Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  tarehe 10 Agosti, 2017 amekutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Mhe. Patricia Scotland ambaye amemueleza juu ya mipango na mikakati mbalimbali ambayo Jumuiya hiyo inaiweka kwa lengo la kuhakikisha nchi wanachama zinanufaika na kuwemo kwao ndani ya Jumuiya hiyo.

Mhe. Patricia Scotland ametaja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni kuongeza fursa ya kufanya biashara miongoni mwa nchi wanachama kutoka asilimia 19 ya sasa hadi kufikia asilimia 30, kuwasaidia wanawake na vijana na kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana ambao idadi yao ni wastani wa asilimia 60 ya watu wote, kutunza mazingira na kutumia ipasavyo fursa ya ukanda wa bahari kwa wanachama wake.

“Mhe. Rais tunaona kuna kila sababu ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kujiimarisha, tunazo fursa nyingi za kutuwezesha kutoka hapa tulipo na kuwa na umoja ambao una manufaa makubwa kwa wanachama wake, tunataka hili kundi kubwa la vijana ambalo kwa hapa Tanzania nimeambiwa ni asilimia 65 ya idadi ya watu wote, lipate matumaini na kuzalisha zaidi” amesema Mhe. Patricia Scotland.

Mhe. Patricia Scotland amesema wakati uchumi wa dunia ukikua kwa wastani wa asilimia 2, Bara la Afrika na Asia ambako kuna wanachama wengi wa Jumuiya ya Madola uchumi wake unakuwa kwa asilimia kati ya 5 na 8 na kwamba hii inatoa fursa zaidi kwa wanachama wa Jumuiya hii kupiga hatua na ametaja maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi kuwa ni miundombinu na nishati.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Patricia Scotland kwa jitihada hizo na amemhakikishia kuwa Serikali yake inaunga mkono na ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kukuza biashara na uwekezaji.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Rais wa Mashirika ya Kipapa kutoka Vatican Mhashamu Baba Askofu Protas Rugambwa ambapo pamoja na kufanya nae mazungumzo amemkabidhi zawadi ya sanamu ya Bikira Maria wa Fatima na Rozari takatifu kutoka Vatican kwa ajili ya kufanyia ibada.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

10 Agosti, 2017