Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 17 Februari, 2020 amezindua kipindi cha 2 cha awamu ya 3 ya mpango wa kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Sherehe za uzinduzi huo zimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Marais Wastaafu Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini na Viongozi wa vyama vya Siasa.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Marais Wastaafu wa kuasisi na kuiendeleza TASAF ambayo imetoa mchango mkubwa katika kupunguza umasikini hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa juhudi za kukabiliana na umasikini hapa nchini ikiwemo mpango wa TASAF zimepata mafanikio makubwa ambapo takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu zimeonesha kuwa kati ya mwaka 1990/91 na 2017/18 umasikini wa mahitaji ya msingi (Basic Needs) umepungua kutoka asilimia 39.0 hadi 26.4, umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 19.7 hadi 9.5, na kwamba takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kasi kubwa ya kupambana na umasikini kati ya nchi za Afrika zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa TASAF ulioanza mwaka 2000 na ambao kwa sasa upo katika awamu ya 3 na utagharimu shilingi Trilioni 4.109 zikiwemo shilingi Trilioni 2.032 za kipindi cha pili cha awamu ya tatu amepangwa kunufaisha Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na Wilaya 11 za Zanzibar, na kwamba baada ya kufanya maboresho sasa ruzuku imepunguzwa kutoka asilimia 67 hadi 38 na itaelekezwa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa wenye kiwango kikubwa cha ulemavu.

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa asilimia 60 (sawa na Shilingi Trilioni 1.22) ya fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takribani 30,000 iliyopo kwenye vijiji na mitaa 16,596 ya Tanzania Bara na Shehia 388 za Zanzibar na miradi hiyo itahusisha afya, elimu, maji, barabara na mazingira. Miradi hii inatarajiwa kuzalisha ajira Milioni 1.2 kwa watu wenye nguvu walio katika kaya masikini.

Amesisitiza kuwa licha ya kuwa sehemu ya fedha hizo ni ufadhili, sehemu kubwa ambayo ni kiasi cha shilingi Trilioni 1.035 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na hivyo amewaagiza viongozi wote wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha wanasimamia utekelezaji mzuri wa mpango huo na kwamba kufanikiwa ama kutofanikiwa kwake itakuwa ni kipimo cha kama wanastahili kuendelea na nyadhifa zao ama laa.

“Mathalani katika zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanywa kuanzia Novemba 2015 hadi Juni 2017 tuliweza kubaini kaya masikini hewa 73,561. Hii ni aibu sana kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladslaus Mwamanga amesema TASAF imepata mafanikio makubwa katika awamu zake zote ambapo katika awamu ya 1 kaya 1,704 zilinufaika na ufadhili wa shilingi Bilioni 72, Awamu ya 2 kaya 12,347 zilinufaika na ufadhili wa shilingi Bilioni 430 na kipindi cha 1 cha awamu ya 3 Mamlaka za Serikali za Mitaa 159 za Tanzania Bara na Zanzibar yote zimenufaika na ufadhili ya shilingi Trilioni 1.46.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema pamoja na takwimu kuonesha Tanzania inafanya vizuri katika kupunguza umasikini, viashiria vya huduma za kijamii navyo vinaonesha Tanzania imepiga hatua kubwa ambapo uandikishaji wanafunzi Shule za Msingi umepanda kutoka asilimia 78 (2012) hadi kufikia asilimia 83 (2018) na huenda imefika zaidi ya asilimia 90 hivi sasa, upatikanaji wa maji kutoka vyanzo bora umepanda hadi kufikia 83, nyumba za Watanzania zimeezekwa mabati kwa asilimia 84.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

17 Dar es Salaam.