Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 18 Desemba, 2019 amefungua Mahakama ya Wilaya ya Chato, ameweka mawe ya msingi ya jengo Jeshi la Zimamoto la Wilaya ya Chato na Msikiti, na amefungua madarasa na mradi wa maji katika Shule ya Msingi Chato ambayo alisoma elimu yake ya msingi.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato lililogharimu shilingi Milioni 913 ni moja ya Majengo 26 ya Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi wa Mkoa, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo zilizojengwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Miaka 5 wa Mahakama ya Tanzania ulioanza 2016/17 hadi 2020/21 ambao umelenga kuboresha miundombinu ya mahakama kwa kukarabati, kumalizia na kujenga majengo mapya.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa shilingi Bilioni 40.8 zilizofanikisha utekelezaji wa miradi 55 ya ujenzi inayojumuisha miradi 12 iliyokuwa imekwama, 29 iliyojengwa na kukamilika na 14 inayoendelea kujengwa, na ameeleza kuwa huo ni uthibitisho wa dhamira yake ya kweli ya kuhakikisha Mahakama inapata majengo ya kisasa ili kutimiza jukumu lake la kikatiba la utoaji wa haki.

Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amebainisha kuwa kwa sasa Mahakama ya Tanzania inajiandaa kuanza ujenzi wa Makao yake Makuu Jijini Dodoma, kujenga majengo jumuishi (majengo yatakayojumuisha huduma za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na Ofisi za Wadau) na kujenga majengo mengine 33 ya Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo, miradi yote ikiwa inagharamiwa na Serikali ya Tanzania.

Jengo la Zimamoto Wilaya ya Chato ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 60 kwa gharama ya shilingi Milioni 713.6 linatarajiwa kukamilika Februari 2020 kwa gharama ya jumla ya shilingi Milioni 943, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na endapo lingejengwa kwa utaratibu wa zabuni za wakandarasi ambapo ungegharimu shilingi Bilioni 1.6.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa shilingi Bilioni 108.743 ambazo zimesaidia kulipa madeni makubwa ya wazabuni, watumishi na mishahara hali iliyoamsha morali na ari ya kazi kwa wafanyakazi.

Amesema katika kipindi cha miaka minne jeshi hilo limepata mafanikio makubwa ikiwemo kujenga jengo la Makao Makuu Dodoma kwa shilingi Bilioni 2.656, kupata magari ya zimamoto 18, magari ya uokoaji 3, gari 1 la wagonjwa na boti 1, kuwapandisha vyeo Maafisa na Askari 683, kukusanya maduhuli ya Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 73.264 na kushiriki kikamilifu katika matukio ya moto 5,367 na matukio 2,060 ya uokoaji.

Msikiti (Masjid Al Huda) ambao ujenzi wake utakamilika Desemba 2020 kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1.6 ukiwa na uwezo wa kuchukua waumini 3,000 watakaoingia ndani na 6,000 wakaokuwa nje, unajengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Al Hikma baada ya kuombwa na Mhe. Rais Magufuli kufanya hivyo kwa ajili ya Waislamu wa Chato.

Rais wa Taasisi ya Al Hikma Sheikh Shareef Abdulqadir Al – Ahdal amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa upendo wake kwa Watanzania wa Madhehebu yote ya Dini na ameahidi kuwa Tasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali ya kutoa huduma kwa jamii.

Jengo la madarasa 3 na ofisi 2 za walimu limejengwa katika Shule ya Msingi Chato ikiwa ni mchango wa Mhe. Rais Magufuli kwa shule hiyo ambayo alisoma kati ya mwaka 1967 na 1974 na mradi wa kisima cha maji katika shule hiyo ni kati ya visima 8 vilivyochimbwa Wilayani Chato na Taasisi ya Kiislamu chini ya ufadhili wa Rais wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa gharama ya shilingi Milioni 340.3.

Akizungumza na wananchi wa Chato waliojitokeza katika ziara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa hatua kubwa za maendeleo ya Mahakama na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha inaimarisha Mahakama ili itende vyema jukumu lake la kutoa haki kwa Watanzania wote.

Amesema katika miaka minne ya uongozi wake Serikali imeongeza Majaji wa Mahakama ya Rufani 11, Majaji wa Mahakama Kuu 39 na Mahakimu 396 na hivyo kuongeza idadi ya watumishi hao kutoka 700 hadi kufikia 938.

Hata hivyo ametoa wito kwa vyombo vyote vinavyohusika kuendelea kutekeleza mpango wa kupunguza mrundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani na amempongeza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Mhe. Biswalo Mganga na vyombo washirika kwa kuwaachia mahabusu 751 katika Mikoa 3 baada ya kubaini kuwa walikuwa na makosa madogo madogo ama kubambikizwa kesi.

Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mafanikio makubwa lililoanza kuyapata ikiwemo kujenga majengo mazuri kwa gharama nafuu, kuanza kuunda magari ya zimamoto hapahapa nchini kwa kushirikiana na Shirika la Nyumbu, kushiriki katika matukio ya uzimajimoto na uokoaji na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuliimarisha jeshi hilo.

Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Taasisi ya Kiislamu (Islamic Foundation) na Rais wa UAE Mtukufu Khalifa bin Zayed Al Nahyan kwa kufadhili mradi wa maji wa visima 8 kikiwemo cha shule ya Msingi Chato na Taasisi Al Hikma kwa kukubali ombi lake la kujenga Msikiti wa Wilaya ya Chato, na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya Dini katika kutoa huduma kwa jamii.

 

Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema pamoja na kuwepo wadau mbalimbali wa maendeleo wanaosaidia juhudi za kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hizo ambapo hivi sasa inatekeleza miradi 350 ya maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3.5 na tayari upatikanaji wa maji kwa Watanzania umepanda kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71.

 

Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kutunza miundombinu ya maji inayojengwa na Serikali na wadau mbalimbali kote nchini badala ya kuiba vipuri na mitambo kama walivyofanya miaka ya nyuma, na pia amewataka Watanzania wanaoathiriwa na maji ya mvua zinazonyesha baada ya kujenga katika mikondo ya maji kutoilaumu Serikali kwa kuwa madhara yanayowapata yanasababishwa na wao wenyewe kuziba njia za maji.

 

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amerejea kauli yake kuwa hatarajii kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amesisitiza kuwa mafanikio yanayopatikana sasa yanatokana na baraka za Mwenyezi Mungu ambaye atabariki kupatikana kwa kiongozi mwingine atakayefanya vizuri.

 

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato

18 Desemba, 2019