Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 07 Oktoba, 2019 ameendelea na ziara yake Mkoani Rukwa ambapo amezindua mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Mji wa Sumbawanga na Msikiti wa Jumuiya ya Istaqaama Tanzania uliopo Mjini Sumbawanga.

Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Manispaa ya Sumbawanga umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (KFW) na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya shilingi Bilioni 35 na umehusisha kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita Milioni 7.5 kwa siku zilizokuwa zikizalishwa kwa kutumia miundombinu ya zamani hadi kufikia lita Milioni 20 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya wakazi 70,932 wa Mji huo wanaohitaji lita Milioni 13 kwa siku.

Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maji ambapo kwa sasa zaidi ya miradi 547 ikiwemo 468 ya maji vijijini na 79 ya maji mijini yenye thamani ya shilingi Trilioni 3.98 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Msikiti mpya wa Istiqaama Bomani uliopo Mjini Sumbawanga una uwezo wa kuchukua waumini 650 kwa mara moja, na umejengwa pamoja na kuchimba kisima cha maji kinachotoa huduma kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Seif Ally Seif amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutengua agizo la kusitisha ujenzi wa Msikiti huo lililotolewa na Manispaa ya Sumbawanga na hivyo kuruhusu Jumuiya hiyo iendelee na ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 100.

Baada ya kuzindua miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga katika uwanja wa Nelson Mandela ambapo ameishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa kufadhili ujenzi wa mradi wa maji wa Mji huo na ameagiza Wizara ya Maji kutafuta fedha za kutekeleza mradi mwingine wa usambazaji maji kwa wananchi.

Ameipongeza Jumuiya ya Istiqaama kwa kujenga Msikiti mzuri katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo pamoja na kuchangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Msikiti, amewataka Waislamu kuutumia Msikiti huo kudumisha amani, upendo, umoja na kuhimiza maendeleo ya wananchi.

Kufuatia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kueleza kuwa kuna Halmashauri za Wilaya 30 ambazo ofisi zake zipo katika Makao Makuu ya Mikoa, Mhe. Rais Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa Halmashauri hizo kuhamia katika maeneo ya halmashauri zao vinginevyo zitafutwa.

Kuhusu mgogoro kati ya Manispaa ya Sumbawanga na wafanyabiashara wa soko la Mandela waliokuwa wanadai kuzuiwa kuendeleza ujenzi wa vibanda vya biashara kwa madai ya Manispaa ya Sumbawanga kutafuta fedha za kujengea soko la kisasa, Mhe. Rais Magufuli ameagiza wafanyabiashara hao waruhusiwe mara moja kuendelea na ujenzi huo na amemuagiza Waziri wa TAMISEMI kutoa shilingi Milioni 300 zitakazosaidia kukamilisha ujenzi wa soko hilo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Rukwa kwa uzalishaji mkubwa wa mazao na ameahidi kuwa kwa kutambua juhudi zao katika maendeleo Serikali itahakikisha uwanja wa ndege wa Sumbawanga unajengwa, barabara za kuunganisha Mkoa huo na Mikoa mingine pamoja na nchi zinajengwa na ameutaka uongozi wa Mkoa huo kushughulikia kero za wananchi.

Ameelezea kuchukizwa na takwimu za idadi kubwa ya wanafunzi wa shule wanaopata ujauzito ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2018 wanafunzi 229 walipata ujauzito na hivyo amewataka wazazi na viongozi wa Dini kusimamia vizuri utoaji wa malezi kwa watoto wao, na viongozi wa Mkoa wa Rukwa kuchukua hatua za kukomesha tatizo hilo.

Kesho tarehe 08 Oktoba, 2019, Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake ambapo atazindua barabara ya Sumbawanga – Kanazi, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, atazindua Kituo cha Afya cha Namanyere na atazindua uandikishaji orodha ya wapiga kura wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 2019.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Sumbawanga

07 Oktoba, 2019