Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Januari, 2020 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 3 walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Ujerumani, Qatar na Algeria hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha hati hizo ni Mhe. Regine Hess – Balozi wa Jamhuri ya Ujerumani hapa nchini, Mhe. Hussein Bin Ahmed Mohamed Ibrahim Al-Homaid – Balozi wa Taifa la Qatar hapa nchini na Mhe. Ahmed Djellal – Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria hapa nchini.

Akizungumza na Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewakaribisha hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayo dhamira ya dhati ya kuukuza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kutoka nchini mwao kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali hasa kilimo, mafuta, gesi, viwanda na madini kwa kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha katika sekta hizo ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika uwekezaji.

Amewaomba Mabalozi hao kufikisha shukrani zake kwa viongozi wa nchi zao na kuwakaribisha kutembelea Tanzania kwa ziara rasmi ama kutembelea vivutio vingi vya utalii vilivyopo.

Kwa upande wao, Mabalozi hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali kuwapokea na katika kipindi cha uwakilishi wao wameahidi kufanya juhudi za kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano hasa katika masuala ya kiuchumi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayapa kipaumbele.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

14 Januari, 2020