Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT, JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA DHIFA YA KITAIFA ALIYOIANDAA KWA HESHIMA YA MHESHIMIWA NARENDRA MODI, WAZIRI MKUU WA INDIA IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 10 JULAI, 2016

Sunday 10th July 2016

Mheshimiwa Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu Wastaafu mliopo;

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali, Vyama na Dini mliopo;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

         Awali ya yote, kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kukukaribisha Mheshimiwa Waziri Mkuu Narendra Modi pamoja na ujumbe wako hapa Dar es Salaam. Karibu sana nchini kwetu. Watanzania wengi walifurahi kusikia uamuzi wako wa kuijumuisha nchi yetu kwenye orodha ya nchi utakazozitembelea kwenye ziara yako hii ya pili  hapa Barani Afrika. Hivyo, kwa hakika, wamepokea ujio wako kwa mikono miwili na moyo mkunjufu. Tutajitahidi kuhakikisha sio tu kwamba unaifurahia ziara yako hapa nchini bali pia kuifanya iwe ya mafanikio makubwa.

 

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

         Licha ya umbali uliopo kati Tanzania na India, nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri tena wa muda mrefu. Sio tu kwamba tunaunganishwa na Bahari ya Hindi, bali pia uhusiano wetu ni wa kihistoria na kidugu. Zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, wafanyabiashara kutoka India wakitumia mashua na ngalawa waliingia hapa nchini kwa minajili ya kuendesha shughuli zao za kibiashara. Walifikia katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, ikiwemo Zanzibar na Kilwa. Baadhi yao walifanya biashara na kurejea India lakini wapo, tena wengi tu, waliolowea hapa nchini. Hawakurudi tena India. Huenda hii ndio sababu, miongoni mwetu hapa leo tunao Wabunge Kumi (10) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wana asili ya India.

 

         Uhusiano wetu ulizidi kukua baada ya Tanzania kupata uhuru, ukichagizwa zaidi na urafiki mkubwa uliokuwepo kati ya Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Jawaharlal Nehru, Waziri Mkuu wa India wa wakati huo. Chini ya viongozi hawa, Tanzania na India zilikuwa mstari wa mbele katika kupinga ukoloni na ubaguzi wa rangi, hususan katika Bara la Afrika. Mahusiano hayo yaliendelezwa na viongozi waliofuatia katika awamu zote za uongozi wa mataifa yetu mawili. Uhusiano huu mzuri pia upo kwenye anga za kimataifa, hususan kupitia Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Nchi zisizofugamana na Upande Wowote, Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association for Regional Cooperation) na hivi karibuni kupitia Jukwaa la Afrika na India lililoanzishwa mwaka 2008, ambapo kwenye kikao kilichoanzisha Jukwaa hilo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mzee Kikwete, ambaye nafurahi tuko naye hapa, alikuwa Mwenyekiti  Mwenza.

 

Mabibi na Mabwana;

Uhusiano wetu mzuri katika ngazi ya kitaifa na kimataifa umeziwezesha nchi zetu kushirikiana vizuri kiuchumi.          Na kwa hakika, naweza kusema kuwa India ni mdau wetu mkuu wa biashara. Biashara kati ya nchi zetu mbili imekuwa ikikua kila mwaka. Mathalan, mauzo ya bidhaa zetu kwenda India yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 187 mwaka 2009 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 1.29 mwaka 2015.  Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, tofauti na nchi nyingi ambazo tunafanya nazo biashara, urari wa biashara na India pia ni mzuri. Mathalan, kati ya Dola za Marekani Bilioni 3.5 ambazo ndio jumla ya thamani ya mauzo ya biashara kati ya nchi zetu kwa mwaka 2015, thamani ya bidhaa kutoka India ni Dola za Marekani Bilioni 2.4 wakati thamani ya mauzo ya Tanzania nchini India ni Dola za Marekani Bilioni 1.29. Aidha, uwekezaji kutoka India ambao umesajiliwa na Kituo chetu cha Uwekezaji una thamani ya Dola za Marekani Bilioni 2.4 na umezalisha ajira 54,176.

 

Ni dhahiri kuwa haya ni mafanikio makubwa. Sisi Watanzania hatuna budi kujivunia uhusiano wetu mzuri na India. Nina imani kuwa ziara hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Modi hapa nchini itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wetu katika masuala ya kiuchumi. Nafurahi kuwa katika kikao chetu na Waziri Mkuu leo asubuhi, tumekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo TEHAMA, kilimo, viwanda vidogo vidogo, elimu, afya, maji nk. Waziri Mkuu pia ameahidi kuwa India itatoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Lakini jambo la kutia moyo zaidi ni kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ujumbe wake ameambatana na Wafanyabiashara takriban 50. Wafanyabiashara hao  wamekutana na wenzao wa Tanzania asubuhi hii na sina shaka, siku chache zijazo tutaanza kuona mafanikio ya ziara hii.

 

Mheshimiwa Waziri Mkuu;

Ziara yako hapa nchini inafanyika wakati nchi yako ikielekea kuadhimisha miaka 70 ya Uhuru wake mwezi ujao. Bila shaka, wengi kama si wote waliopo hapa watakubaliana nami kuwa katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, India imepata mafanikio makubwa sana. India hivi sasa ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa. Ni miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiviwanda. Lakini pia mmepiga hatua kubwa katika masuala ya sayansi na teknolojia, hususan teknolojia ya habari. Mafanikio haya hayakujileta bali yametokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na viongozi wa India, ukiwemo wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kushirikiana na wananchi wenu. Napenda kutumia fursa hii kupitia kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwapongeza wananchi wa India kwa miaka 70 ya Uhuru wenu na pia kwa mafanikio makubwa mliyoyapata.

 

  Nchi nyingi kama si zote za Afrika zimenufaika sana na mafanikio ya India.  Sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na mafanikio mliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, maji, kilimo, TEHAMA n.k; kupitia ama misaada ya moja kwa moja au kwa njia ya ushirikiano. Lakini sambamba na kutunufaisha, mafanikio yenu yametupa fursa sisi Watanzania na Waafrika kwa ujumla kujifunza masuala mbalimbali, ikiwemo Programu zenu kama vile Skill India, Digital India, 100 Smart Cities na pia program mpya uliyoianzisha ya Make in India.  Napenda kukiri kuwa binafsi nimevutiwa sana na program hii ya Make in India ambayo inahimiza uwekezaji kwenye sekta ya viwanda vyenye kutumia malighafi, wataalamu/nguvu kazi kutoka ndani ya nchi. Programu hii imenivutia kwa vile dhima yake inafanana sana na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa nchi yetu, ambao unalenga kujenga uchumi wa viwanda. Viwanda tunavyovilenga katika Mpango huu ni vyenye kutumia malighafi za ndani, nguvu kazi kubwa na kuzalisha bidhaa zenye kutumika zaidi ndani ya nchi. Hivyo basi, naamini tutaweza kubadilishana uzoefu katika kutekeleza Mipango hii.

Mheshimiwa Makamu wa Rais;

Mheshimiwa Rais wa Zanzibar;

Mheshimiwa Waziri Mkuu;

Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu Wastaafu mliopo;;

Waheshimiwa Wageni Waalikwa mliopo;

Mabibi na Mabwana:

Kama nilivyodokeza hapo juu, leo asubuhi mimi na Waziri Mkuu tulipata fursa ya kufanya mazungumzo rasmi. Tumezugumza mambo mengi. Tumejadiliana kwa kirefu na kukubaliana namna ya kuboresha na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zetu. Kwa sababu hiyo, nisingependa kuwachosha kwa hotuba ndefu.  Na kwa hakika hapa sio mahali muafaka pa kutoa hotuba ndefu. Tupo hapa kwa ajili ya kufurahi na mgeni wetu, Waziri Mkuu Narendra Modi, pamoja na kusheherekea uhusiano mzuri na wa muda mrefu kati ya India na Tanzania.

 

Hivyo basi, kwa heshima na taadhima, niwaombe sote kwa pamoja tusimame na kisha tunyanyue glasi zetu ili tufurahie na mgeni wetu:

 

  • Kwa ajili ya afya nzuri ya Waziri Mkuu Narendra Modi;
  • Kwa ajili ya urafiki na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na India.

 

 “Ahsanteni kwa kunisikiliza”.