Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 Aprili, 2019 ameanza ziara yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani Njombe akitokea Mkoani Ruvuma ambapo amezindua Kituo cha Afya cha Madaba Wilayani Songea na amefungua kiwanda cha chai cha Kabambe kilichopo Lwangu Mjini Njombe.

Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Madaba Wilayani Songea umehusisha jengo la wodi ya wazazi, maabara, jengo la upasuaji, nyumba ya mtumishi, chumba cha kuhifadhi maiti, kichomeo cha taka na vifaa tiba kwa gharama ya shilingi Milioni 665.5 fedha ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Pamoja wa Wadau wa Sekta ya Afya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya na ametaja baadhi ya mafanikio kwa Mkoa wa Ruvuma kuwa ni kuongezeka kwa bajeti ya dawa kutoka shilingi Milioni 845 hadi kufikia shilingi Bilioni 3 na kuongezeka kwa idadi ya akina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya tiba kutoka asilimia 63 hadi 82.

Mhe. Ummy Mwalimu amewashukuru wadau wa huduma za afya kwa kuendelea kuchangia shilingi Bilioni 130 kila mwaka na kubainisha kuwa wiki iliyopita wametoa sehemu ya fedha hizo kiasi cha shilingi Bilioni 50 ambazo zimesambazwa katika vituo vya tiba kwenye Mikoa yote hapa nchini kupitia utaratibu mpya wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo husika.

Mbunge wa Jimbo la Madaba Mhe. Joseph Mhagama amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa jinsi Serikali inavyowahudumia wananchi wake na amebainisha kuwa vijiji vyote vya Jimbo hilo isipokuwa vitatu vimepatiwa umeme, vituo vya afya 2 vimepatiwa shilingi Milioni 900 na miradi mingine ya maji yenye thamani ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 900.

Akizungumza na wananchi wa Madaba katika sherehe za uzinduzi wa kituo chao cha afya, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wadau wa afya wote waliochangia ujenzi wa kituo hicho na pia amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Songea kwa kusimamia vizuri ujenzi.

Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi na watumishi wa Wizara ya Afya kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi zinaelekezwa katika miradi husika na amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inaimarisha huduma za afya kwa Watanzania wote.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayochangia katika Mfuko wa Pamoja wa huduma za Afya hapa nchini na kwa niaba yao Balozi wa Denmark hapa nchini Mhe. Einar Jensen ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutilia mkazo huduma za afya ikiwemo kujenga hospitali mpya 67 na vituo vya afya 352 ambapo 210 kati yake vimechangiwa na mfuko huo.

Mkoani Njombe ziara ya Mhe. Rais Magufuli imeanza kwa kufungua kiwanda cha chai cha Kabambe kinachomilikiwa na kampuni ya Unilever Tanzania katika eneo la Lwangu Mjini Njombe.

Kiwanda hiki ambacho kilianza kujengwa Januari 2017 kinasindika tani 50 za chai kwa siku (na kina uwezo wa kusindika hadi tani 150), kimeajiri wafanyakazi 700 na kinawahudumia wakulima wadogo wa chai 3,000.

Mkurugenzi Mtendaji wa Unilever Tanzania Bw. David Minja amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kiwanda hicho ni moja ya viwanda vya Unilever Tanzania vilivyoajiri Watanzania 7,000 na kuwanufaisha watu 40,000 na kwamba Unilever Tanzania imewekeza kiasi cha shilingi Bilioni 49.6 katika viwanda na hivyo kuunga mkono sera ya viwanda.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Joseph Kakunda amesema kiwanda hicho ni kati ya viwanda 36 vya chai hapa nchini na ni kati ya viwanda 108 vilivyoanzishwa katika mwaka 2018/19.

Mwekezaji wa kiwanda cha chai cha Kabambe Sir Ian Wood kutoka Wood Foundation amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukifungua kiwanda hicho na amesema anaamini kiwanda hicho kitasaidia kuinua kipato cha wakulima kama ambavyo viongozi wa Njombe wakiwemo viongozi wastaafu walimuomba kuwekeza.

Akizungumza baada ya kufungua kiwanda na kujionea mitambo ya kisasa ya kusindika chai inavyofanya kazi, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Unilever Tanzania kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa wakulima wa Mkoa wa Njombe kuongeza uzalishaji wa chai kutoka asilimia 20 ya chai wanayopeleka kiwandani hapo hivi sasa hadi kufikia asilimia 70 iliyopangwa kutoka kwa wakulima wadogo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekemea tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakiwakwamisha wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda na amemuomba Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kumjulisha pale watakapobaini mwekezaji amekwamishwa.

“Ndio maana nimeamua kuitoa TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kuipeleka Ofisi ya Waziri Mkuu, na huko nako nikiona mambo hayaendi nitaitoa na kuileta ofisini kwangu, nataka mtu anayetaka kuwekeza akija leo, kesho aoneshwe eneo la kujenga kiwanda, sio kumzungushazungusha” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea furaha yake ya kuona Tanzania ya Viwanda inafanikiwa ambapo katika kipindi cha miaka 3 viwanda 3,500 vimejengwa na Watanzania wengi wanaendelea kupata ajira.

Kesho tarehe 10 Aprili, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Njombe ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na ataweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Njombe – Makete na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.  

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Njombe

09 Aprili, 2019