Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua maadhimisho ya 4 ya wiki ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuhimiza nchi wanachama kutilia mkazo utekelezaji wa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda wa kuanzia mwaka 2015 – 2063.

Ufunguzi huo umefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wabunge, Sekretarieti ya SADC, viongozi kutoka sekta binafsi na washiriki wa maonesho ya viwanda kutoka nchi mbalimbali.

Mhe. Rais Magufuli ambaye amengozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema pamoja na kuwepo kwa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda bado kasi ya ukuaji wa viwanda ni ndogo na hivyo kusababisha viwanda kuendelea kutoa mchango mdogo katika maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za SADC.

Amebainisha kuwa nchi za SADC zimeendelea kuwa wazalishaji wa malighafi na nguvu kazi kwa ajili ya mataifa mengine huku zenyewe zikiwa waagizaji wa bidhaa za viwandani kutoka nje ilihali zikipangiwa bei ya kuuza na kununua bidhaa hizo, hali inayodidimiza wakulima na kurudisha nyuma juhudi za kupata maendeleo ya kiuchumi.

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa kutokana na kutokuwa na viwanda urari wa biashara kati ya Afrika na mabara mengine umekuwa sio mzuri na ametolea mfano wa mwaka 2017 ambapo thamani ya biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ilikuwa ni shilingi Trilioni 708 (Euro Bilioni 280) ambapo Afrika ilinunua bidhaa za shilingi Trilioni 376.7 (Euro Bilioni 149) na ikauza bidhaa za shilingi Trilioni 331 (Euro Bilioni 131), lakini asilimia 60 ya bidhaa ilizouza zilikuwa ghafi na hivyo kuwa na thamani ndogo.

“Hii inathibitisha kwamba sisi Afrika tunazalisha bidhaa ambazo hatuzitumii na tunatumia bidhaa ambazo hatuzizalishi, ni lazima tubadilishe mwelekeo huu ili tuzalishe bidhaa ghafi, tuzisindike au kutengeneza viwandani na tuzitumie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Ili kuepukana na changamoto hii inayosababisha upotevu wa fedha za kigeni, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kutekeleza kwa vitendo nguzo 3 za Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda ambazo ni kuhimiza maendeleo ya viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na kiteknolojia, kuongeza ushindani wa bidhaa za viwandani na kutumia mtangamano wa kikanda na jiografia yetu (yenye watu takribani Milioni 350) kwa maendeleo ya viwanda na uchumi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kuweka kipaumbele katika uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda vya ndani ya Jumuiya na ndani ya Afrika pamoja na kuuziana malighafi na bidhaa zingine miongoni mwa nchi wanachama ili kukuza mitaji na kuendeleza viwanda vya ndani ya SADC na Afrika nzima, kukuza na kuendeleza ubunifu wa watu wa Afrika pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta ya viwanda.

Maeneo mengine ni kuondoa vikwazo vyote vinavyochelewesha maendeleo ya sekta ya viwanda na kuhimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa za kuwekeza katika viwanda badala ya kubaki ikilalamikia changamoto inazokumbana nazo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Tanzania katika kuendeleza viwanda kuwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme ikiwemo mradi mkubwa wa kuzalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, kujenga miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na kuhamasisha ujenzi wa viwanda ambapo kati ya mwaka 2015 na sasa viwanda zaidi ya 4,000 vimejengwa.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stergomena Tax na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Salum Shamte wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa za kujenga mazingira wezeshi ya ujenzi wa viwanda hapa nchini, na wametoa wito kwa nchi zote za SADC kutilia mkazo uboreshaji wa mazingira wezeshi na wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika viwanda.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

05 Agosti, 2019