Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya habari
Taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 08 Januari, 2018 amemuapisha Mhe. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini na kuiagiza Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kanuni za sheria mpya ya madini namba 7 ya mwaka 2017 inasainiwa ifikapo Ijumaa tarehe 12 Januari, 2018.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya Mhe. Biteko kuapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na ameelezea kutoridhishwa kwake na namna viongozi na watendaji wa Wizara ya Madini wanavyotekeleza majukumu yao polepole na bila kujali maslahi ya nchi.

“Sheria hii imepitishwa na Bunge na mimi nikaisaini tangu mwezi wa 7 mwaka 2017, mpaka leo ni miezi 7 bado hamjasaini kanuni zake ili sheria ianze kutekelezwa, na wahusika wote wapo, yaani mpaka leo hamjaelewa Watanzania wanataka nini? amesema Mhe. Rais Magufuli.

Amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi kushirikiana na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wanaohusika katika Wizara ya Madini kuhakikisha kanuni hizo zinasainiwa.

Pamoja na maagizo hayo Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Kamishna wa Madini Mhandisi Benjamin Mchwampaka na amemteua Prof. Shukrani Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini.

Kabla ya uteuzi huu Prof. Shukrani Elisha Manya alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Jiolojia.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbolea inafikishwa katika mikoa yote ya uzalishaji wa chakula ukiwemo mkoa wa Rukwa ifikapo Ijumaa tarehe 12 Januari, 2018.

Mhe. Rais Magufuli amemuelekeza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kufuatilia jambo hilo na amebainisha kuwa endapo mbolea haitafikishwa katika maeneo hayo ifikapo Ijumaa wahusika waachie ngazi.

“Wakulima wanataka mbolea na muda ni huu, inasikitisha sana, fedha kwenye bajeti zimetengwa lakini mpaka leo mbolea haijawafikia wakulima, sasa Mkoa kama Rukwa ndio tunaoutegemea kwa chakula, Waziri yupo na watendaji wake wapo lakini mpaka leo mbolea haijapelekwa, wakulima watazalishaje chakula?” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amewataka watendaji wote wa Serikali kutekeleza majukumu yao ipasavyo na ameonya kuwa hatosita kumfukuza kazi mtendaji yeyote atayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.

“Nataka kila mmoja afanye kazi, Watanzania wanataka maendeleo, hakuna muda wa kubembelezana, kila mmoja afanyie kazi mambo yanayomhusu asisubiri kuambiwa, kule bandarini niliunda timu za kuchunguza madudu yaliyopo huko naambiwa kuna makontena 178 ya makinikia hayana mwenyewe, mengine yapo Ubungo, mengine bandari” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri wanayoifanya zikiwemo kamati zinazoundwa kuchunguza mambo mbalimbali na amekiri kuwa Bunge limekuwa likiisaidia sana Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Hafla ya kuapishwa kwa Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Mashaka Biteko imehudhuriwa na Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai na viongozi mbalimbali wa Wizara na vyombo vya ulinzi na usalama.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

08 Januari, 2018