Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya Habari
Taarifa kwa vyombo vya Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza wafanyakazi wote kote nchini kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kazi na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha zaidi mazingira ya kazi, kupanua uwekezaji katika miradi ya maendeleo na kutatua kero za wafanyakazi ili kulinda maslahi yao.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, muda mfupi baada ya kupokea maandamano ya wafanyakazi na kusikiliza risala ya wafanyakazi iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Dkt. Yahaya Msigwa.

Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kutambua kuwa wafanyakazi wana mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi na hivyo ameridhia bodi ya mishahara kukutana ilimradi isitumie vibaya fedha za umma, kupunguza viwango vya kodi ya mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi wote na kuwajali wafanyakazi wote wakiwemo wenye elimu ya Darasa la Saba.

“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu wafanyakazi, Serikali ninayoiongoza inawapenda wafanyakazi, hata hili la wafanyakazi wa Darasa la Saba nataka kuwajulisha kuwa kati ya wafanyakazi wote 525,506 walioajiriwa na Serikali wafanyakazi 98,615 wana elimu ya Darasa la Saba, Serikali haiwabagui wafanyakazi wenye elimu ya Darasa la Saba” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameyapokea mapendekezo ya TUCTA kuhusu Serikali kutilia mkazo ujenzi wa viwanda katika maeneo ya uzalishaji wa mazao, kuwekeza zaidi katika uchumi wa bahari ikiwemo kununua meli kubwa za uvuvi katika bahari kuu na kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza uwigo wa ajira na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yatawanufaisha Watanzania wote wakiwemo wafanyakazi.

Pamoja na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo hayo, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuelekeza fedha nyingi katika miradi itakayochochea uchumi na kuwanufaisha Watanzania wote wakiwemo wafanyakazi na ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Ujenzi wa reli ambao utagharimu shilingi Trilioni 7.026 (kati ya Dar es salaam na Dodoma), kuanza ujenzi wa mradi wa umeme wa mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,100 kwa gharama ya shilingi Trilioni 6.5 na ununuzi wa ndege 8 kwa ajili ya kukuza utalii na kurahisisha usafiri.

Maeneo mengine yaliyoelekezewa fedha nyingi ni kukarabati na kujenga meli mpya katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa gharama ya shilingi Bilioni 287.9, kupanua bandari 3 za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kwa gharama ya shilingi Trilioni 1.2 na kupanua viwanja vya ndege 11.

“Na kwa taarifa yenu jana (tarehe 30 Aprili, 2019) Benki ya Maendeleo Afrika – AfDB imeidhinisha mkopo kwa Tanzania shilingi Bilioni 415.3 zitakazotumika kujenga kilometa 110 kuzunguka Jiji la Dodoma na itakuwa ni barabara ya njia nne” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeamua kuelekeza fedha nyingine nyingi katika miradi ya huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 uliogharimu shilingi Bilioni 105, kujenga na kukarabati Vituo vya Afya 352 kwa shilingi Bilioni 184.67 na vifaa vyake vya shilingi Bilioni 41.6 pamoja na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi 270.

Miradi mingine ni maji ya Ziwa Victoria kwenda Miji ya Nzega, Igunga, Tabora na Sikonge pamoja na mradi wa maji wa Jiji la Arusha yote ikigharimu shilingi Trilioni 1 na mradi wa maji katika Miji 28 hapa nchini utakaogharimu shilingi Trilioni 1.2.

Na katika elimu, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatoa shilingi Bilioni 23.8 kila mwezi kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo, imeongeza mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi Bilioni 365 hadi 473 na fedha nyingine nyingi kuelekezwa katika miradi ya kusambaza umeme, kilimo, ufugaji na mawasiliano.

Kwa upande wa wafanyakazi, Mhe. Rais Magufuli amesema baada ya uhakiki kufanyika Serikali imetoa nyongeza ya mshahara ya shilingi Bilioni 72.8 kwa wafanyakazi 505,985, imelipa malimbikizo ya mishahara ya shilingi Bilioni 75.5 kwa wafanyakazi 50,386, imelipa shilingi Bilioni 29.5 kwa wafanyakazi 118,989 waliopandishwa madaraja, imelipa shilingi Bilioni 291.3 kwa madai ya wafanyakazi yasiyo ya mshahara na kwamba wafanyakazi wengine 193,166 watapandishwa madaraja mwaka ujao wa fedha.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeinusuru mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kulipa deni la shilingi Trilioni 1.5 ambazo Serikali haikuwa inawasilisha kwa mifuko hiyo tangu mwaka 2012, imeridhia kuendelea na kikokotoo cha zamani kwa malipo ya wafanyakazi wanaostaafu ambao ni mzigo mkubwa na kwamba pamoja na hayo yote pia imewajengea walimu nyumba 11,077, watumishi wa wizara ya afya nyumba 301 na katika mwaka ujao wa fedha itaajiri wafanyakazi wapya 45,000.

Kufuatia majukumu hayo mazito Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyakazi kuwa na subira katika ombi lao la kuongezewa mishahara na ameahidi kuwaongezea mishahara hiyo kabla hajamaliza kipindi chake cha uongozi.

“Nawasihi ndugu wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuiletea maendeleo nchi yetu, Wazee wetu wa zamani walijitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kisiasa, ni jukumu letu kizazi cha sasa kujitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kiuchumi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Sherehe za Mei Mosi mwaka huu zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassa, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Mabalozi, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila.

Kesho, Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atafungua Hospitali ua Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) na kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbarali katika uwanja wa Barafu Mjini Rujewa.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Mbeya

01 Mei, 2019