Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe  Magufuli tarehe 30 Novemba, 2018 amekutana na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta kando ya Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Mara baada ya kikao cha ndani kilichofanyika katika moja ya kumbi za watu mashuhuri ndani ya kituo cha AICC, Marais wote watatu wamesafiri kwa gari moja hadi Ikulu ndogo ya Arusha Mjini ambako Mhe. Rais Magufuli amewaalika wageni wake kwa chakula cha mchana.

Baada ya chakula cha mchana Mhe. Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeahirishwa hadi tarehe 27 Desemba, 2018 utakapofanyika tena.

Mhe. Rais Museveni amesema mkutano huo umeahirishwa kutokana na mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo ambaye ni nchi ya Burundi kutohudhuria, ilihali mkataba wa jumuiya hiyo unataka maamuzi yafanywe na wanachama wote kwa pamoja.

“Tuliamua kuahirisha mkutano kwa leo kwa sababu mmoja wetu ambaye ni Burundi hakuja, tumeahirisha mkutano mpaka tarehe 27 Desemba, 2018 wakati sisi wote tutakapokuwepo, kwa sababu mkataba wa Afrika Mashariki unasema mambo mawili, moja lazima tuwe na mkutano mmoja wa kawaida kila mwaka na ndio huu wa leo.

Lakini vile vile uamuzi wowote utakaofanyika lazima wanachama wote wawepo, kwa hiyo kama mmoja hayupo sio vizuri kuendelea, inakuwa inakwenda kinyume na mkataba” amesema Mhe. Rais Museveni.

Akiwa hapa Arusha kesho tarehe 01 Desemba, 2018 Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta watafungua kituo cha huduma za pamoja mpakani (One Stop Border Post) katika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

30 Novemba, 2018