Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi wote hapa nchini kwa kazi nzuri wanazozifanya na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi na mazingira yao ya kazi.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 20 Februari, 2020 wakati akihutubia mkutano wa Madaktari uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Madaktari na watoa huduma za afya zaidi ya 1,500 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mhe. Rais Magufuli amesema sambamba na juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuimarisha huduma za afya, Madaktari wameonesha ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo utoaji huduma za matibabu ya kibingwa.

Katika mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) iliyotolewa na Rais wa MAT Dkt. Elisha Osati na pia amesikiliza maoni na kero mbalimbali za Madaktari ambapo ameahidi kuwa Serikali itatoa jengo kwa ajili shughuli za MAT na pia ameahidi kuwa Serikali itaanza kuwaajiri Madaktari wapya 1,000 waliohitimu masomo yao.

Kuhusu changamoto zingine zilizotolewa na MAT na Madaktari hao, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Madaktari na watoa huduma za afya hao kuwa changamoto hizo amezisikia na ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuanza kuzishughulikia.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa katika miaka 4 iliyopita Serikali ya Awamu ya Tano imefanya juhudi kubwa kuimarisha huduma za afya ambapo Zahanati zimeongezeka kutoka 6,044 hadi 6,467 (zahanati 368 zimejengwa na Serikali), Vituo vya Afya vimeongezeka kutoka 718 hadi 1,169 (Vituo vya Afya 352 vimejengwa na Serikali), Vituo vya Afya vinavyotoa huduma za upasuaji vimeongezeka kutoka 115 hadi kufikia 467 na Hospitali zenye hadhi ya Wilaya zimeongezeka kutoka 77 hadi kufikia 147 (Hospitali mpya 70 zimejengwa na Serikali). Miundombinu hii imegharimu shilingi Bilioni 293.705 na imewekewa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Bilioni 68.706.

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hiki pia Hospitali za Rufaa za Mikoa 23 zimekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 89.5, Hospitali za Mloganzila na Benjamin Mkapa zimekamilishwa na kuwekewa vifaa tiba kwa gharama ya shilingi Bilioni 102.9, Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Geita, Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe zimejengwa kwa shilingi Bilioni 58 na ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Musoma, Mtwara, Mwananyamala na Sekou Toure Mwanza unaendelea. Juhudi hizi zimesaidia kuongeza idadi ya vituo vya kutolea tiba kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi kufikia 8,446 mwaka 2019.

Pia, Mhe. Rais Magufuli ametaja maeneo mengine ya mafanikio kuwa ni kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi Shilingi Bilioni 270, kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kutoka wastani wa 200 kwa mwaka hadi 60 kutokana na kuimarika kwa huduma za matibabu ya kibingwa, kuajiri watumishi wapya wa afya 13,479 (kati ya watumishi wote 62,498) wakiwemo Madaktari Bingwa 22 na Madaktari 1,156, imejenga nyumba 832 za watumishi wa afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa.

Kutokana na juhudi hizo, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Madaktari kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na amewataka kutengeneza mikakati ya kuiwezesha Tanzania kuzalisha dawa na vifaa tiba, badala ya kuendelea kuagiza kutoka nje ya nchi kwa kiasi kikubwa.

Amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwaweka mahabusu Madaktari lakini amewataka Madaktari kujiepusha na vitendo viovu ili wasichuliwe hatua.

Mapema Rais wa MAT Dkt. Elisha Osati na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Boniface wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika sekta ya afya hususani kuimarisha matibabu ya kibingwa katika hospitali na taasisi zake, na wamemhakikishia kuwa Madaktari wataendelea kumuunga mkono kwa kuchapa kazi zaidi.

Katika Mkutano huo, Mhe. Rais Magufuli amekabidhi tuzo 2 zilizoandaliwa na MAT kwa Dkt. Jesse Mbwambo (Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akili) na Wilson Koweli Chotamganga (Afisa Tabibu) kwa kutambua mchango wao mkubwa katika matibabu na pia amepokea tuzo ya MAT kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

20 Februari, 2020