Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Juni, 2019 amekutana na wabunifu wawili wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya mito kutoka Mkoani Njombe na kuagiza wataalamu wa wizara na taasisi zinazojihusisha na sayansi, teknolojia na uvumbuzi kuwafuatilia na wabunifu na wavumbuzi mbalimbali ili kuwaunga mkono katika kuboresha kazi zao.

Wabunifu waliokutana na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam ni John Akani Fute na Jairos Ngairo ambao wamebuni miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji yanayotiririka mtoni, kusukuma maji kwa kutumia pampu zisizotumia umeme na kusaga nafaka kwa kutumia machine zinazoendeshwa na maji ya mto. Bwana Fute amebuni mradi unaozalisha kilowati 28 na Bw. Ngairo anazalisha kilowati 15 za umeme.

Mkutano huo umewahusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamis Mwinyimvua, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Ludovick Nduhiye pamoja na viongozi na wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wabunifu hao kwa kuzalisha umeme wa gharama nafuu unaowanufaisha wananchi na ameagiza TANESCO na COSTECH kuwaunga mkono ambapo TANESCO itatoa shilingi Milioni 30 na COSTECH shilingi Milioni 20 kwa wabunifu hao, na pia timu ya wataalamu itaondoka kesho kwenda Njombe ilipo miradi hiyo kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu na kuiboresha.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na vitendo vya wataalamu kuwakatisha tamaa na kuwatisha wabunifu wa vitu mbalimbali vinavyowasaidia wananchi kama ambavyo Bw. John Fute (Pwagu) na Bw. Jairos Ngairo wamekuwa wakifanyiwa na badala yake ametaka wabunifu hao waungwe mkono kwa ushauri wa kitaalamu na kuwawezesha kuongeza tija.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TBC kwa kufuatilia kazi za ubunifu na uvumbuzi kupitia makala yake ya Hadubini (Habari kwa Kina) ikiwemo makala ya ubunifu wa mradi huo wa umeme iliyoandaliwa na waandishi wa Habari Bi. Tatu Abdallah na Bi. Zaituni Mkwama na ameagiza Wizara na Taasisi za Serikali kufuatilia taarifa zinazotangazwa na vyombo vya habari na kuchukua hatua katika maeneo yanayozihusu.

Ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kufuatilia jengo la ghorofa 3 linalodaiwa kutelekezwa na raia mmoja wa kigeni huko Kunduchi Jijini Dar es Salaam ambalo limebaki mikononi mwa mlinzi ambaye anatishwa na wajanja wanaotaka kujimilikisha kwa nguvu. Taarifa hii pia ilitangazwa na TBC kupitia makala ya Hadubini.

“Nakupongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba na wafanyakazi wa TBC kwa kazi nzuri mnayoifanya, angalau nyinyi mnathubutu kujituma hadi vijijini kufuatilia mambo haya muhimu kwa jamii, nataka wizara na taasisi ambazo zina wataalamu na wasomi ziigeni mfano huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Wakizungumza katika mkutano huo, Bw. Fute na Bw. Ngairo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapa shilingi Milioni 5 ikiwa ni kutambua ubunifu wao na wameahidi kwenda kuboresha zaidi kwa kushirikiana na wataalamu wa Serikali.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

13 Juni, 2019