Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Mei, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chato Mkoani Geita kusali Ibada ya Jumapili iliyoongozwa na Mchungaji Thomas Paschal Kangeizi.

Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru Waumini wa KKKT Usharika wa Chato kwa kumkaribisha kusali Ibada ya Jumapili pamoja nao, na pia amemshukuru Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Fredrick Shoo na Askofu wa Jimbo la Kusini C (Biharamulo) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Askofu Abednego Keshomshahara kwa kuwaruhusu Waumini kuendelea na Ibada huku wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote wa Dini hapa nchini ambao wamemtanguliza Mwenyezi Mungu na kuwaongoza Waumini kumuomba Mungu aepushe janga la ugonjwa wa Corona na pia kwa kumuombea na kumtia moyo katika kipindi hiki kigumu ambapo dunia inapita katika janga la ugonjwa huo.

Mhe. Rais Magufuli amesema hakutoa amri ya kuwafungia ndani wananchi (lockdown) wala kufunga mipaka kwa sababu ingeleta madhara makubwa katika shughuli za uzalishaji mali, utekelezaji wa miradi, ajira za watu na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo chakula hali ambayo ingesababisha madhara makubwa zaidi.

Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa anamuamini Mungu aliyehai na ndio maana aliamua kumtanguliza Mungu katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona kwa maombi ya siku 3 na sasa amewasihi viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa ujumla kutumia siku 3 za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ijayo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa hivi sasa maambukizi ya ugonjwa Corona yameanza kupungua.

Ametoa takwimu za mpaka leo tarehe 17 Mei, 2020 kuwa Hospitali ya Amana (Dar es Salaam) iliyokuwa na wagonjwa 198 imebakiwa na mgonjwa 12, Hospitali ya Mloganzila iliyokuwa na wagonjwa 30 imebakiwa na wagonjwa 6, Kituo cha Lulanzi (Kibaha) kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 wamebaki 22, Agha Khan wamebaki wagonjwa 31, Hindu Mandal 16, Regency wamebaki 17, TMJ 7, Rabinisia 14, Moshono (Arusha) 11, Longido 0, Karatu 0, Buswelu 2, Misungwi 2, Ukerewe 0, Magu 0, Mkuyuni 0, Nyahunge 0, Sengerema 0, Kwimba 0, Bugando na Sekou Toure 2, Dodoma 2 (kutoka zaidi ya 40), Kongwa 0, Kondoa 0 nakadhalika. Na kwamba wagonjwa wengi wana hali nzuri.

“Mimi namwamini Mungu na Mungu amejibu maombi yetu, tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutusikiliza na tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu wa Corona” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amesema endapo hali ya ugonjwa wa Corona itaendelea hivi Serikali inafikiria kufungua vyuo ili wanafunzi warudi vyuoni kuendelea na masomo na pia michezo itaruhusiwa kuendelea kufanyika hapa nchini.

Amebainisha kuwa kuna idadi kubwa ya watalii wanaotaka kuja hapa nchini na ambao tayari wameonyesha nia ya kukata tiketi za kuja, hivyo ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka zingine zinazohusika kutowazuia watalii na ndege zinazotaka kuleta wageni hapa nchini.

Amesisitiza kuwa viongozi na Watanzania wote wasiwe na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa Corona kiasi cha kusababisha matatizo mengine ikiwemo kutowahudumia ipasavyo wagonjwa mbalimbali ambao baadhi wanaambiwa wana Corona ilihali hawajaambukizwa ugonjwa huo, ama kuwazuia watoa huduma wakiwemo Madaktari na Wauguzi wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa Corona.

Amesema “wapo watu ambao wanaambiwa wana Corona lakini wakipimwa tena wanakutwa hawana” na amewataka viongozi waache kuwazuia watu kuzika kwa heshima marehemu wao kama ambavyo wanawazika watu waliokufa kwa magonjwa mengine yakiwemo ukimwi, kifua kikuu na surua.

“Hata mimi mtoto wangu alipata Corona lakini amepona, alikuwa anakula limau, tangawizi, anajifukiza mpaka amepona, kwa hiyo ugonjwa huu utasambaa na utakwisha, hatuwezi kufunga mipaka, sisi Tanzania tukifunga mipaka nchi zinazotuzunguka watapata shida, hata sasa tulipata tatizo la upungufu wa sukari, nimezungumza na Rais wa Uganda Mhe. Museveni na zimekuja tani 26,000 kwa meli hadi Mwanza, na tani nyingine 10,000 zimekuja kupitia bandari ya Dar es Salaam, tungefunga mipaka ingekuwaje?” amesema Mhe. Rais Magufuli

Amesisitiza kuwa Watanzania waendelee kuchapa kazi hasa kuzalisha chakula kwa wingi kwa kuwa majirani ambao wamefunga mipaka na wamewafungia watu wao (lockdown), pindi watakapofungua watahitaji chakula na watakuja Tanzania.

“Tutumie mvua hizi za mwisho zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwetu, kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili baadaye wenzetu watakapofunguliwa tuwauzie chakula, endeleeni kuchapa kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu uchunguzi uliofanyika katika Maabara ya Taifa, Mhe. Rais Magufuli amesema tume iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu imefanya kazi nzuri na matokeo ya uchunguzi wake yatatangazwa na Waziri mwenyewe.

Mchungaji wa KKKT Usharika wa Chato Thomas Paschal Kangeizi amemshukuru Mhe. Rais Magufulu kwa kuungana nao katika Ibada, kuruhusu Makanisa kufanya Ibada na amemuahidi kuwa Wataendelea kumuombea ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ulinzi wa Mwenyezi Mungu.

Katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamechangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa jipya la KKKT Chato na amechangia shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kwaya 3 zilizoimba katika Ibada hiyo.

  

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato

17 Mei, 2020