Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Januari, 2020 amewaapisha Mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.

Walioapishwa ni Mej. Jen (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi anayekuwa Balozi wa Tanzania Pretoria - Afrika Kusini, Dkt. Modestus Francis Kipilimba anayekuwa Balozi wa Tanzania Windhoek – Namibia, Prof. Emmanuel David Mwaluko Mbennah anayekuwa Balozi wa Tanzania Harare – Zimbabwe na Dkt. Benson Alfred Bana anayekuwa Balozi wa Tanzania Abuja – Nigeria.

Baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya wiki 2 kuanzia sasa na amewasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia maslahi ya Taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizopo katika nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewataka Mabalozi hao kufuatilia maeneo yote ambayo Mhe. Rais Magufuli alikubaliana na Waheshimiwa Marais wenzake alipotembelea nchi hizo hivi karibuni, na pia kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.

Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Kabla ya kuwaapisha Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

14 Januari, 2020