Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Desemba, 2019 ameungana na Watanzania wote katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kwa mara ya kwanza katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Sherehe za maadhimisho hayo zimehudhuriwa na maelfu ya wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu.

Viongozi wengine ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali.

Sherehe za maadhimisho hayo zimepambwa kwa gwaride rasmi lililoandaliwa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama, maonesho ya ndege vita, helkopta, zimamoto na burudani za kwaya, ngoma za asili, dansi na Bongofleva.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote kwa kuadhimisha miaka 58 ya tangu Tanzania Bara ipate Uhuru na amewashukuru waasisi wa Taifa wakiongozwa na Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa juhudi kubwa walizozifanya kupigania uhuru kupitia chama cha TANU na hatimaye uhuru kupatikana tarehe 09 Desemba, 1961.

Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wana kila sababu ya kujipongeza kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi chote cha miaka 58 na amewapongeza Marais wa awamu zote nne zilizotangulia kwa kuiongoza Tanzania kwa mafanikio.

Ameyataja baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania imeyapata baada ya Uhuru kuwa ni kuongezeka kwa barabara za lami kutoka kilometa 1,360 hadi kilometa 12,679.55 ilihali nyingine zaidi ya 2,000 zikiwa katika ujenzi, kuongezeka kwa vituo vya tiba (Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati) kutoka 1,098 hadi 7,293, kuongezeka kwa Shule za Msingi kutoka 3,100 hadi 17,379 na kuongezeka kwa Shule za Sekondari kutoka 41 hadi kufikia 4,817.

Maendeleo mengine ni kuongezeka kwa Vyuo Vikuu kutoka 1 hadi kufikia 48, Madaktari waliosajiliwa kutoka 403 (Watanganyika wakiwa 12) hadi kufikia 9,400, Wahandisi kutoka 2 hadi 19,164, Wakandarasi kutoka 2 hadi kufikia 9,350 na pia wastani wa umri wa mtu kuishi kuongezeka kutoka miaka 37 hadi kufikia miaka 61.

Mhe. Rais Magufuli amesema katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza imedhamiria kuimarisha zaidi uchumi kwa kujenga viwanda ambavyo kwa miaka minne vimejengwa zaidi ya 4,000, kuimarisha miundombinu kwa kufufua reli na kujenga reli ya kisasa (standard gauge), kujenga barabara, kupanua na kuboresha bandari, kujenga na kukarabati meli 5, kununua ndege 11, kujenga viwanja vya ndege 11, kujenga Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme, kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania, kuongeza Hifadhi za Taifa, kuinua uvuvi na kuimarisha usimamizi wa maliasili hasa madini.

Amewashukuru Watanzania wote na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi hizi na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakuwa, huduma za kijamii zinaboreshwa na Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa na kuwepo kwa idadi kubwa ya Wafungwa 17,547 na Mahabusu 18,256 waliopo Magerezani na hivyo ameamua kutoa msamaha kwa idadi kubwa ya wafungwa 5,533 ambao wanapaswa kuachiwa huru kuanzia kesho tarehe 10 Desemba, 2019.

Ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mahakama kwa kuwaachia huru Mahabusu 601 waliokuwa wakikabiliwa na kesi za uhujumu uchumi baada ya kutekeleza masharti ya msamaha alioutoa na ametaka wasirudie kufanya makosa.

Kabla ya kumaliza hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amemkaribisha Rais wa Zanzibar, Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu na viongozi wa vyama vya siasa kuwasalimu Watanzania ambapo wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano, kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza, kuchapa kazi na wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri na mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana kwa kipindi kifupi cha miaka minne ya uongozi wake.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Mwanza

09 Desemba, 2019