Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Mei, 2020 amemuapisha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Chato Mkoani Geita.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mhe. Nchemba kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Marehemu Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyefariki dunia tarehe 01 Mei, 2020 na pia kushirikiana na viongozi wenzake katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali.

“Nimekuteua kwa mara ya pili kwa sababu naamini unaweza kutekeleza jukumu hili vizuri, na bahati nzuri vijana wengi niliowateua hawajaniangusha, kwa hiyo nakutakia heri katika kazi zako na Mungu akutangulie” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kuwataka Watanzania kutokuwa na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelekezwa na wataalamu.

Amefafanua kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa ambao unasambazwa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi, hali ambayo haisadii kupunguza tatizo bali kuliongeza na kutengeneza sintofahamu kubwa.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Walimu ambao ni asilimia 49 ya wafanyakazi wote hapa nchini pamoja na wafanyakazi wengine kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na ugonjwa wa Corona, Serikali imejipanga kuhakikisha wanalipwa mishahara yao kama kawaida na ametoa wito kwa taasisi za kifedha za kimataifa zilizoonesha nia ya kusaidia uchumi wa nchi zinazoendelea, kusamehe mikopo badala ya kutaka kuzikopesha mikopo mipya.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe (aliyeteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni) kwa kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa vifaa vya uchunguzi wa ugonjwa wa Corona na ameagiza maabara kuu ya Taifa inayofanya uchunguzi wa ugonjwa huo ichunguzwe vizuri ili kujiridhisha juu ya usahihi wa majibu ya sampuli zinazopelekwa kuchunguzwa.

Amewataka Watanzania wote hasa wanasiasa pamoja vyombo vya habari kuacha kueneza taarifa zinazowajaza watu hofu ama kutumia ugonjwa huu kwa manufaa ya kisiasa na badala yake waungane kutoa elimu sahihi na kuhimizana kuchukua tahadhari za kutoambukizwa.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Madaktari, Wauguzi, Wafanyakazi wa Afya na wadau mbalimbai walio mstari wa mbele katika kuwahudumia watu wanaopatwa na maambukizi ya ugonjwa wa Corona na amewahakikishia kuwa Serikali inachukua hatua madhubuti za kukabiliana nao ikiwemo kupata dawa kutoka mahali popote itakapopatikana.

Ameelezea kushangazwa kwake na viongozi ambao wanazuia watu wanaofariki dunia kusafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao, na Viongozi wa Dini walioonesha kutetereka kiimani, hivyo ametoa wito kwa viongozi wote kusimama imara, kuonesha uongozi wa kweli na kuwapa matumaini wananchi badala ya kuwajaza hofu.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeiry bin Ally na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga pamoja na viongozi wengine wa Dini waliosimama katika imani na kuwataka Waumini waendelee kusali, kufunga na kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe ugonjwa huu.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato

03 Mei, 2020