Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU


Simu : +255-22-2114512, 2116898

Email : press@ikulu.go.tz

Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi : 255-22-2113425

OFISI YA RAIS,

IKULU,

1 BARABARA YA BARACK OBAMA,

11400 DAR ES SALAAM,

TANZANIA


Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kukabiliana na uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo leo tarehe 15 Aprili, 2017 amefungua mabweni mapya ya wanafunzi wa chuo hicho yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840.

Mhe. Rais Magufuli alitoa ahadi ya kujenga mabweni hayo tarehe 02 Juni, 2016 na ujenzi ukaanza tarehe 01 Julai, 2016 ambapo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wamejenga majengo 20 yenye ghorofa 4 kila moja kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10, na pia wamejenga uzio wa kuzunguka majengo hayo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimenunua vitanda, makabati, meza, viti na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wote 3,840.

Sherehe za ufunguzi wa majengo hayo zimefanyika ndani ya eneo la mradi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Mawaziri, Wabunge, Makatibu Wakuu, Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala na Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO) Bw. Erasmi Leon wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake tena kwa muda mfupi wa chini ya miezi 8, na wamemuhakikishia kuwa Jumuiya ya chuo hicho inamuunga mkono katika jitihada zake za kujenga Tanzania imara chini ya kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

Pamoja na kuelezea furaha yake ya kufanikiwa kwa ujenzi wa mabweni hayo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TBA na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuharakisha ujenzi huo na kwa gharama nafuu, na ametaka mradi huo uwe mfano wa kuigwa kwa miradi mingine itakayotekelezwa nchini kote.

“Nilipowaambia wataalamu wanipe makadirio ya gharama za ujenzi wa mradi huu waliniambia utagharimu kati ya Shilingi Bilioni 150 hadi 170, nikamuita Mtendaji Mkuu wa TBA Bw. Mwakalinga nikamuambia kuna Bilioni 10 za kujenga mabweni haya.

“Sasa naambiwa kwenye miaka ya 2000 kulijengwa mabweni ya wanafunzi kule Mabibo, mabweni yale yanachukua wanafunzi 4,000 na yaligharimu Shilingi Bilioni 27, sisi hapa tumejenga mabweni mwaka 2017 yanachukua wanafunzi 3,840 na yamegharimu Shilingi Bilioni 10, sasa hapo mtapiga mahesabu wenyewe” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza wanafunzi watakaoishi katika mabweni hayo mapya walipie Shilingi 500/= kwa siku badala ya Shilingi 800/= na amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwapigania wanyonge na masikini kwa kuhakikisha wanapata haki ya elimu ikiwemo mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Mhe. Rais Magufuli amekubali mwaliko wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wa kwenda kufungua Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lakini ameagiza chuo hicho kitakapofunguliwa wanafunzi wote wanasomea masomo ya tiba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wahamishiwe Mloganzila.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kuwajengea nyumba wakazi wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambapo leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 644 za wakazi hao waliovunjiwa nyumba zao na kubaki bila makazi.

Mhe. Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuwajengea nyumba wakazi hao tarehe 09 Septemba, 2016 na ujenzi ukaanza tarehe 01 Oktoba, 2016 ambapo TBA inaendelea na kazi ya kujenga majengo matano yenye ghorofa 8 na 9 na yatakayokuwa na jumla ya nyumba 652, majengo ya biashara na bustani vitakavyokamilika mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 20.

Mhe. Dkt. Magufuli amepongeza maendeleo ya ujenzi huo na baada ya kuelezwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa kuna maeneo mbalimbali nchini yenye nyumba zaidi ya 5,000 zilizo katika maeneo kama Magomeni Kota, ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya kuwapatia makazi bora wananchi kwa kuwajengea nyumba katika maeneo hayo.

“Nyumba hizi zikikamilika wapatieni hawa wakazi wa Magomeni Kota waliovunjiwa nyumba wakae bure kwa miaka mitano na baada ya hapo ndipo muwauzie kwa utaratibu mtakaouweka, lakini Mhe. Lukuvi najua nchi nzima kuna maeneo yana nyumba kama hizi za Magomeni kota 5,331 nilishaagiza nyumba hizo zirudishwe Serikalini na wewe mwenyewe umeahidi kuwa utaleta hati zake mwezi ujao, siku zote tulikuwa tunajenga nyumba kwa ajili ya wafanyakazi, sasa tutaanza kujenga nyumba kwa ajili ya watanzania, uwe mfanyakazi, uwe muuza chipsi uwe nani una haki ya kupata nyumba” amesema Mhe. Rais Magufuli.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

15 Aprili, 2017