Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya habari
Taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 01 Julai, 2018 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kufanya uteuzi wa Waziri mmoja, Naibu Mawaziri wawili na kuwabadilisha wizara Mawaziri wawili.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi Ikulu Jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa pamoja na mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Mhe. Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa taasisi na idara za Serikali.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Kangi Alphaxard Lugola (Mbunge wa Jimbo la Mwibara) kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Lugola alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Mussa Ramadhani Sima (Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini) kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Mazingira.

Kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo, Mhe. Rais Magufuli ameamua kuongeza nguvu katika usimamizi wa sekta hiyo kwa kuongeza Naibu Waziri mmoja ambapo amemteua Mhe. Omary Tebwete Mgumba kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Mhe. Mgumba ni Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewabadilisha wizara Mawaziri wawili ambapo aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amehamishiwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, na aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe amehamishiwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mhe. Rais amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuu wanne kama ifuatavyo.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Moses Mpogole Kusiluka kuwa Katibu Mkuu Ikulu, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Alphayo Kidata ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Kusiluka alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Rashid Adam Tamatamah kuwa Katibu Mkuu Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kujaza nafasi iliyoachwa na Dkt. Yohana Budeba ambaye amestaafu.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Tamatamah alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tanzania Fisheries Research Institute – TAFIRI).

Mhe. Rais Magufuli amemteua Mej Jen. Jacob Kingu kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mej Jen. Mstaafu Projest Anatory Rwegasira ambaye amestaafu.

Kabla ya uteuzi huo, Mej Jen. Kingu alikuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College – NDC).

Mhe. Rais Magufuli amemteua Balozi Joseph Edward Sokoine kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Butamo Kasuka Phillipo ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kabla ya uteuzi huo Balozi Sokoine alikuwa Balozi wa Tanzania, Brussels nchini Ubelgiji.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Ramadhani Kailima kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kabla ya uteuzi huo Bw. Kailima alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (National Electoral Commission - NEC).

Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Siza Donald Tumbo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Thomas Didimu Kashililah ambaye amestaafu.

Kabla ya uteuzi huo Prof. Tumbo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Vifaa vya Kilimo na Teknolojia (Center for Agriculture Mechanisation and Rural Technology – CAMATEC).

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Mathias Bazi Kabunduguru kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kabla ya uteuzi huo Bw. Kabunduguru alikuwa Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Sera, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Hassan Simba Yahaya kuwa Balozi, kituo chake cha kazi kitatangazwa baadaye.

Kabla ya uteuzi huo Balozi Hassan Simba Yahaya alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Athumani Juma Kihamia kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Ramadhani Kailima ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kabla ya uteuzi huo Bw. Kihamia alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama ifuatavyo.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Jaji Mbarouk Salim Mbarouk kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, kujaza nafasi iliyoachwa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Hamid Mahmoud Hamid.

Makamishna wengine wa NEC walioteuliwa ni Mhe. Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na Mhe. Balozi Omar Ramadhani Mapuri.

Tarehe ya kuapishwa kwa wateule wote itatangazwa baadaye.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

01 Julai, 2018