Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa ameipongeza Tanzania kwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na kubainisha kuwa hiyo ni fursa muhimu ya kuhakikisha Tanzania na Afrika Kusini zinakuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mhe. Rais Ramaphosa amesema hayo leo tarehe 15 Agosti, 2019 katika Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kuhimiza kukuza uhusiano wa kiuchumi, Mhe. Ramaphosa amesema Tanzania na Afrika Kusini ambazo zina uhusiano wa kirafiki, kihistoria na kidugu zinayo changamoto ya kuhakikisha zinaliwezesha na kulitumia vizuri kundi kubwa la vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa, kwa kuhakikisha sekta binafsi inakuzwa na hivyo kuiwezesha kuajiri vijana wengi.

Ametolea mfano wa hatua zilizochukuliwa na uongozi wake za kuanzisha mpango wa kutoa vivutio kwa kampuni binafsi zinazotoa fursa kwa vijana kufanya kazi ikiwemo kuzipunguzia kodi na kubainisha kuwa mpango huo umesaidia kuwapa fursa vijana takribani 100,000 katika kipindi kifupi, ambapo wanapata fursa ya kujifunza ujuzi mbalimbali na kujenga uwezo wa kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Mhe. Rais Ramaphosa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada mbalimbali za kukuza uchumi wa Tanzania anazozifanya na amesema licha ya kumuunga mkono katika kipindi cha Uenyekiti wake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) atakachokianza tarehe 17 Agosti, 2019 anaamini jitihada hizo pia ataziweka katika SADC.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Ramaphosa kwa dhamira yake ya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini hususani katika uchumi na amempongeza kwa mpango wake wa kusaidia vijana ujulikanao kwa jina la YES (Youth Employment Service) ambao ameahidi kuwa Serikali itaufanyia kazi ili kuona namna ya kuutekeleza hapa Tanzania.

 

Kabla ya Dhifa ya Kitaifa, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Ramaphosa wameshiriki mkutano wa wafanyabiashara wa Afrika Kusini na Tanzania uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kupuuza kauli zinazodai Tanzania inawachukia wawekezaji na badala yake amewakaribisha kuja kuwekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji vikiwemo viwanda ili Tanzania iondokane na uagizaji mkubwa wa bidhaa za viwandani kutoka nchi za nje.

Amewataka wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini kujielekeza katika mijadala ya masuala muhimu yatakayosaidia kuinua biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo, kupata wabia makini wa biashara, kuainisha maeneo ya biashara na uwekezaji na kujiandaa kwa utekelezaji.

Nae Mhe. Rais Ramaphosa ameishukuru Tanzania kwa mchango mkubwa ilioutoa kwa Afrika Kusini wakati wa harakati za ukombozi na kubainisha kuwa baada ya ukombozi kupatikana nchi hizo zinapaswa kujikita katika kuimarisha uchumi ili kuinua maisha ya wananchi wake ambao ni ndugu.

Mhe. Rais Ramaphosa amezungumzia changamoto mbalimbali zinazokwamisha ufanyaji wa biashara na uwekezaji baina ya nchi za SADC zikiwemo Tanzania na Afrika Kusini na ametoa wito kwa nchi hizo kufanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kuongeza imani kwa wafanyabiashara kwa kuondoa vikwazo, urasimu na taratibu ambazo zinawakatisha tamaa wafanyabiashara na wawekezaji.

Amesema Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na ametoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana kutatua changamoto ili kwa pamoja zipige hatua za kimaendeleo badala ya kuacha nchi zingine zikiwa nyuma.

Mhe. Ramaphosa amesisitiza kuwa kwa hivi sasa Afrika ndio Bara lenye uchumi unaokua vizuri na linazo fursa nyingi za uchumi ikilinganishwa na Mabara mengine, hivyo ni wakati wake sasa kuchangamka na kujiimarisha.

Ijumaa (Tarehe 16 Agosti, 2019), Mhe. Rais Ramaphosa ataendelea na ziara yake hapa nchini kwa kutembelea kambi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini iliyopo Mazimbu Mkoani Morogoro.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

15 Agosti, 2019