Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya habari
Taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Julai, 2018 ameongoza mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL).

Mapokezi ya ndege hiyo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Wabunge, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Wakuu wa Mikoa, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa, wadau wa usafiri wa anga wakiwemo wafanyabiashara na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.

Ndege hiyo imewasili majira ya saa 11:10 jioni katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, kisha kupewa heshima ya kumwagiwa maji (Water Salute) na baadaye Mhe. Rais Magufuli akiwa na viongozi wakuu walioambatana nae akaizindua rasmi na kuikagua kwa kuingia ndani ya ndege ili kujionea mandhari ya ndani.

Akizungumza kabla ya kuwasili kwa ndege hiyo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania kwa kuchapa kazi na kulipa kodi, na hivyo kuiwezesha Serikali kupata fedha za kutekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa ndege kwa ajili ya kuimarisha ATCL ambayo ilikuwa na hali mbaya.

“Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya sana, lilikuwa na ndege moja tu tena ilikuwa inafanyiwa matengenezo mara kwa mara, soko la ATCL lilishuka sana hadi kufikia asilimia 2.5, lakini sasa tumenunua ndege 7, hii ni ndege ya 4 na nyingine mbili zitakuja kabla ya mwaka huu kuisha, na nyingine kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner itakuja mwaka 2020.

“Tangu tumeongeza ndege 3 mpya aina ya Bombardier Q400 biashara ya ATCL imeongezeka, Shirika letu lilikuwa linasafirisha abiria 4,000 tu kwa mwezi lakini sasa linasafirisha abiria 21,000 na ndege zinatua katika vituo 12” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Serikali iliamua kuchukua hatua ya kulinusuru Shirika la Ndege la Taifa ili kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa, kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.

Mapema akitoa taarifa ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyowasili hapa nchini leo, Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho amesema ndege hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 262, itaanza kutoa huduma kwa safari za ndani katika vituo vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza, mwezi Septemba itaanza safari zake kwenda Bombay nchini India, Guangzhou nchini China na Bangkok nchini Thailand na kwamba utaratibu umeanza ili ifanye safari za kwenda Uingereza na miji mingine duniani.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe.  Inmi Petterson amewapongeza Watanzania kwa mafanikio makubwa ya kununua ndege hiyo kutoka nchini Marekani na amesema hiyo ni hatua muhimu ya Tanzania kujenga uchumi wake.

Viongozi wa Dini waliohudhuria katika tukio hili wameongoza dua ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio haya makubwa na kuliombea Taifa pamoja na Mhe. Rais Magufuli katika majukumu yake ya kuongoza juhudi za kuleta maendeleo.

Katika sherehe hizo Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi amekabidhi ndege hiyo ya Serikali kwa Katibu Mkuu wa Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho kwa ajili ya kuikodisha ATCL ili kuanza kuitumia.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

08 Julai, 2018