Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA HAFLA YA KUPOKEA TAARIFA YA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI WA MWAKA 2015 IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 23 JUNI 2016

Thursday 23rd June 2016

 

Mheshimiwa Jaji (Mst) Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi;

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Mheshimiwa Zuber Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar;

Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

Waheshimiwa Marais Wastaafu;

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu;

Mheshimiwa Jecha Salum Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar;

Waheshimiwa Mawaziri;

Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa;

Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi;

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya siasa;

Waheshimiwa wa Wawakilishi wa Asasi za Kiraia;

Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa wazima. Aidha, napenda kutoa shukran zangu za dhati kwa Mwenyekiti na uongozi mzima wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kunialika katika hafla hii fupi ya kunikabidhi Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika hapa nchini mwezi Oktoba mwaka jana. Nimearifiwa kuwa tukio hili ni kwa mujibu wa utamaduni uliokuwekwa na Tume kwamba kila baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu, Tume huwasilisha Taarifa kwa Rais. Naipongeza Tume kwa kubuni na kuenzi utamaduni huu.

Kwa kipekee kabisa, napenda kuwashukuru Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na wageni wote waalikwa mliojitokeza kwa wingi mahali hapa. Uwepo wenu hapa ni kielelezo tosha kuwa mnatambua na kuthamini umuhimu wa tukio hili. Ahsanteni sana.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Wageni Waalikwa;

Ndugu Viongozi;

Uchaguzi ni tukio muhimu katika nchi. Ni tukio linaloashiria kukua kwa demokrasia katika nchi. Kupitia uchaguzi, wananchi hupata fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa hiari.  Hata hivyo, uchaguzi usiposimamiwa vizuri unaweza kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa na vurugu katika nchi. Ipo mifano mingi ya namna chaguzi katika nchi mbalimbali zimevuruga amani. Sina haja ya kuitaja.  

Mwezi Oktoba mwaka jana nchi yetu ilifanya Uchaguzi wake Mkuu. Mtakubaliana nami kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni wa kipekee sana. Ulikuwa wa kipekee kwa sababu kubwa mbili. Mosi, uchaguzi huu ulikuwa ni wa kwanza kufanyika kwa kutumia Mfumo wa Kisasa wa Biometric Voter Registration (maarufu kama BVR). Hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ililazimika kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia Mfumo wa BVR. Ili kufanya kazi hiyo, Tume iliomba kupata vifaa vya BVR vipatavyo 15,000. Lakini kutokana na ufinyu wa bajeti, vilipatikana vifaa 8,000 tu. Licha ya upungufu huo wa vifaa na pia ufinyu wa muda, Tume iliweza kukamilisha kwa ufanisi mkubwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Idadi ya wapiga kura walioandikishwa ilikuwa ni 23,161,440 sawa na asilimia 96.9 ya wapiga kura 23,901,471 waliokadiriwa. Nawapongeza sana Tume kwa kufanikisha zoezi hili.

Sababu ya pili ni kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa na ushindani mkali. Ulikuwa wenye mvuto na msisimko wa kipekee ndani na nje ya nchi yetu. Kutokana na hali ya ushindani iliyokuwepo, baadhi ya watu walionesha wasiwasi kuwa huenda amani na utulivu katika nchi ingepotea. Hata hivyo, tulimaliza uchaguzi kwa salama. Nchi yetu imebaki kuwa yenye amani na tulivu mkubwa. Bila shaka, kukamilika vizuri kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ni matokeo ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Tume yetu ya Uchaguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa siasa pamoja na wananchi kwa ujumla.

Hivyo basi, kwa mara nyingine tena, napenda kutoa pongezi zangu nyingi kwako wewe Mheshimiwa Mwenyekiti, Jaji Mstaafu Lubuva pamoja na Sekretarieti ya Tume ikiongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndugu Kailima Ramadhani, kwa kusimamia na kuendesha vizuri Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.  Mlifanya kazi kubwa sana. Watazamaji wa Uchaguzi wengi kutoka ndani na nje ya nchi yetu wamekiri kuwa Uchaguzi wetu ulifanyika katika mazingira ya uwazi, uhuru, haki na amani. Aidha, nimearifiwa kuwa kutokana kusimamia vizuri zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa njia ya kieletroniki (BVR), baadhi ya nchi zimeonesha nia ya kutaka kujifunza kutoka kwenu. Naipongeza sana Tume.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Hakuna kizuri kisicho na kasoro. Hivyo basi, naamini zipo baadhi ya kasoro zilijitokeza kwenye Uchaguzi wa mwaka jana.  Jambo hili lisiwanyime raha. Ni suala la kawaida kabisa. Kama ambavyo wewe mwenyewe umetoka kusema hivi punde kuwa hakuna nchi hapa duniani imewahi kufanya uchaguzi bila ya kutokea kwa kasoro yoyote.

Pamoja na ukweli huo, natambua wametokea wakosoaji. Wakosoaji hao ni wa aina mbili. Kundi la kwanza ni la wakosoaji ambao wametaja mapungufu ya msingi kwa lengo la kuboresha chaguzi zetu zijazo. Naiomba Tume ipokee mapungufu waliyoyataja na kuyafanyia kazi ili uchaguzi ujao uwe bora zaidi. Kundi la pili ni la wakosoaji ambao kazi yao ni kukosoa. Hawa hata mngefanyaje wangekosoa tu. Hawana jema. Mtunzi wa Vitabu Maarufu wa Marekani, Ben Carson, alipata kusema, nanukuu “Even if you dance on water, Haters will accuse you of raising dust” (Hata ukicheza kwenye maji, wenye husda na wewe watasema unawatimulia vumbi), mwisho wa kunukuu.

Kwa wakosoaji wa namna hii, ili uchaguzi uonekane kuwa huru na haki ni lazima Chama Tawala kishindwe. Kikishinda, basi uchaguzi unakuwa sio huru. Ninyi wenyewe mmejionea wakati wanawalaumu ninyi kwa mapungufu yaliyojitokeza, kule Zanzibar wanailaumu ZEC kwa kufuta uchaguzi ambao ulidhihirika kuwa una mapungufu. Lakini mimi sishangai. Maana hii ndio imekuwa tabia yao. Wakosoaji wa namna hii nawafananisha na wale watu ambao wamekuwa wakizunguka kila siku sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi wakilaumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia masuala ya ndani ya Zanzibar. Ndio watu hao hao wamekuwa wakijinasibu kuwa wanataka Tume huru ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Lakini cha kustaajabisha ni kwamba baada ya ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar, wakanitaka mimi niingilie kati ili kutengua maamuzi ya ZEC. Wakajisahaulisha kuwa Zanzibar ina mamlaka yake na ZEC ni chombo huru ambacho maamuzi yake hayaingiliwi na mtu au chombo chochote.

Mimi niliwaambia hapana maana naheshimu Katiba na sheria. Naheshimu mamlaka ya Zanzibar na uhuru wa ZEC. Lakini niliwaahidi kwamba ningehakikisha Zanzibar inabaki kuwa salama na amani.  Ninafurahi nimetekeleza ahadi yangu. Uchaguzi wa marudio Zanzibar umefanyika huku amani na utulivu ukiendelea. Nitumie fursa hii kuwapongeza ZEC na wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi wa marudio kwa usalama na utulivu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti;

Mabibi na Mabwana;

Uchaguzi sasa umekwisha. Lakini mtakubaliana nami kuwa mwisho wa uchaguzi mkuu mmoja ndio mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine. Nafahamu ipo dhana iliyojengeka katika jamii yetu kuwa mwisho wa uchaguzi unaashiria pia mwisho wa kazi za Tume. Dhana hii si sahihi hata kidogo. Tume ya Uchaguzi ni taasisi ya kudumu. Kazi zake zinaendelea kama kawaida. Mathalan, kwa mujibu wa kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Tume ya Uchaguzi, sura ya 343, Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi mmoja na mwingine. Lakini pia Tume inao wajibu wa kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura na pia kusimamia chaguzi ndogo ndogo zinazojitokeza. Kwa mantiki hiyo, niiombe Tume kuanza mapema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Natambua zipo changamoto zinazokabili Tume katika kutekeleza majukumu yake hivi sasa. Mwenyekiti wa Tume amezitaja baadhi ya changamoto hizo hivi punde, ikiwemo ufinyu wa bajeti, ukosefu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi na ukosefu wa ofisi. Changamoto nyingine zinahusu masuala ya kisheria. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imepokea changamoto hizi na tutazifanyia kazi. Tutatilia maanani pendekezo la Tume kuhusu kuanzisha Mfuko wa Uchaguzi. Mimi binafsi naliona pendekezo hili kuwa ni zuri sana. Mfuko huo ukianzishwa, utatoa fursa kwa Serikali na wadau wengine kuweza kuchangia kila mwaka na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa fedha kwa Tume, hasa nyakati za Uchaguzi Mkuu.

Lakini niseme tu kuwa kati ya changamoto mlizozitaja ipo moja ambayo imenigusa sana. Changamoto hiyo inahusu Tume kukosa jengo la ofisi. Mimi nilishuhudia ukubwa wa changamoto hii wakati nikichukua na kurudisha fomu za kuwania Urais mwaka jana. Nakiri kwa dhati kabisa kuwa mahali ilipo Ofisi ya Tume hivi sasa sio muafaka. Baya zaidi ni kwamba ofisi hiyo ipo kwenye jengo la kupanga. Tena sio kwenye jengo moja, mmepanga kwenye majengo matatu. Hii si sawa hata kidogo. Kwanza ni gharama. Nimearifiwa kuwa katika majengo matatu mliyopanga mnalipa takriban shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka.  Lakini kubwa zaidi ni kwamba kutokana na unyeti wa shughuli zake, Tume haipaswi kuwa kwenye jengo la kupanga. Hivyo, kama nilivyoahidi wakati Tume iliponikabidhi hundi ya kurejesha bakaa ya shilingi bilioni 12 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, nitahakikisha bakaa hiyo inarejeshwa kwa Tume ili ituike kwa ujenzi wa ofisi. Naamini fedha hizi zikitumika vizuri zitatosha kabisa kujenga jengo zuri na la kisasa. Lakini ningependa kurudia ombi langu kwa Tume kuwa, kama mtaona inafaa, basi jengo hilo la ofisi lijengwe kwenye Makao Makuu ya nchi yetu mjini Dodoma.

Mkijenga Dodoma mtakuwa mnatekeleza ndoto ya Baba wa Taifa letu ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi yetu. Lakini kwa kuwa Dodoma ni katikati ya nchi itakuwa rahisi kwenu kufika kwenye maeneo mbalimbali ya nchi tena tena kwa haraka. Aidha, wadau wenu mbalimbali nao itawawia rahisi kuwafikia ninyi lakini pia mtasaidia kupunguza tatizo la foleni hapa Dar es Salaam.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti;

Katika hotuba yako, umezungumza kwamba baada ya uchaguzi kumalizika, sasa Tume inataka kujielekeza kwenye suala mchakato wa Katiba Mpya ambao ulibaki kiporo kutokana na kuingiliwa na ratiba ya uchaguzi. Hilo ni jambo jema ambalo binafsi naunga mkono. Mchakato wa Katiba Mpya ulifikia mahali pazuri hivyo ni vyema tukaumalizia. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein; Mweyekiti wa Bunge la Katiba, Mzee Samweli Sitta na Makamu wake, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Joseph Warioba kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kufikia hatua tulipo sasa. Naahidi kuhakikisha kumalizia sehemu iliyosalia. Hivyo, kama ulivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba muanze kuchukua hatua mahsusi pamoja na taratibu zinazohitajika ili mtakapozikamilisha, Serikali iendelee na taratibu nyingine za kumalizia mchakato huo. Ni azma ya Serikali kuona mchakato huo unakamilika kwa muafaka ili kupata Katiba nzuri.  

 

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kwa ajili ya kushuhudia makabidhiano ya Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Hivyo, haitakuwa busara kwangu kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu napenda kusema jambo moja la mwisho.

Kama nilivyosema hapo awali sasa uchaguzi umekwisha. Ni kweli katika uchaguzi uliopita, kama ilivyo kawaida kwenye nchi za vyama vingi, watu mbalimbali kupitia vyama vyao walijitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na baadhi yetu kuibuka washindi. Lakini kwa mtazamo wangu na bila shaka huu ni mtazamo wa Watanzania waliowengi kuwa katika uchaguzi huo hakuna aliyeshindwa. Watanzania wote kwa umoja wetu ni washindi. Hivyo, ni vyema sasa tukajielekeza kwenye kuchapa kazi ili kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Tuache kuendeleza kampeni na siasa zisizo na tija. Itakuwa vyema kama siasa sasa zitahamia Bungeni ama kwenye vikao vya madiwani.

Watanzania wana uchu wa maendeleo. Watanzania wanataka maisha bora. Watanzania wanataka kuona kero zao mbalimbali zinaondolewa na Serikali iliyopo madarakani. Sisi tuliyopewa dhamana ya kuongoza Serikali kuna mambo tuliyowaahidi wananchi kuwa tutayatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Tunataka tutekeleze ahadi zetu. Sitakuwa tayari kuona mtu anatukwamisha kutekeleza yale tuliyowaahidi wananchi. Hivyo, nawaomba viongozi wenzangu, hususan viongozi wa siasa, tushirikiane katika kuwahamasisha wananchi wetu kufanya kazi ili azma ya nchi yetu ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 itimie. Serikali kwa upande wake ipo tayari kushirikiana na kupokea ushauri wa kila Mtanzania ili kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kurudia kutoa pongezi kwa Tume kwa kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Aidha, napenda kupongeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wagombea wa nafasi mbalimbali, Viongozi wa Vyama, Viongozi wa Dini, Wana-Habari na wananchi kwa ujumla kwa ushiriki wenu mzuri uliowezesha nchi yetu kumaliza uchaguzi salama. Nawapongeza pia viongozi wa siasa waliohudhuria tukio hili la leo. Mmeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Siasa si uadui.

Kipekee kabisa nawapongeza Marais Kikwete na Dkt. Shein kwa kusimamia vizuri uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru washirika wetu mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine walitoa michango ya hali na mali iliyowezesha Uchaguzi wa mwaka jana kufanyika kwa ufanisi, amani na utulivu. Tunatambua na kuthamini mchango wenu.

 

Mungu Ibariki Tume ya Taifa ya Uchaguzi!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Asanteni Kwa Kunisikiliza”