Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Februari, 2020 amekutana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini Mhe. Manfred Fanti na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Dkt. Stergomena Tax amesema alikuja kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya SADC ikiwemo uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara ambapo wamekubaliana kuendelea kuhamasisha nchi wanachama kuendeleza viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Ameelezea baadhi ya maeneo yaliyopo katika mkakati wa kukuza uchumi wa SADC kuwa ni kuendeleza miundombinu hasa ya usafiri na nishati ambayo bado ni changamoto kwa nchi za SADC, lakini ameipongeza Tanzania kwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na kuongeza uzalishaji wa umeme.

Kwa upande wake Balozi wa EU hapa nchini Mhe. Manfred Fanti amesema mazungumzo yake na Mhe. Rais Magufuli yamekuwa na manufaa makubwa ambapo wamejadili maendeleo mazuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na EU, na kwamba katika siku za karibuni wamekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa EU kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania ambapo shilingi Bilioni 132 zilizokuwa zimezuiwa zimeruhusiwa na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka 7 utakaoanza mwaka huu.

Mhe. Manfred Fanti amesema kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania ana matumaini makubwa kuwa EU itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Tanzania ili kufanya vizuri zaidi.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Balozi Fanti kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na EU na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kumkabidhi barua aliyomwandikia Rais wa China Mhe. Xi Jinping akimpa pole kwa janga la homa ya virus vya Corona lililolikumba Jiji la Wuhan nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.

“China ni ndugu zetu ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Mhe. Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Balozi Wang Ke amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu. Ametumia nafasi hiyo kueleza hali ilivyo nchini China ambapo amesema Serikali ya China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na homa hiyo, imefanikiwa kuzuia isienee katika nchi zingine kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Aidha, amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa homa ya Corona, pia Watanzania 400 waliopo katika Jiji la Wuhan ambao wengi wao ni wanafunzi hawajaambukizwa homa hiyo na jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama zinafanyika.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

05 Februari, 2020