Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na Watanzania waishio nchini Uganda katika Mji wa Masaka na kuwahakikishia kuwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mabadiliko zimeanza kuzaa matunda.

Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Mawaziri na viongozi wakuu wa taasisi za Serikali ametaja baadhi ya matokeo hayo kuwa ni kusimamia vizuri uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 5.1, kuokoa Shilingi Bilioni 238 walizokuwa wanalipwa watumishi hewa kwa mwaka na kuondoa watumishi wenye vyeti feki waliokuwa wakilipwa Shilingi Bilioni 142 kwa mwaka.

Matokeo mengine ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi Bilioni 850 hadi wastani wa Shilingi Trilioni 1.2 kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726 ambapo Shilingi Trilioni 7 zitatumika, kununua ndege 6 za Serikali kwa ajili ya kuinua utalii na kuimarisha usafiri wa anga, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi 269.

Mhe. Rais Magufuli pia amesema Serikali imechukua hatua madhubuti za kuwavutia wawekezaji na sasa wengi wapo katika hatua mbalimbali za uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda na ametoa wito kwa Watanzania hao kuendelea kuwashawishi wawekezaji wengine kwenda kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa fursa zipo nyingi.

Katika mkutano huo Watanzania waishio Uganda wamemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi mbalimbali anazozifanya na wameomba Serikali iwajengee mazingira bora pale wanapowapeleka wawekezaji nchini Tanzania.

Pamoja na Mhe. Rais Magufuli kuahidi kufanyia kazi maoni ya Watanzania hao, Mawaziri waliokuwa wakijibu hoja mbalimbali zilizotolewa wamewataka kutosita kuwasiliana nao pale wanapokuwa na jambo linalohitaji majibu ya Serikali.

Huu ni mkutano wa kwanza wa Mhe. Rais Magufuli kukutana na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), na Uganda kuna Watanzania 45,000 waishio nchini hapa.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Masaka, Uganda

10 Novemba, 2017