Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli tarehe 22 Novemba 2019 ameweka mawe ya msingi katika miradi minne ya ujenzi wa majengo ya Serikali Mkoani Dodoma.

Majengo yaliyowekwa mawe ya msingi ni Hopsitali ya Uhuru inayojengwa katika eneo la Maduka Wilayani Chamwino, nyumba 118 za makazi ya Askari Polisi, Soko Kuu na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma vinavyojengwa katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.

Ujenzi wa jengo la Hospitali ya Uhuru utakamilika Aprili 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.9 ambapo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kwa kukabidhi kazi ya ujenzi wa hospitali hiyo kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) baada ya kutoridhishwa na kasi ndogo ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Ujenzi wa nyumba 88 zilizopo Dodoma ambazo ni kati ya nyumba 118 za makazi ya Askari Polisi utakamilika Desemba 31, 2019 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2 na Milioni 728, ambapo Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Askari Polisi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kuwa anatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na jeshi hilo pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kulinda amani, usalama wa raia na mali zao.

Akizungumza na Askari na wananchi waliojitokeza katika eneo la Nzuguni zinapojengwa nyumba hizo, Mhe. Rais Magufuli amesema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ameamua jengo la Wizara ya Maji na Umwagiliaji lililopangwa kutumiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya makao makuu ya hilo.

Jengo hilo la ghorofa 4 lina vyumba 157, ukarabati wake umefikia asilimia 95 na Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro kuanza kulitumia wakati ukarabati ukikamilishwa.

Ujenzi wa Soko Kuu utakamilika Februari 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 14.4 ambapo Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuwapongeza viongozi wa Jiji la Dodoma amependekeza soko hilo liitwe Soko Kuu la Ndugai, ikiwa ni kutambua mchango wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai katika kuongoza Bunge la 11 linaloidhinisha bajeti ya utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano likiwemo soko hilo.

Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma utakamilika Februari 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 24. Fedha hizo pamoja na za ujenzi wa Soko Kuu zimetolewa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Kituo hiki kitakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi 250, magari madogo 600, bajaji 150, bodaboda 250 na kutumiwa na watu 6,000 kwa mpigo, na pia kitaunganishwa kwa miundombinu ya reli inayoungana na reli ya kati, na reli ya kwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato ambao unaanza kujengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 500.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la kituo hicho, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru wananchi wa Dodoma kwa kuwapokea wafanyakazi na viongozi mbalimbali akiwemo yeye mwenyewe, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ambao tayari wameshahamia Dodoma na pia amewapongeza kwa maendeleo ya kasi kubwa yanayofanyika Mkoani humo.

“Nafarijika kuona Serikali yote sasa imehamia Dodoma, huu ni uthibitisho kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiahidi kinatekeleza, niliahidi kuwa Serikali itahakikisha mandhari ya Dodoma yanaboreshwa na sasa mnaona nyinyi wenyewe, kila mahali panajengwa majengo mazuri, hata siku nilipotangaza Dodoma kuwa Jiji kuna watu walibeza lakini sasa wote ni mashahidi, Dodoma inapendeza” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kujengwa kwa Soko Kuu na Kituo Kikuu cha Mabasi, Serikali inajenga miradi mingine mikubwa ikiwemo barabara za mzungumzo za njia 4 zenye urefu wa kilometa 110 kwa shilingi Bilioni 415, eneo la kuegeshea malori, dampo la taka, eneo la kupumzikia, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato na Hospitali ya Uhuru.

Ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma kuchapa kazi, kuchangamkia fursa za maendeleo zinazokuja kutokana na kuhamia kwa Makao Makuu ya Serikali ikiwemo kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya kuuza.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi dhidi ya matapeli wanaowadanganya ili waanzishe migogoro ya ardhi dhidi ya Serikali na ameonya kuwa watakaostahili kulipwa kwa mujibu wa sheria watalipwa na wasiostahili hawatalipwa.

Baada ya kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli amekabidhi jengo la DUWASA kwa Jeshi la Polisi Nchini kwa ajili ya Makao Makuu ya jeshi hilo na amekabidhi iliyokuwa Ofisi ya TAMISEMI iliyopo katikati ya Jiji la Dodoma kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kwa ajili ya kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Ofisi za DUWASA na TAMISEMI zimehamishiwa katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba.

Kesho tarehe 23 Novemba, 2019 Mhe. Rais Magufuli atawaapisha Mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni, kuanzia saa 3:00 asubuhi katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chamwino

22 Novemba, 2019