitwe, Waziri wa Mambo

ya Nje wa Jamhuri ya Burundi;

 

Mheshimiwa Aggrey Tisa Sabuni, Mjumbe Maalum na

Mwakilishi wa Rais wa Sudan Kusini;

 

Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Mwenyekiti

wa Baraza la Mawaziri wa EAC;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa;

 

Mheshimiwa Balozi Liberat Mfumukeko, Katibu Mkuu wa EAC;

 

Mheshimiwa Dan Kidega, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki;

 

Mheshimiwa Jaji Dkt. Emmanuel Ugirashebuja,

Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kimataifa;

 

Wageni Waalikwa;

 

Mabibi na Mabwana;

 

Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninayo furaha kubwa kuwakaribisha wageni wote hapa nchini kwetu na hususan katika Jiji hili la Dar es Salaam. Kipekee kabisa, napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa, Viongozi Wenzangu kwa kukubali mwaliko wangu wa kuhudhuria Mkutano huu Maalum. Uwepo wenu hapa leo ni ishara tosha ya mshikamano uliopo katika Jumuiya yetu. Aidha, huu ni uthibitisho wa azma tuliyonayo sisi viongozi wa Jumuiya kuhakikisha ukanda wetu unakuwa na amani, utulivu na maendeleo.

 

Kabla sijaendelea, napenda kutumia fursa hii pia kuipongeza Sekretarieti ya Jumuiya yetu chini ya uongozi mahiri wa Balozi Liberat Mfumukeko kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu.  Sote tunafahamu, huu ni Mkutano wa Kwanza wa Jumuiya yetu unafanyika tangu Balozi Mfumukeko kuanza kazi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya yetu hapo mwezi Aprili mwaka huu. Lakini kwa kile ambacho tumeshuhudia mpaka sasa, ni dhahiri kuwa Balozi Mfumukeko anastahili pongezi nyingi.  Rai yangu kwake aendeleze mwanzo huu mzuri ili kuleta maendeleo kwa wananchi wetu na Jumuiya yetu kwa ujumla.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Mkutano huu Maalum unafanyika kwa ajili ya shughuli mahsusi. Kwa hakika, tumekutana hapa kujadili ajenda tatu muhimu kwa maendeleo ya Jumuiya yetu. Ajenda hizo ni: Ripoti ya Baraza la Mawaziri kuhusu masuala yanayohusu Sudan Kusini; Ripoti ya Rais Mstaafu Benjamini Mkapa ambaye ni Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi; na Ripoti ya Baraza la Mawaziri kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya yetu na Jumuiya ya Ulaya. Napenda kutumia fursa hii, kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na Baraza letu la Mawaziri wa Jumuiya chini ya Mwenyekiti wake Balozi Dkt. Mahiga katika kuandaa Mkutano huu. Mmefanya kazi kubwa sana na kwa hakika, mmeturahisishia sana kazi yetu katika Mkutano huu.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

         Kama mnavyofahamu, Mkutano wa Kawaida wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya yetu uliofanyika Arusha tarehe 2 Machi, 2016 kwa kauli moja ulipitisha uamuzi wa kukubali ombi la Sudan Kusini kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kulingana na uamuzi huo, tarehe 15 Aprili, 2016 katika ukumbi huu huu, mimi kwa wadhifa wangu wa Uenyekiti wa Jumuiya nikiwa pamoja na Mheshimiwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, tulisaini Mkataba wa Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya. Baada ya hapo, Serikali ya Sudan Kusini imewasilisha Hati ya Kuridhia (Instrument of ratification) Mkataba kwenye Sekretarieti ya Jumuiya. Hiyo inamaanisha kuwa hivi sasa nchi ya Sudan Kusini ni mwanachama kamili, mwenye haki zote na wajibu katika Jumuiya yetu.   Nimeambiwa kuwa Sekretarieti kwa sasa inakamilisha Mpango Kazi kwa ajili ya kuiwezesha nchi hiyo kujumuishwa kwenye mipango na miradi ya Jumuiya.

 

Kwa niaba ya Jumuiya, napenda kwa mara nyingine tena kuipongeza Sudan Kusini kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya yetu. Kwa heshima ya tukio hili, naomba tuwapongeze kaka na dada zetu wa Sudan Kusini kwa kupiga makofi mengi kufuatia nchi yao kujiunga rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Pamoja na furaha kubwa tuliyo nayo kuikaribisha Sudan Kusini kwenye Jumuiya, wananchi wa Afrika Mashariki tulishtushwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kuibuka upya kwa mapigano nchini humo. Napenda kutumia fursa hii, kuwaomba viongozi na wananchi wa Sudan Kusini kwa ujumla kuweka maslahi ya taifa lao mbele ili kumaliza mgogoro nchini humo. Suala hili ni muhimu sana kwa sababu kuimarika kwa amani na usalama kutaleta manufaa kwa wananchi wa nchi hiyo na kwenye ukanda wetu wote. Ni kwa sababu hii, napongeza kazi kubwa iliyofanywa na IGAD kurejesha amani na utulivu nchini Sudan Kusini. Na kwa bahati nzuri, nchi nyingi za Jumuiya yetu ni wanachama wa IGAD. Hivyo basi, nina uhakika kuwepo kwao katika IGAD, kumewezesha na kutaendelea kuwezesha mawazo na maoni yetu kuwasilishwa vizuri kwenye usuluhishi wa mgogoro huo.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Kuhusiana na Burundi, kama ambavyo sote tunafahamu vizuri, nchi hiyo imekuwa kwenye mgogoro wa kisiasa kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa. Mgogoro huo umesababisha madhara mengi, ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha ya wananchi wasio na hatia. Napenda kutumia fursa hii, kwa niaba ya Jumuiya, kutuma tena salamu nyingi za pole na rambirambi kwa Serikali, ndugu na wananchi wote wa Burundi kufuatia kifo cha mwakilishi wao kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Marehemu Hafsa Mossi, aliyeuawa tarehe 13 Julai, 2016. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.

 

Licha ya changamoto zinazoendelea kuikabili Burundi, Jumuiya yetu imeendelea na jitihada za kurejesha amani nchini humo. Hii ndiyo sababu, katika Mkutano wetu wa 17 uliofanyika mwezi Machi 2016 mjini Arusha, tulimteua Rais Mstaafu wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kuwa Mpatanishi wa Mazungumzo ya Amani ya Burundi. Mpatanishi amefanya mikutano kadhaa mjini Arusha na Brussels nchini Ubelgiji kwa kuwakutanisha wadau wakubwa katika mgogoro wa Burundi. Leo tumepokea Taarifa ya Msuluhishi ambayo imetoa mapendekezo kadhaa ya kumaliza mgogoro. Tumeyapokea na kuyakubali mapendekezo yote. Lakini kwa ujumla tu naweza kusema kuwa Taarifa tuliyoipokea inatoa matumaini ya kurejea kwa amani nchini Burundi.

 

    Nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa jitihada zake za kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini Burundi. Nawahimiza wahusika nchini Burundi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mpatanishi (Facilitator) na halikadhalika kwa Msuluhishi (Mediator), Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. Niwaombe pia viongozi wenzangu wote tuendelee kutoa michango yetu ya hali na mali kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi. Kurejea kwa amani nchini Burundi, kutawezesha Wana-Burundi kuelekeza nguvu zao kwenye shughuli za maendeleo kwa manufaa ya nchi yao na Jumuiya yetu kwa ujumla. Nitumie fursa hii pia, kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia na kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Msuluhishi.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Naomba sasa nieleze suala la Mkataba wa Ubia wa Biashara kati ya Jumuiya yetu na Jumuiya ya Ulaya (EAC-EAC Economic Partnership Agreement – EPA). Kama mnavyofahamu, EPAs ni Mikataba ya Biashara baina ya Jumuiya ya Ulaya na nchi kutoka Afrika, Caribbean na Pacific. Lengo kuu la mikataba hii ni kuwezesha nchi maskini kutoka Afrika, Caribbean na Pacific kuingia kwenye uchumi wa dunia. Malengo mahususi ya EPA, ni kukuza ushirikiano wa kikanda, biashara ya bidhaa na maendeleo.

 

Majadiliano kati ya EAC na EU yalianza mwaka 2007. Majadiliano haya yalikamilika kwa kupatikana kwa EAC-EU-EPA, ambayo ilitarajiwa kukasainiwa mwaka huu. Kusainiwa na kuridhiwa kwa Mkataba huu, kutawezesha bidhaa kutoka Jumuiya ya Ulaya  kuingia kwenye soko la Afrika Mashariki bila vikwazo chochote (free-access) na kwa upande wetu tutanufaika na viwango vya chini vya tozo (tariffs) zitakazotozwa bidhaa zitakazoingia kwenye soko la Jumuiya ya Ulaya. Napenda kukiri kuwa suala hili la EPA limechukua muda mwingi wa majadiliano yetu leo. Lilikuwa ni suala gumu kidogo.

 

Katika majadiliano yetu, yapo maswali mengi ambayo tulijiuliza, hususan kuhusu nini kitatokea au athari zipi zitatupata endapo Jumuiya yetu itasaini EPA. Baadhi ya maswali tuliyojiuliza ni haya yafuatayo:

 

Moja, Ni kwa namna gani Jumuiya yetu itaweza kulinda viwanda vya ndani na kukuza sekta ya viwanda katika mazingira ya ushindani mkubwa utakaotokana na kuruhusiwa kwa bidhaa nyingi za viwandani kutoka Jumuiya ya Ulaya kuingia katika soko la jumuiya yetu? Mathalan, Tanzania inalenga kujenga uchumi wa viwanda, lakini kupitia EPA, Tanzania italazimika kufungua soko lake kwa bidhaa nyingi za viwandani kutoka Jumuiya ya Ulaya. Je ufunguaji huu mkubwa wa soko letu kwa bidhaa kutoka Jumuiya ya Ulaya ambazo zimetengenezwa kwa gharama ya chini na teknolojia ya kisasa utakuwa na athari gani katika harakati za nchi yetu na Jumuiya yetu kwa ujumla kujenga na kukuza uchumi wa viwanda?

 

Pili, Je ni kwa namna gani tutaweza kuzuia Jumuiya yetu isigeuzwe kuwa soko la bidhaa za kilimo kutoka Ulaya? Na ni njia zipi tutazitumia  kuwalinda wakulima wetu na sekta yetu ya kilimo kwa ujumla, ambayo kwa sasa ndiyo sekta kuu ya uchumi katika nchi zetu, hasa kwa kuzingatia ruzuku kubwa inayotolewa na Serikali za Ulaya kwa wakulima wake na pia kutokana na matumizi ya dhana za kisasa zinazotumiwa na wakulima wa Ulaya?

 

Tatu, Ni kwa namna gani tutaweza kukabiliana na tatizo la kukosekana kwa urari wa biashara kwa upande wetu, unaotokana na sisi kuendelea kuuza bidhaa ghafi kwenye soko la Ulaya?

 

Nne, Je, ni kwa namna gani nchi zetu katika Jumuiya zitaweza kuziba pengo la kuondoka kwa mapato ya kodi ambayo hivi sasa tunakusanya kutokana na bidhaa zinazoingia kutoka kwenye Jumuiya ya Ulaya? Mathalan, utafiti uliofanywa na Shirika la Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (the Economic and Social Research Foundation) mwaka 2009 ulibainisha kuwa endapo Tanzania itatia saini EPA itapoteza takriban asilimia 45 ya mapato kutoka Jumuiya ya Ulaya katika kipindi cha miaka 20 tangu kusainiwa kwa EPA.

 

Tano, Je ni kwa kiwango gani uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye EU utaathiri EPA hasa kwa kuzingatia kuwa Uingereza ilikuwa ni soko kubwa la bidhaa nyingi kutoka kwenye Jumuiya yetu? Kwa mfano, takwimu zinaonesha kuwa kati ya bidhaa zote ambazo Tanzania ilipeleka katika Jumuiya ya Ulaya katika kipindi cha mwaka 2002 hadi 2014, asilimia 21 ya bidhaa hizo zilikwenda kwenye soko la Uingereza. Aidha, kwa mujibu wa takwimu nilizonazo, asilimia 28 ya bidhaa zote kutoka Kenya kwenda kwenye Jumuiya ya Ulaya zinauzwa kwenye soko la Uingereza. Tulijiuliza pia kama nchi za Marekani na Canada zimeanza kutafakari upya ushirikiano wake wa kibiashara na Jumuiya ya Ulaya baada ya uamuzi wa Uingereza kujitoa, iwejesisi tusitafakari suala hili?

 

Sita, Je ni namna gani tutaweza kushughulikia suala la Upendeleo Maalum (Most Favoured Nations Clause), ambapo katika Ibara 15 (2) ya EPA, nchi za EAC zinazuiwa kuingia kwenye ushirikiano wa kibiashara au kutoa upendeleo maalum kwa nchi zinazoibukia kiuchumi ambazo hazina ushirikiao na kiuchumi na Jumuiya ya Ulaya?  Kipengele hiki kinakwenda kinyume na malengo ya kipengele wezeshi (Enabling clause) cha Shirika la Biashara Duniani (World Trade Organization) ambacho kinahimiza kutolewa kwa upendeleo maalum kwa nchi zinazoendelea na ushirikiano wa nchi za Kusini (South South Cooperation);

 

Saba, Je takwa la kwamba nchi za EAC zitoe fursa sawa za EPA kwa nchi na jumuiya zote zenye Mikataba ya Forodha na Jumuiya Ulaya lina athari gani kwa nchi zetu?

 

Nane; Je ni kwa namna gani tutashughulia suala la kukosekana kwa uhuru wa kisera katika kuweka kodi (Restrictions on Duties and Taxes on Exports)?  Kama tunavyofahamu, kodi na tozo kwa bidhaa kwenda nje, hususan tozo kwenye bidhaa ghafi, ni njia mojawapo ya kuimarisha sekta ya viwanda na upatikanaji wa ajira. Kodi na tozo za namna hii kwa kiasi fulani zinawalazimisha wasafirishaji wa bidhaa ghafi kwenda nje kuongezea thamani bidhaa zao kabla ya kuzisafirisha kwenda nje ya nchi. Aidha, tozo na kodi hizo zinasaidia kuhakikisha uwepo usalama wa chakula katika nchi. Sasa je, uhuru wa kuweka kodi hizo ukiondoka kama ambavyo EPA inaelekeza, tutawezaje kusimamia suala la uongezaji thamani wa bidhaa ghafi kwenda nje na pia kuhakikisha usalama wa chakula katika nchi zetu?

 

Tisa, Ni njia zipi zitatumika kuzisaidia nchi ambazo, kwa kuendelea kubaki kwenye EPA, itathibitika dhahiri kuwa maslahi yake yanaathirika kwa kiwango kikubwa na hasa kwa kuzingatia kuwa EPA hautoi fursa kwa nchi moja peke yake kujitoa? (Mkataba unaitambua Jumuiya);

 

Kumi,  Ipo haja gani kwa Burundi kusaini EPA wakati imewekewa vikwazo vya biashara na Jumuiya ya Ulaya?

 

Kwa hakika tulijiuliza maswali mengi na mjadala ulikuwa mzito. Lakini kama ilivyo kawaida katika Jumuiya yetu, kila linapotokea jambo lenye maslahi makubwa kwetu sote, hata kama ni ugumu kiasi gani, tumekuwa na utaratibu wa kufanya mazungumzo na mashauriano na hatimaye kuweza kufikia muafaka. Na wakati mwingine, hata kama tukishidwa kupata muafaka wa pamoja, tumekuwa tukitafuta njia ambayo itatusaidia kupata ufumbuzi. Kwa mara nyingine tena leo tumedhihirisha umoja na mshikamano wetu.

 

 Baada ya mazungumzo ya marefu tuliyoyafanya kwa njia ya urafiki na uwazi mkubwa, tumeweza kupata njia ya kushughulikia suala la EPA. Mambo muhimu tuliyokubaliana kuhusu suala hili ni, kwanza, kujipa muda wa miezi mitatu kufanya mazungumzo zaidi kati yetu kwa lengo la kupata ufumbuzi na muafaka. Pili, kuiomba Jumuiya ya Ulaya kutoiadhibu Kenya kwa kuanza kutoza kodi bidhaa zake zitakazoingia kwenye soko lake ifikapo mwezi Januari 2017. Tatu, tumeiagiza Sekretarieti kuwasilisha uamuzi huu kwenye Jumuiya ya Ulaya. Na nne, baada ya miezi mitatu, tutakutana tena ili kufanya uamuzi wa pamoja wa Jumuiya yetu kuhusu suala la EPA. Haya ndiyo maamuzi yetu na nina imani Jumuiya ya Ulaya itatuelewa na kuyazingatia maombi yetu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Itakuwa si jambo la busara kwangu kuhitimisha hotuba yangu bila kutoa pongezi zangu nyingi na za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Christophe Bavivamo kutoka Rwanda, ambaye amechaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya yetu. Nakupongeza sana Mheshimiwa Bavivamo. Nina imani kuwa  mawazo, maono, mtazamo na uzoefu mpya unaokuja nao, utasaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika jumuiya yetu.  Kwa niaba ya Jumuiya, nakuahidi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yako mapya ya Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya.

 

Baada ya kusema hayo, naomba kuwakaribisha tena hapa nchini kwetu na nina imani kubwa kuwa, kwa muda mfupi mtakaokuwepo, mtalifurahia Jiji letu la Dar es Salaam.

 

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”