Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Septemba, 2017 amemuapisha Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Prof. Ibrahim Hamis Juma anakuwa Jaji Mkuu wa nane baada ya uhuru na hafla ya kuapishwa kwake imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai.

Akizungumza baada ya kumuapisha, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma na Majaji wengine wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kwa kazi kubwa wanayofanya, na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa mhimili huo wa dola ikiwa ni pamoja kukabiliana na changamoto mbalimbali kulingana na uwezo wa kibajeti.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Jaji Mkuu, Majaji na Mahakimu wote wa mahakama nchini kuongeza kasi ya kufanyia kazi changamoto mbalimbali za mahakama ikiwemo ucheleweshaji wa kesi, na zaidi amewataka kuongeza msukumo katika kushughulikia tatizo la rushwa.

“Na ndio maana nimechukua muda mrefu kuteua Jaji Mkuu, kwanza nilitaka niteue Jaji Mkuu atakayekaa muda mrefu, sio baada ya miaka miwili nilazimike kuteua tena Jaji Mkuu, na pili nilitaka nijiridhishe huyu nitakayemteua ataweza kupambana na rushwa? Maana rushwa imetapakaa kila mahali, Serikalini kuna rushwa, Mahakamani kuna rushwa” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amesema hakumteua Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa shinikizo la mtu yeyote na hivyo ametaka yeye pamoja na Majaji na Mahakimu wa mahakama nchini wafanye kazi kwa kutanguliza maslahi ya wananchi na Maslahi ya Taifa.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amemshukuru Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman kwa utumishi wake na ametoa wito kwa Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma kutosita kuwatumia Majaji Wakuu wastaafu ili kuendelea kupata uzoefu wao.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na ameahidi kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba huku akiwatoa hofu wananchi kuwa hakuna mgongano wowote katika mihimili ya dola hapa nchini, kwani kila mhimili una majukumu yake ya kuwasaidia wananchi.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

11 Septemba, 2017