Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri ya kuchunguza sampuli mbalimbali, kusimamia sheria za usimamizi wa kemikali na kudhibiti vinasaba vya binadamu.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Agosti, 2019 alipotembelea Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo Kivukoni Jijini Dar es Salaam ambapo ameona jinsi mitambo ya uchunguzi vya kisasa inavyofanya kazi ikiwemo uchunguzi wa vinasaba vya miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya moto iliyotokea Mjini Morogoro tarehe 10 Agosti, 2019 baada ya lori lililobeba mafuta kupinduka na kisha kulipuka moto.

Akiwa katika maabara hiyo, Mhe. Rais Magufuli amejionea mitambo mipya ya uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, sumu, dawa za kulevya, kemikali na dawa inavyofanya kazi kwa haraka ambapo uchunguzi wa sampuli moja huchukua muda wa dakika 45 na unafanywa na vijana wa Tanzania.

Akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi kubwa ya utambuzi wa vinasaba waliyoifanya kwa miili 10 ya ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere, miili 14 ya ajali ya moto iliyotokea Tarime Mkoani Mara na miili 50 kati ya 69 ya watu walioungua moto katika ajali ya lori la mafuta Mjini Morogoro.

Pamoja na kufanikisha utambuzi wa vinasaba katika miili hiyo na hivyo kuwawezesha ndugu wa marehemu kutambua ilipozikwa miili ya ndugu zao, Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza kwa uadilifu na uchapakazi wao katika majukumu mengine yakiwemo kutambua dawa za kulevya, kutoa ushahidi mahakamani na kufanya kazi katika mazingira yenye kemikali hatari kwa afya ya binadamu.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kununua vifaa vipya na vya kisasa, kuongeza wafanyakazi na kuibadili kutoka kuwa Wakala wa Serikali na kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wake mkubwa na kuiongezea nguvu za kufanya kazi kwa uhuru zaidi ili kupata manufaa yanayotarajiwa.

“Nafahamu kuna wakati mlikuwa mnachunguza jambo na mnaandika ripoti ya uchunguzi wenu lakini hizo ripoti zilikuwa zinazimwa kwa sababu mlikuwa hamna nguvu, sasa mna nguvu nataka mfanye kazi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, kutopokea rushwa, kutotoa siri na ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha watumishi wa ofisi hiyo wanaofanya uchunguzi wa masuala mazito wanakuwa salama na hawaingiliwi katika majukumu yao.

Amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya mamlaka hiyo Prof. Ester Hellen Jason na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinatumika kununua mahitaji mbalimbali vikiwemo vitenganishi vitumikavyo maabara.

Mapema katika taarifa yake, Dkt. Mafumiko amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa shilingi Bilioni 5.338 kwa ajili ya kununulia mitambo na kuongeza wafanyakazi kutoka 110 hadi 294 hali iliyoongeza ufanisi wa kazi ambapo kwa kipindi cha miaka 4 tangu 2015 vielelezo 204,974 vimechunguzwa sawa na wastani wa vielelezo 51,244 kwa mwaka, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 510 ikilinganishwa na rekodi za mwaka 2015/16.

Amebainisha kuwa ufanisi wa mamlaka hiyo pia umesaidia kuongeza mahudhurio mahakamani kutoka kesi 35 kwa mwezi (2015) hadi kufikia kesi 220 kwa mwezi mwaka huu (2019) na imeongeza ofisi nyingine 2 za Kanda ya Kati na Kanda ya Kusini hali iliyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Rais Magufuli ambaye amepata nafasi ya kuwasiliza wafanyakazi wa mamlaka hiyo ameahidi kufanyia kazi changamoto mbalimbali zikiwemo mahitaji ya vifaa vya kisasa zaidi vya kufanyia kazi, kuboresha maslahi ya watumishi na kuimarisha miundombinu.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

20 Agosti, 2019