Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

Taarifa kwa vyombo vya habari
Taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya kutunzia magari ndani bandari ya Dar es Salaam na kubaini uwepo wa magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 ambayo yamekwama bandarini hapo tangu tarehe 29 Juni, 2015 na magari ya Jeshi la Polisi 53 ambayo yamekwama tangu Juni 2016.

Mhe. Rais Magufuli pia amebaini uwepo wa magari yaliyotekelezwa bandari hapo kwa zaidi ya miaka 10 hali inayopunguza uwezo wa bandari kuhifadhi mizigo.

Kufuatia hali hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 7 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Jeshi la Polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari hayo kukwama bandarini hapo kwa muda mrefu na kinyume cha sheria, na pia ameagiza magari yote ambayo yamekaa bandarini hapo kwa muda mrefu yaondolewe kwa taratibu za kisheria na kwa uwazi.

“Nataka magari yote yaliyokaa muda mrefu kupita muda uliopangwa kisheria yaondolewe haraka, kama ni kupigwa mnada yapigwe mnada, kama ni kuchukuliwa na Serikali yachukuliwe, hatuwezi kuendelea kutunza magari ya watu humu kwa miaka 10 tena watu wengine hawajulikani” ameagiza Mhe. Rais Magufuli.

Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna Valentino Mlowola kufanya uchunguzi kwa magari yote yaliyokwama bandarini hapo baada ya kuagizwa kwa majina ya taasisi za Serikali na kuwabaini wote walioshiriki katika uingizaji.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, amewataka Mawaziri hao kufuatilia utendaji kazi wa vyombo na taasisi wanazozisimamia na kuchukua hatua kwa wakati pale wanapobaini uwepo wa mambo yasiyofaa.

Mapema kabla ya kufanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya utunzaji wa magari yaliyokaa bandarini hapo kwa muda mrefu Mhe. Rais Magufuli ametembelea meli ya Jeshi la Jamhuri ya Watu wa China iitwayo Peace Ark ambayo tangu tarehe 20 Novemba, 2017 ilikuwa ikitoa huduma za matibabu ya bure kwa wananchi.

Meli hiyo ambayo ni hospitali yenye vifaa vyote vya uchunguzi na dawa ina madaktari 115, wauguzi na wafanyakazi wengine 266 na vitanda vya kulaza wagonjwa 300, kwa muda wa wiki 1 imetoa huduma za matibabu kwa wagonjwa 6,421 wakiwemo 31 waliofanyiwa upasuaji. Meli hiyo imeondoka nchini leo.

Kamanda anayeongoza timu ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika meli hiyo Guan Bailin amesema meli hiyo imekuja kwa mara ya pili nchini Tanzania na kwamba China inafanya hivyo kwa kutambua uhusiano na ushirikiano mzuri, wa kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na China na kwamba meli hiyo inaweza kuja tena endapo Tanzania itahitaji.

Akizungumza baada ya kutembelea vitengo mbalimbali ya uchunguzi na matibabu ndani ya meli hiyo Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya China kwa kuleta meli na kutoa matibabu kwa idadi kubwa ya wananchi na amesema Tanzania inaikaribisha kwa wakati mwingine wowote ili isaidie juhudi za kutoa matibabu kwa wananchi.

Mhe. Rais Magufuli amemkabidhi Kamanda wa meli hiyo Guan Bailin barua ya shukrani kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping yenye shukrani zake kwa ujio wa meli hiyo, na pia amemuomba Mhe. Rais Xi Jinping kuisadia Tanzania kupata meli kama hiyo na kuendelea kuwaleta madaktari kutoka China.

“Kwa wiki moja mmetoa matibabu kwa wananchi 6,421 lakini nimeambiwa waliojiandikisha walikuwa zaidi ya 10,000 hii inaonesha kuwa kuna mahitaji makubwa ya matibabu, kwa hiyo natoa wito kwa ndugu zetu wa China mje muwekeze katika ujenzi wa vituo vya tiba hapa Tanzania” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Amewashukuru madaktari wa China waliotoa huduma kwa wiki nzima pamoja na madaktari wa hapa nchini walioshirikiana nao, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda kwa kusimamia zoezi hilo na ametaka Wakuu wa Mikoa yote nchini waige mfano wa Bw. Makonda kuwapenda na kuwapigania wananchi wao.

Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jen. Venance Salvatory Mabeyo, Mawaziri na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

 

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

26 Novemba, 2017