Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Julai, 2020 amewaongoza Watanzania katika mazishi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa aliyezikwa kijijini kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.

Mazishi ya Mhe. Benjamin William Mkapa yamefanyika kwa taratibu za kidini na heshima zote za kijeshi ambapo Ibada ya Mazishi imeongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga (Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limefanya gwaride la mazishi likiambatana na kupiga mizinga 21 kwa heshima ya Rais Mstaafu na Amiri Jeshi Mkuu wa Awamu ya Tatu.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria mazishi hayo wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Viongozi wengine ni Maspika, Majaji Wakuu, Makamu wa Rais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Maspika Wastaafu, Majaji Wakuu Wastaafu, Mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi.

Pamoja na kuongoza Ibada ya mazishi, Askofu Mkuu Nyaisonga amesoma salamu za rambirambi za Baba Mtakatifu (Papa Francis) aliyewapa pole Watanzania wote na kuwataka kuwa wavumilivu na wenye matumaini na salamu za Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi na Rais Mstaafu wa Nchi hiyo Mhe. Joaquim Chissano zimesomwa na Balozi wa Msumbiji hapa nchini Mhe. Mónica Patrício Clemente.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amesema wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wenzao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na kiongozi shupavu na hodari aliyetoa mchango mkubwa kwa Taifa na katika kuuhifadhi na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kwamba Wazanzibar daima watamkumbuka na kuuenzi mchango huo.

Marais Wastaafu Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wamemuelezea Hayati Benjamin William Mkapa kuwa alikuwa kiongozi hodari, mbunifu, aliyechukia umasikini na aliyeelekeza nguvu zake kujenga uchumi wa Tanzania.

Wamempa pole Mhe. Rais Magufuli na familia ya Hayati Benjamin William Mkapa ikiongozwa na Mjane wake Mama Anna Mkapa kwa kuguswa zaidi na msiba huu mkubwa na wamewataka Watanzania wote waendelee kumuombea.

Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha maombolezo, ameishukuru kamati ya maombolezo iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na amewashukuru viongozi wote wa Dini ambao walimlea tangu alipobatizwa na hata alipofariki dunia wamemuombea na kufanyia Ibada ya maziko.

Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kujifunza kutoka kwa Hayati Benjamin William Mkapa aliyewapenda Watanzania kwa dhati na aliyewapenda wanakijiji wenzake wa Lupaso kwani wakati wa uhai wake alipoulizwa azikwe wapi atakapofariki dunia alisema anataka azikwe kijiji cha Lupaso na sio Dodoma ambako kulikuwa na mapendekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa kuzikwa makao makuu ya nchi.