Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA KUANZISHWA KWA BENKI KUU YA TANZANIA DAR ES SALAAM, TAREHE 22 JUNI 2016

Wednesday 22nd June 2016

 

Mheshimiwa Dkt. Servacius Likwelile, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango;

Mheshimiwa Prof. Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;

Waheshimiwa Magavana wa Benki Kuu kutoka Nchi Wanachama wa SADC na EAC;

Waheshimiwa Magavana Wastaafu na Wajumbe wa Bodi ya Benki Kuu;

Wafanyakazi wa Benki Kuu mliopo;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

Napenda nianze kwa kutoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Gavana wa Benki Kuu kwa kunipa mwaliko ili niweze kujumuika nanyi katika Maadhimisho haya ya Miaka 50 tangu kuanzishwa Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, nawashukuru kwa kunipa fursa hii adimu ya kuzungumza katika hafla hii. Nafahamu hii si mara yangu ya kwanza kufika hapa tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba mwaka jana. Nilishafika hapa mara moja. Lakini ziara ile ya kwanza haikuwa rasmi.  ‘Nilivamia”. Hii ndio ziara yangu ya kwanza rasmi hapa. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kunipa kura nyingi zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya nchi yetu. Ahsanteni sana.

Nitumie fursa hii pia kuwashukuru wageni waalikwa wote mliohudhuria kwa kukubali kutenga muda wenu na kuja hapa kujumuika nasi. Nimearifiwa miongoni mwa wageni waliopo hapa, wapo Magavana wa Benki Kuu au wawakilishi wao kutoka Nchi 20 Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Karibuni sana Tanzania, hususan katika Jiji hili la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Gavana;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Tupo mahali hapa kwa ajili ya kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania, ambayo ilianzishwa rasmi siku ya Jumatatu ya tarehe 14 Juni, 1966. Mtakubaliana nami kuwa kipindi cha miaka 50 ni kipindi kirefu kwa taasisi yoyote. Ukiangalia nyuma kwenye kumbukumbu za historia ya Benki hii ilivyokuwa siku ile ya tarehe 14 Juni, 1966 na ilivyo sasa, hutasita kutambua na kukiri kuwa Benki Kuu ya Tanzania imepata mafanikio makubwa. Hivi punde, Gavana Profesa Ndulu ametoka kueleza mafanikio kadhaa ambayo Benki imepata katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Kwa haraka haraka napenda kurudia kutaja mafanikio hayo ingawa mimi nimeyaweka katika makundi makubwa mawili:

Mosi, Kukua Kitaasisi: Wakati Benki hii ikianzishwa ilikuwa na ofisi moja tu hapa Dar es Salaam. Ofisi yenyewe ilikuwa ndogo yenye vitendea kazi vichache. Nimeambiwa kutokana na udogo wa ofisi, ilibidi fedha za za benki kuhifadhiwa Jeshini na kwenye Benki binafsi. Watumishi wa Kitanzania nao walikuwa wachache na hivyo kulazimu Benki kutumia wafanyakazi kutoka nchi marafiki, ikiwemo Uingereza, Ujerumani, Sweden, India n.k. Leo miaka 50 baadaye, Benki ina ofisi yake tena jengo lake ni miongoni mwa majengo ya kisasa kabisa hapa nchini. Aidha, Benki imefungua matawi sehemu mbalimbali ikiwemo Arusha, Dodoma, Mtwara, Mwanza na Zanzibar.  

Pili, Utekelezaji wa Majukumu: Benki Kuu imekuwa na majukumu makubwa mawili tangu kuanzishwa kwake. Kati ya mwaka 1967 hadi katikati mwa miaka ya 1980, Benki Kuu ilijikita zaidi katika kutekeleza shughuli za maendeleo, ikiwemo kuelekeza nguvu kwenye ujenzi wa viwanda na kuimarisha kilimo. Hata hivyo, kutokana na changamoto zilizojitokeza na mageuzi ya kiuchumi yaliyofanyika kuanzia miaka ya 1990, jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania limekuwa ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumko wa bei na kujenga mfumo thabiti wa fedha kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. Majukumu mengine ambayo yamekuwepo tangu Benki Kuu ilipoanzishwa ni pamoja na kutoa sarafu ya nchi, kusimamia mabenki na taasisi za fedha, kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini, kuhifadhi akiba ya nchi, ikiwemo fedha za kigeni pamoja na kutoa ushauri kuhusu masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali.  Mafanikio ya utekelezaji wa majukumu yaliyopatikana ni pamoja:

(i)              Benki kuweza kutoa ushauri kwa Serikali na kusimamia mageuzi ya kiuchumi ya kuinusuru au kuikinga nchi yetu nyakati za misukosuko ya uchumi, mathalan wakati wa mdororo wa uchumi ulioikumba nchi miaka ya 1980, na hivi karibuni mdororo wa uchumi ulioikumba dunia mwaka 2008/09;

(ii)            Benki imedhibiti mfumko wa bei nchini, ambapo katika miaka ya 1990 ulifikia 30%. Hivi sasa umepungua na kuwa wastani wa tarakimu moja kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita;

(iii)          Benki imewezesha ukuaji wa sekta ya fedha, hususan kuongezeka kwa huduma za kibenki, na mchango wake kwenye pato la taifa. Idadi ya benki imeongezeka maradufu kutoka benki 3 mwaka 1990 hadi kufikia 54 hivi sasa. Aidha, uwiano kati ya mikopo inayotolewa na benki na pato la taifa umeongezeka kutoka 4% mwaka 1995 hadi kufikia 23.1% mwaka 2015.   

(iv)          Benki imeweza kurahisisha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini huku ikiendelea na jukumu lake la kuchapisha noti na kufua sarafu ya nchi.

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

          Sisi waswahili tunao msemo usemao “usione vyaelea, vimeundwa”. Mafanikio haya yote hayakujileta. Wapo watu ambao walijitoa na wanaendelea kujitoa kwa dhati kuyaleta. Baadhi yao ni ninyi watumishi wa Benki Kuu wa sasa na wastaafu mliopo hapa, mkiongozwa na Gavana wa sasa Profesa Ndulu na Gavana wa kwanza Mzee Edwin Mtei. Kwa niaba yao wote, naleta kwenu, pongezi zangu binafsi pamoja na za Serikali na Watanzania kwa ujumla, kwanza kwa kuwezesha Benki hii kutimiza nusu karne. Aidha, nawapongeza kwa mafanikio ambayo Benki imeyapata. Mmetoa mchango mkubwa sio tu kwa Benki hii bali kwa Taifa kwa ujumla. Hongereni sana. Nafahamu wapo ambao wametoa mchango kwenye Benki Kuu hii lakini wametangulia mbele za haki. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Gavana na Wafanyakazi wa Benki Kuu;

          Nimezungumza mafanikio mengi ya Benki Kuu ya Tanzania. Pamoja na mafanikio hayo, maadhimisho haya yanatoa fursa kwa Benki na taifa kwa ujumla kutafakari kwa kina changamoto zilizopo na kubuni mikakati ya kuzitatua. Mathalan, hivi sasa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu kubwa moja nalo ni kudhibiti mfumko wa bei na kujenga mfumo thabiti wa fedha kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. Benki Kuu na hata taasisi nyingi za fedha hazijihusishi moja kwa moja kwenye masuala ya ukuzaji uchumi. Lakini ukiangalia historia katika nchi zilizoendelea, kama Marekani, Uingereza, Japan, Korea Kusini utaona Benki Kuu zilitoa mchango mkubwa katika shughuli za uchumi, hususan kwenye kilimo, ujenzi wa nyumba na miundombinu.

          Hivyo basi, si vibaya na sisi tukatafakari namna ambavyo Benki Kuu inavyoweza kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi. Lakini ingefaa nieleweke kuwa ninaposema Benki Kuu kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi sina maana kuwa ni lazima mshiriki moja kwa moja. Mnaweza kubuni mikakati au kutengeneza mazingira mazuri yatakayowezesha taasisi za fedha nchini, hususan mabenki binafsi na mifuko ya hifadhi ya jamii, kuona umuhimu wa kushiriki katika shughuli hizo. Mathalan, hivi sasa Serikali imeanzisha Benki ya Uwekezaji na Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Hivyo, Benki Kuu inaweza kuweka masharti na kutengeneza mazingira wezeshi kwa mabenki binafsi nayo kutenga kiwango fulani cha mikopo wanayotoa kwa ajili ya shughuli za kilimo, mikopo ya nyumba na miundombinu. Kwa kufanya hivyo, nchi yetu itaweza kukuza uchumi kwa haraka na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini.

Mheshimiwa Gavana na Wafanyakazi wa Benki Kuu;

          Sambamba na kutafakari suala hilo la nafasi ya Benki Kuu katika shughuli za kiuchumi, yapo mambo mengine ambayo Benki Kuu haina budi kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi wake au kurekebisha. Baadhi ya mambo hayo ni haya yafuatayo:

          Mosi, kusimamia usambazaji wa huduma za fedha. Katika mafanikio ya Benki Kuu, nimetaja kuwa idadi ya mabenki na taasisi za fedha imeongezeka. Hata hivyo, idadi ya Watanzania wenye kupata huduma za kifedha ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya Watanzania. Sababu zipo nyingi lakini mojawapo kubwa ni kwamba taasisi nyingi za fedha zinafanya shughuli zake mijini wakati takriban asilimia 70 ya wananchi wanaishi vijijini. Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangiwa na mabenki mengi kufanya zaidi biashara na taasisi za Serikali, hususan kupitia ununuzi wa dhamana na amana zinazotolewa na Benki Kuu. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba fedha zinazotumiwa na mabenki hayo katika kununua dhamana na amana hizo ni zile zilizotunzwa katika benki hizo na taasisi mbalimbali za Serikali. Hii maana yake ni kwamba mabenki yamekuwa yakitumia fedha za Serikali kufanya biashara na Serikali lakini wanaonufaika ni wao. Na kwa kuwa utaratibu huu umekuwa ukiwanufaisha hawaoni umuhimu wa kusambaza huduma zao vijijini. Hivyo, wito wangu kwa Benki Kuu ni kwamba zihimizeni taasisi za fedha, ikiwemo mabenki, makampuni ya Bima na hata Mifuko ya Hifadhi, kupeleka huduma zao vijijini ambako Watanzania wengi wanaishi. Mkifanya hivyo, idadi ya wananchi wanaopata huduma za kibenki itaongezeka na pia itasaidia juhudi zetu za kuwaingiza wananchi katika mfumo rasmi na hatimaye kuwezesha Serikali kukusanya mapato kwa shughuli mbalimbali za maendeleo. Serikali kwa upande ilikwishaelekeza kufunguliwa kwa akaunti moja kwenye Benki Kuu ambayo taasisi zote za Serikali zitatunza fedha zao.  

          Pili, kushughulikia tatizo la Riba. Taasisi nyingi za fedha hapa nchini zimekuwa zikitoza riba kubwa ya mikopo. Hali hii imefanya Wajasiliamali wengi kuogopa kukopa kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kupanua biashara zao. Kwa wenye ujasiri wa kukopa wengi wao wanaishia kupata hasara ama kufilisiwa. Nafahamu zipo sababu nyingi zinazofanya viwango vya riba hapa nchini kuwa juu, mojawapo ikiwa ni kukosekana mfumo wa taarifa na kuwatambua wakopaji. Lakini kwa bahati nzuri Sheria ya Benki Kuu imeipa Benki hiyo mamlaka ya kuanzisha Mfumo wa Kumbukumbu za Mikopo na Madeni (Credit Reference System) ya wateja wa taasisi za fedha. Nitoe wito kwa Benki kufanyia kazi hili ili kusudi benki ziweze kushusha kiwango cha riba. Suala hili la riba kubwa pia limekuwa likisababishwa na tatizo nililoeleza hapo juu kuhusu mabenki kupenda kufanya biashara na taasisi ya Serikali zaidi ambako wamekuwa wakipata faida kubwa.

          Tatu, kulinda thamani ya shilingi. Nafahamu Sheria ya Benki Kuu ya sasa hatoi nafasi ya moja kwa moja kwa Benki Kuu kulinda thamani ya sarafu yetu. Thamani ya shilingi inaamuliwa na nguvu za soko. Hata hivyo, zipo njia ambazo Benki Kuu inaweza kutumia katika kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu. Moja ya njia hizo ni kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani, hapa nchini. Jambo hili limekuwa likizungumzwa mara nyingi lakini hakuna hatua mahsusi zinazofanyika. Sijui kwa nini linashindikana maana nafahamu nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea, zikiwemo za Afrika, ambazo zimefanikiwa katika kusimamia suala hili. Nitoe wito kwenu Benki Kuu mshirikiane na vyombo vingine vinavyohusika katika kuhakikisha suala hili linasimamiwa ipasavyo. Hii itasaidia sio tu kuzuia kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu bali pia kuzuia uwezekano wa nchi yetu kutumika kama sehemu ya kutakatisha fedha haramu kutoka kwa waharifu, wakiwemo magaidi na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya.

          Nne, kulinda usalama na ubora wa huduma. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya fedha, ikiwemo uwepo wa huduma za kieletroniki kama vile mashine za kutoa fedha (ATM) na huduma za kibenki kwa njia ya simu za viganjani (tigo pesa, M-pesa, airtel money n.k). Matumaini yangu ni kwamba Benki Kuu mmejipanga vizuri katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa huduma hizo lakini pia kuhakikisha Serikali inapata mapato yake stahiki. Mathalan, katika kipindi cha mwezi Machi 2016 pekee, shughuli za kibenki zilizofanyika (transactions) kwa njia ya simu za viganjani ni takriban shilingi trilioni 5.5 lakini sina hakika kama Serikali ilikusanya mapato yake yote yaliyotokana na shughuli hizo za kibenki. Nitoe wito kwa Benki Kuu mshirikiane na Mamlaka ya Mawasiliano katika kuhakikisha Serikali inakusanya mapato yake.  

          Tano, usimamizi na udhibiti wa Maduka ya kubadilishia fedha za kigeni (Bureau de Change). Ni vema Benki Kuu ikaimarisha usimamizi kuhusu uendeshaji wa maduka haya. Mnapaswa kufahamu uhalali wa fedha zinazobadilishwa na matumizi yake, ili maduka haya yasitumike kutakatisha fedha haramu au kutorosha fedha nje ya nchi na hatimaye kuharibu uchumi wetu.

          Sita, suala la mfumko wa bei. Hivi punde nimewapongeza kuhusu kushuka kwa mfumko wa bei nchini. Hata hivyo, licha ya kushuka kwa mfumko wa bei hali ya maisha ya Watanzania wengi bado ni ngumu na huenda takwimu za kushuka kwa bei tunazowatangazia hawaoni umuhimu wake. Nitoe wito kwenu kujipanga vizuri katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kwa kasi na wananchi waone manufaa ya takwimu tunazozitoa.

 

 

Mheshimiwa Gavana na Wafanyakazi wa Benki Kuu;

          Nimeeleza mafanikio na changamoto za Benki Kuu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Na huenda nimeeleza zaidi changamoto kuliko mafanikio. Nimefanya hivyo kwa makusudi kabisa kwa vile nataka msibweteke kwa kuwa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Nimefanya hivyo pia kwa kuwa nafahamu Benki Kuu chini ya uongozi mahiri wa Gavana Ndulu mnao uwezo mkubwa wa kuzitatua changamoto za kiuchumi zilizopo nchini.

          Mimi naamini Benki Kuu mkiamua kusimamia haya niliyoyaeleza na mengineyo ambayo sikuyaeleza nchi yetu itaweza kupata maendeleo ya kiuchumi tena kwa haraka. Nasema hivyo, kwa sababu nchi yetu ina kila kitu. Tuna rasilimali za kutosha. Nchi yetu ipo kwenye eneo la kimkakati ambapo Bandari yetu inahudumia nchi nyingi za ukanda wetu ambazo hazina bahari. Aidha, nchi yetu ina amani na utulivu. Hivyo, nina imani kuwa kama kila mtu atatimiza wajibu wake ipasavyo nchi yetu itapata maendeleo.

          Serikali kwa upande imejipanga kushirikiana na watumishi wa Benki Kuu pamoja na wafanyakazi wote nchini ili kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi. Mtakumbuka wakati wa Sherehe za Mei Mosi, Serikali ilifanya uamuzi wa kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa watumishi wa Serikali kutoka asilimia 11 hadi 9. Tulifanya hivyo kwa lengo la kutoa motisha kwa wafanyakazi. Kinyume na baadhi ya watu wanavyosema, Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda na kuwathamini wafanyakazi wa Serikali. Na hapa napenda kufafanua uamuzi wa Serikali wa hivi karibuni wa kusimamisha ajira mpya na promosheni zote Serikalini. Uamuzi huu umetokana na kuwepo kwa tatizo kubwa la wafanyakazi hewa Serikalini ambao idadi yake ni zaidi ya 12,000 hivi sasa. Aidha, Serikali imebaini wapo wastaafu hewa zaidi ya 2000 ambao nao wanalipwa pensheni. Hivyo, ili kukabiliana na tatizo hili, Serikali imeamua kusitisha zoezi la kuajiri watumishi wapya na kutoa promosheni ili kujipa nafasi ya kushughulikia tatizo la wafanyakazi hewa. Nina imani zoezi hili litakamilika ndani ya kipindi cha miezi miwili na baada ya hapo taratibu za ajira mpya na promosheni zitaendelea kama kawaida.  

Mheshimiwa Gavana;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

         Tupo hapa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 ya Benki Kuu. Nafahamu kwenye programu yenu mmeandaa mambo mengi ya kufanya, ikiwemo kongamano kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali. Hivyo, nisingependa kuwapunja muda wenu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha  hotuba yangu, ningependa kuzungumzia suala moja la mwisho.

Hivi karibuni, nchi yetu imekamilisha kuandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao utatekelezwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21. Mpango huu unadhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa unatarajiwa kugharimu takriban shilingi trilioni 107, zikiwemo trilioni 59 kutoka Serikalini. Je Benki Kuu mmejipangaje katika kuhakikisha Mpango huu utatekelezwa?

Naamini mtakubaliana nami kuwa, moja ya changamoto kubwa ambayo nchi nyingi za Afrika inakabiliana nayo katika kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ni ukosefu wa fedha. Kutokana na kukosa fedha za kutosha, tumebaki tukitegemea sana mikopo na misaada kutoka kwa wahisani, ambayo katika miaka ya hivi karibu imepungua sana. Nyakati nyingine imekuwa ikitolewa kwa kuchelewa ama kwa masharti magumu sana. Hivyo, nchi zetu hazina budi kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto hii. Ni kwa sababu hii, nimefurahi sana kuona kuwa kaulimbiu ya kongamano lenu itahusu “Namna ya Kupata Fedha za Maendeleo na Athari za Mikopo na Misaada (Beyond Aid and Concessional Borrowing: New Ways of Financing Development in Africa and its Implications)”.  Nina imani kuwa uwepo wa washiriki kutoka nchi za EAC na SADC, pamoja na Mtaalam Prof. Justin Lin kutoka nchi ya China, ambayo miaka kadhaa iliyopita ilikuwa inalingana na nchi nyingi za Kiafrika kimaendeleo lakini hivi sasa ni kinara miongoni mwa nchi zinazotoa misaada mingi, itasaidia kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabili changamoto hii. Na mimi nitashukuru na kufurahi sana kama nitapata ripoti ya Kongamano lenu.

 

 

 

 

 

Mheshimiwa Gavana;

Menejimeti na Wafanyakazi wa Benki Kuu;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa hotuba yangu kwa kurudia kutoa pongezi nyingi kwa Benki Kuu kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Nawapongeza pia kwa mchango wa fedha mlioutoa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la madawati katika shule zetu. Wito wangu kwenu mzidi kuongeza juhudi ili miaka 50 ijayo iwe ya mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa nchi yetu.

 

Mungu Ibariki Benki Kuu!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Asanteni Kwa Kunisikiliza”